Magazeti

Mgombea Urais ACT leo, Mabomu msafara wa LOWASSA na Mrithi wa Askofu MALASUSA..#StoriKubwa

on

swaa

MWANANCHI

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward Lowassa jana kwa mara ya kwanza alikumbana na joto la upinzani baada ya msafara wake kushambuliwa na mabomu ya polisi.

Tukio hilo, ambalo lilifanyika mbele ya msafara wa Lowassa, lilitokea jana eneo la Daraja la Nduruma katika Jiji la Arusha na kusababisha umati wa watu kutawanyika na wengine kutelekeza magari yao.

Wakati Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akimkaribisha kwenye chama hicho wakati wa mkutano mkuu alimwambia; “Mzee huku inabidi uwe unafanya mazoezi kidogo, kuna mabomu huku.”

Lowassa alikumbwa na kadhia hiyo, akiwa njiani na mgombea mwenza, Juma Duni Haji na viongozi wengine wa Ukawa, wakitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), huku wakiwa wamesindikizwa na umati wa watu na magari.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema kuwa polisi walilazimika kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya watu waliokuwa wakiwarushia mawe polisi na wengine kufunga barabara.

“Kwa hali ile, tungefanya nini? Wanatupa mawe kwa polisi na wamefunga barabara na kuzuia magari mengine yasipite…ikumbukwe kulikuwa hakuna kibali cha maandamano na hata kingekuja, matamko ya kuzuia maandamano yameshatolewa,”  Sabas.

Katika tukio hilo, idadi kubwa ya polisi walikuwa kwenye magari na silaha mbalimbali ambao baadaye walianza kurusha mabomu kutawanya watu na magari kwa eneo la daraja hilo.

Hata hivyo, katika tukio hilo, lililotokea saa nane mchana hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa na kutokana na nguvu hiyo ya polisi watu walitawanyika, na barabara hiyo ya Arusha- Moshi ilifunguka baada ya kutopitika kwa saa tano kuanzia saa nne asubuhi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Tindigani, Mbunge wa jimbo la Arusha, Godbless Lema alisema wamesikitishwa na kitendo cha polisi kumpiga mabomu Lowassa na msafara wake.

Tunajua polisi wamepata maelekezo na sasa wanataka kuwatisha wananchi, lakini tunasema leo ndiyo mwisho hatutakubali tena kunyanyaswa,” alisema Lema.

Lowassa aliwasili KIA saa 3:20 asubuhi akiwa ameongozana na viongozi wa Ukawa, Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia na Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi, Kaimu Mwenyekiti wa CUF taifa, Twaha Taslima na viongozi wengine.

Kwenye Uwanja wa KIA, shughuli mbali mbali zilisimama katika eneo la kushuka viongozi mashuhuri (VIP), ambapo mawaziri kadhaa walikuwa katika eneo hilo.

Baadhi ya viongozi hao ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Hassadi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Dk Mary Nagu, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tzeba.

Baada ya Lowassa kutua KIA, alikwenda moja kwa moja kwenye Hoteli ya KIA Lodge na mgombea mwenza wake, Juma Duni Haji kwa mapumziko mafupi.

Baada ya kupumzika saa 5:30 msafara ulianza kuelekea uwanja wa Tindigani Kimandolu na ulifika saa tisa na kukutana uwanja ukiwa tayari umefurika maelfu ya watu.

Akihutubia mkutano huo Lowassa alitahadharisha viongozi wa polisi, kuacha kutumia nguvu kupita kiasi, kwani anaweza kuwafikisha Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague nchini Uholanzi.

Lowassa alisema alikuwa akiiamini polisi, lakini alichokiona jana cha kupigwa mabomu ni jambo baya.

Kuhusu suala la Babu Seya aliyefungwa kifungo cha maisha gerezani alisema atafuatiliwa kwa kutumia suala la utawala bora kwa kuangalia vyombo vya sheria na hatua zingine zitafuatwa.

MWANANCHI

Askofu Dk Fredrick Shoo amechaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), akichukua nafasi ya Dk Alex Malasusa aliyemaliza kipindi chake cha miaka minane.

Dk Shoo, ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, alichaguliwa juzi usiku katika siku ya tatu na ya mwisho ya mkutano mkuu wa 19 wa kanisa hilo uliofanyika Chuo Kikuu cha Tumaini (Tuma) jijini Arusha baada ya kuwashinda maaskofu wenzake wawili, katika uchaguzi uliokuwa na kila aina ya ushindani.

Waliokuwa wakichuana kuwania nafasi hiyo baada ya kupendekezwa na Halmashauri Kuu ya KKKT ni Askofu Dk Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Askofu Charles Mjema wa Dayosisi ya Pare na Dk Shoo.

Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Dk Malasusa, ambaye pia ni askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, alimtangaza Dk Shoo kuwa mkuu wa kanisa hilo kwa kipindi cha miaka minne baada ya kupata kura 153, huku Dk Munga akipata kura 67, ikiwa ni baada ya uchaguzi huo kurudiwa mara tatu kutokana na mshindi kutopata zaidi ya theluthi mbili ya kura zote.

Kanuni za uchaguzi za KKKT zinaeleza kuwa mshindi atapatikana kwa kupata kura zisizopungua theluthi mbili ya kura zote zilizopigwa, iwapo mshindi hatapatikana katika duru la kwanza, majina mawili yaliyopata kura nyingi ndiyo yatakayopigiwa tena kura.

Iwapo theluthi mbili haitapatikana katika duru la pili, kura ya wingi au uchache itatumika kwa duru la tatu ili kumpata mshindi.

Katika kuhakikisha mshindi anapatikana, mkutano huo ulilazimika kutumia hatua ya wingi wa kura na Dk Shoo kuibuka mshindi.

Katika awamu ya kwanza, Askofu Mjema alipata kura 53, Dk Munga kura 81 na Dk Shoo kura 86, idadi ambayo haikufika theluthi mbili ya kura zote kulingana na kanuni za kanisa hilo jambo lililosababisha uchaguzi kurudiwa mara ya pili.

Dk Malasusa alitangaza matokeo ya awamu ya pili ya kura zilizopigwa ambapo Askofu Munga alipata