Jopo la madaktari wa hospitali ya Wilaya ya Kiteto limefanikiwa kuokoa maisha ya Sinyati Parla mwenye umri wa miaka 33 aliyekaa na mimba ya mtoto aliyefia tumboni kwa miaka mitano.
Upasuaji huo ulifanyika mwishoni mwa wiki katika hospitali hiyo baada ya mwanamke huyo kulazwa na kufanyiwa uchunguzi na kubainika ana uvimbe mkubwa tumboni na alipofanyiwa upasuaji alikutwa na mtoto mfu.
Dk. Leadry Malisa aliyefanya upasuaji huo akishirikiana na wenzake alisema walifanikiwa kutoa maiti ya mtoto wa kiume aliyekaa tumboni kwa miaka mitano.
“Haikuwa rahisi kama tulivyozoea upasuaji wa kawaida, lakini kwa mapenzi ya Mungu tulifanikiwa na hali ya mgonjwa inaendelea vizuri ,tunaamini atapona na kuendelea na shughuli zake” Malisa.
Hata hivyo jopo hilo la madaktari lilisema upasuaji huo ulikuwa wa aina yake na wa kihistoria kutokea Wilayani humo na tukio kama hilo halijawahi kutokea tangu hospitali hiyo ifunguliwe mwaka 1974.
Mimba hiyo ilikuwa ya nne kwa mama huyo na watoto watatu aliojifungua awali walizaliwa salama na wakiwa na afya njema.
JAMBOLEO
Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila amesema Chama cha CCM hakina mgombea anayefaa kuwania Urais mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo alisema iwapo UKAWA itashindwa Kushinda kiti cha Urais, Ubunge na Udiwani hawataweza kushinda tena kwa miaka inayokuja.
Alisema tangu kufariki kwa baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, CCM imepoteza imani kwa wananchi wake na hakuna mtu wa kurejesha imani hiyo tena.
Alisema wakati wa Nyerere aliweza kubadilisha upepo wa wananchi kuacha kumchagua Augustine Mrema na kumchagua Benjamini Mkapa.
Alisema wakati wa Ukawa kufanya maajabu kupitia uchaguzi mkuu umefika na kwani mpaka sasa CCM haina mgombe anayeweza kuwa sahihi kuwakilisha chama hicho katika nafasi ya Urais.
“Napenda kuweka wazi kuwa wakati wa upinzani kuingia ikulu ni huu,, kwani kiuhalisia CCM haina mtu wa kumsimamsha kuwania Urais na ndio maana hadi leo wameshindwa kutaja mgombea wao” Kafulila
MWANANCHI
Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu jana alichafua hali ya hewa bungeni baada ya kudai kuwa Serikali ya Awamu ya Nne ni ya kichovu, kauli ambayo ilizua mabishano makali kati yake na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama.
Akichangia Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2015/16, Lissu alisema Serikali hiyo imeshindwa karibu kila jambo, ikiwamo uandikishaji wa wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Alisema uchovu huo pia umejidhihirisha wazi baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kueleza kwamba mpaka sasa haijapewa fedha za maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, wakati imebaki miezi mitano ufanyike.
Lissu alivutana na Spika Anne Makinda pale alipotakiwa kukaa chini kumpisha Mhagama azungumze baada ya kugoma kwa maelezo kuwa waziri huyo ameingilia wakati akitoa ufafanuzi wa uchovu wa Serikali.
Mvutano huo ulianza Lissu alipokuwa akisema kuwa mbali na kukwama kwa uandikishaji katika Daftari la Wapigakura, hata katika upigaji wa kura za kupitisha Katiba Inayopendekezwa katika Bunge Maalumu la Katiba, marehemu, mahujaji na wagonjwa ni miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo waliopiga kura.
“Hata Uchaguzi Mkuu mpaka sasa Serikali haijatoa fedha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, hakuna maandalizi yoyote. Hatukubali kuona Serikali hii ikijiongezea muda kwa kisingizio hicho,” Lissu.
Kauli hiyo ilimwinua Mhagama na kueleza kuwa katika Bunge la Katiba zilipigwa kura halali, huku akifafanua jinsi Serikali ilivyofanya shughuli nyingi za maendeleo.
“Mheshimiwa Spika, Lissu analidanganya Bunge. Kauli zake ni za kuudhi namwomba asiendee kupotosha umma,” alisema Mhagama huku Lissu akisisitiza kauli yake.
Wakati Mhagama akisimama kuomba utaratibu wa Spika, Lissu naye alisimama akipinga kitengo cha kukatizwa na waziri huyo kuchangia, tukio ambalo liliingiliwa na Spika na kuzua majibizano.
“Huyu ananizuia kwa misingi gani, kafuata utaratibu upi,” alisema Lissu huku Mgahama naye akiendelea kuzungumza huu akiwa amesimama kabla ya wote wawili kukatishwa na Spika Makinda aliyewataka wakae chini na kufafanua kuwa yeye ndiye anayejua utaratibu.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Makinda alimpa nafasi Mhagama kuendelea kuzungumza na alipomaliza alimpa nafasi Lissu ili amalizie kuchangia hotuba hiyo.
MWANANCHI
Jumla ya Sh600 bilioni zitatumika katika Mradi wa Kuendeleza Jiji la Dar es Salaam (DMDP), katika mwaka wa fedha 2015/2016, ikiwamo kuboresha miundombinu ili kudhibiti mafuriko.
Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia alisema hayo bungeni jana aliposoma maelezo kuhusu mapitio ya kazi ya wizara yake kwa mwaka huo wa fedha.
“Mradi wa DMDP, utatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB),” Ghasia.
Alisema kazi zilizopangwa kwenye mradi huo ni kuimarisha miundombinu ya barabara za mabasi yaendayo haraka.
Waziri Ghasia alisema fedha hizo zitatumika kujenga mifereji mikubwa na midogo ya maji ya mvua katika maeneo yanayoathiriwa na mafuriko mara kwa mara hasa mabondeni.
Alisema mradi huo umegawanyika katika sehemu tatu, ya kwanza ni kuboresha miundombinu ya barabara na mifumo ya maji ya mvua katika mabonde matano yaliyopo katika halmashauri za Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam.
Alisema sehemu ya pili ya mradi huo itaboresha njia za waenda kwa miguu, taa za barabarani, madaraja pamoja na miradi ya ujenzi inayohusiana na usafi wa mazingira.
Waziri Ghasia alisema sehemu ya tatu ya mradi huo, itazijengea uwezo taasisi zinazotoa huduma kwa jamii.
Hata hivyo, alisema ili mradi huo utekelezwe, Serikali inapaswa kulipa fidia kwa wananchi wote watakaoathirika kutokana na utekelezaji wake.
“Dola 23.4 milioni za Marekani, zitatumika kwa ajili ya kulipa fidia. Manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam zimeshatenga fedha katika bajeti zao,” alisema Waziri Ghasia.
Alisema katika kuanza utekelezaji wa mradi huo kwa mwaka wa fedha wa 2015/16, Sh11.7 bilioni zitatumika katika shughuli za ujenzi wa barabara.
“Sh5.6 bilioni zitatumika kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za miradi,” alisema Waziri Ghasia.
MWANANCHI
Wakati CCM ikifanya jitihada za kudhibiti makada wake wanaotajwa kuwania urais, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal amemtuma waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuendesha moja ya shughuli ambazo chama hicho kinaamini kuwa ni moja ya majukwaa ya kampeni kwa wagombea.
Dk Bilal amemtuma Lowassa, mmoja wa makada wanaotajwa kutaka urais, kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti wa Patandi mkoani Arusha Alhamisi wiki hii, ambako habari zinasema siku mbili baadaye huenda mbunge huyo wa Monduli akatangaza rasmi nia yake ya kuanza safari ya kuelekea Ikulu kwa tiketi ya CCM.
Taarifa iliyotolewa jana na mwandishi wa habari wa Makamu wa Rais, Boniface Makene inaeleza kuwa Dk Bilal anakabiliwa na majukumu mengine ya kitaifa na hivyo ametoa ombi maalumu la kuwakilishwa kwenye harambee ya kukamilisha ujenzi wa msikiti huo ulioanza mwishoni mwa miaka 90.
“Makamu wa Rais ameona kuwa shughuli hii ya uchangiaji wa ujenzi wa msikiti isisogezwe mbele kumsubiri, bali iendelee kwa kuwa anaamini Lowasa ana uzoefu katika kufaninikisha shughuli za aina hii. Pia mchango wake katika shughuli za harambee katika shughuli ni wa mfano,” inasema taarifa hiyo.
Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa mchango wa wanajamii wanaoswali katika msikiti wa Patandi ni mkubwa kwani wamekuwa wakijitoa kwa namna nyingi kujenga mshikamano baina ya jamii zinazowazunguka bila kuwa na vikwazo na wameshiriki kuwasaidia watoto yatima.
Uamuzi huo wa Dk Bilal, ambaye kwa nafasi yake anaingia kwenye vikao vyote vya juu vya chama tawala, vikiwamo vya Zanzibar, utakuwa umetikisa harakati za kudhibiti baadhi ya makada wanaotajwa kuwania urais, hasa kambi ya Lowassa ambayo inasemekana inalalamikia kuchezewa rafu na uongozi wa CCM, ingawa haijabainisha rafu hizo.
Lowassa ni mmoja wa makada sita waliopewa onyo kali na CCM Februari mwaka jana, likiwazuia kujihusisha na uchaguzi kwa zaidi ya miezi 12 baada ya kubainika kuwa walianza kampeni mapema kwa kushiriki vitendo vinavyokiuka maadili, zikiwamo za harambee na hivyo kutakiwa kuomba kibali kabla ya kushiriki.
Hata hivyo, wiki mbili zilizopita Lowassa na makada wengine wanaotajwa kuwania urais walialikwa Zanzibar kwenye harambee ya kuchangia mfuko wa maendeleo wa mkoa mpya wa Magharibi, ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki tangu walipofungiwa na chama hicho mwaka jana.
Wasomi waliotafutwa na Mwananchi kuzungumzia uteuzi huo walikuwa na maoni tofauti.
NIPASHE
Mkuu wa zamani wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Tabora, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Bhoke Bruno na polisi wawili, wamefikishwa mahakamani kujibu shitaka la upotevu wa bunduki nane aina ya Sub Machine Gun (SMG) mali ya Jeshi la Polisi.
Walifikishwa jana katika Mahakama ya Mkoa wa Tabora.
Washtakiwa wengine waliofikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Issa Magoli, ni Koplo Iddi Abdallah na Mwinyi Gonga, wa Kikosi cha FFU Tabora.
Akiwasomea mashitaka, Wakili wa Serikali, Juma Masanja, alidai kuwa washtakiwa wote watatu wanakabiliwa na shitaka moja la kutochukua tahadhari stahiki katika utunzaji wa silaha.
Alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Aprili, mwaka jana na Aprili, mwaka huu wakiwa waajiriwa wa Jeshi la Polisi Kikosi cha FFU Tabora.
Wakili Masanja alidai kuwa washtakiwa kwa pamoja walishindwa kutumia njia za kiusalama katika utunzaji wa silaha na matokeo yake bunduki nane aina ya SMG ziliangukia katika mikono ya watu ambao si wamiliki halali wa silaha hizo.
Watuhumiwa wote walikana shitaka na kurejeshwa mahabusu baada ya kunyimwa dhamana kutokana na Wakili wa Serikali kupinga dhamana kwa hofu ya kuingilia upelelezi pale watakapokuwapo nje.
Hakimu Magoli aliamuru washtakiwa hao warejeshwe tena mahakamani hapo Mei 21, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.
NIPASHE
Mji wa Kibaha mkoani Pwani, umegawa vitambulisho maalum vya matibabu kwa wazee wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea vitakavyowawezesha kupatiwa matibabu bure.
Ugawaji wa vitambulisho hivyo ulizinduliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Jeniffer Omolo, mjini hapa jana.
Hatua hiyo inafuatia siku chache baada ya serikali kutoa agizo kwa halmashauri zote nchini kuwatambua wazee wastaafu hususan wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea na kuwapa vitambulisho vitakavyowafanya watibiwe bure ikiwa ni njia sahihi ya kutambua juhudi zao za kulitumikia taifa wakiwa na nguvu.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Dk. Issessanda Kaniki, alisema uorodheshaji wa wazee wote kwa kupita nyumba kwa nyumba ulifanyika kwa kusaidiana na Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Good Samaritan ‘Help Age’ International ambapo jumla ya wazee 4,672 waliandikishwa.
Aidha, Dk. Kaniki aliongeza kuwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonyesha kuwa Halmashauri ya Mji Kibaha ina wazee 5,111.
“Hivyo baada uzinduzi huu wa leo (jana), ofisi yangu itapita tena kwenye mitaa yote 73 kuwahamisisha wazee ambao hawakupiga picha za vitambulisho wapige ili wapate vitambulisho vya matibabu bure,” alisema.
Aidha, Omolo aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, aliwataka watumishi wa Idara ya Afya kuzingatia maadili ya kazi yao na kuwahudumia wazee hao kikamilifu.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, jana Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alizuiwa kumaliza kusoma hotuba yake ambayo ndani yake ilikuwa ikiwalipua vigogo waliohusika na uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow huku akieleza kilichojificha ndani ya kashfa ya mtambo wa kufua umeme wa Dowans na Richmond.
Amesema suala hilo la Dowans na Richmond, lilichochewa na makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) , na sasa linaliligharimu taifa kwa kudaiwa Sh bilioni 120.
Wakati Mbowe akitakiwa kuketi kwa madai kuwa muda wake ulikuwa dakika 30 na zilikuwa zimeisha, mwanzo wa hotuba yake alikuwa amezungumzia masuala ya kura ya maoni, uandikishaji wapiga kura na Uchaguzi Mkuu.
Pamoja na juhudi za baadhi ya wabunge wa upinzani akiwamo Mbowe, kumweleza Spika wa Bunge, Anne Makinda kwamba kambi hiyo walikuwa wamekubaliana kiongozi wao atumie dakika 50 na wengine watumie 20 kila mmoja, kiongozi huyo wa Bunge aligomea hatua hiyo na kusema kanuni hairuhusu.
Mwiba wa Mbowe
Katika sehemu ya hotuba ya Mbowe, ilisema: ‘Mlolongo huu wa kushindwa kusimamia nchi, kuendekeza makundi na vita vya siasa ndani ya CCM na Serikali yake kwa gharama ya taifa.
“Taifa hili sasa linadaiwa Sh bilioni 120 baada ya kushindwa kwenye kesi ya Dowans/Richmond katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) huko Paris,”
Serikali haijataka kuliweka jambo hilo wazi na ni dhahiri kuna siri kubwa inayosababisha jambo hilo kuwa la usiri mkubwa.
“Huko mbele ya safari jambo hili litaligharimu taifa mabilioni haya ya fedha ambayo yangeweza kuepukika kama ukweli, uwazi na haki vingetawala mchakato mzima wa kashfa ya Richmond.
“Serikali isimame sasa na ilieleze taifa ni nani anasema kweli, ni nani alilidanganya Bunge na ni nani analindwa na serikali katika kashfa hii?” ilihoji.
Iliendelea kusema: “Mapambano ya mitandao ndani ya serikali ya CCM na minyukano ya kupigania maslahi na ulaji ndani ya mikataba mbalimbali ya miradi ya umma ikiongozwa na walio karibu na watawala na familia zao imeota mizizi katika serikali hii.
“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ingependa kujua kwamba serikali hii ya CCM ambayo imefikia mwisho wake ni kwa nini inawaachia Watanzania madeni makubwa hivi?
“Je, kashfa hizo zote za serikali kushindwa kuwajibika, kutafuta visingizio vya kufunika madhambi yake, ndiyo maisha bora kwa kila Mtanzania ambayo wananchi waliahidiwa miaka 10 iliyopita?” alisema na kuhoji.
Alihoji na kutaka kujua kauli ya serikali juu ya tabia ya kuwabebesha wananchi mizigo ya madeni huku Serikali ikijitahidi kwa nguvu zake zote kuwasafisha viongozi walioitumbukiza nchi kwenye madhila hayo.
Kuhusu kashfa ya Escrow, hotuba ya Mbowe ilieleza tangu kampuni hiyo ilivyoingia nchini mwaka 1994 na mawaziri waliokuwa kwenye wizara mbalimbali zinazodaiwa kuisaidia kuwekeza nchini mpaka kuchotwa kwa zaidi ya Sh bilioni 300 Benki Kuu (BoT).
MTANZANIA
RAIS Jakaya Kikwete jana alitembelea maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ambayo yameathirika na mafuriko kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.
Ziara hiyo ilianzia katika daraja linalotenganisha Mbagala Kuu na Mtoni Kijichi katika Wilaya ya Temeke na kumalizia katika Daraja la Jangwani katika Wilaya ya Ilala.
Rais Kikwete baada ya kuona daraja linalotenganisha Mbagala Kuu na Mtoni Kijichi, alitoa agizo kwa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) kuweka daraja la muda katika eneo hilo huku ujenzi ukiendelea.
Hata hivyo Rais Kikwete alipotembelea katika Daraja la Jangwani aliwataka wahandisi kutumia maarifa kuondoa taka zinazosababisha madaraja hayo kuziba ili maji yaweze kupita kwa urahisi.
“Katika eneo hili tuliwaambia watu wahame lakini walikataa sasa tutafanyaje. Inabidi wahandisi mtumie maarifa ya kutoa taka zilizoziba katika madaraja haya ili maji yasipite juu ya daraja bali yaweze kupita chini kwa urahisi.
“Nimeanza ziara yangu ya kuangalia madhara yaliyotokana na mafuriko na nimeanzia katika eneo la Mbagala na Jangwani.
“Kesho (leo) nitamalizia katika eneo la Mkwajuni na Tegeta na hapo ndipo nitakapotoa hitimisho la athari za mafuriko Dar es Salaam,” alisema Rais Kikwete.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, alisema imepokelewa msaada wa Sh bilioni 250 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kutengenenezea daraja la Mbagala Kuu na barabara kwa kiwango cha lami.
Alisema daraja hilo pamoja na barabara vitatengenezwa kwa miezi mitatu hadi minne.
Naye Mhandisi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Eliseus Mtenga, alisema itatafutwa mashine itakayotoa taka zote zilizoziba katika daraja la Jangwani maji yaweze kupita kwa urahisi.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyezahapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahaukusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTVikufikie.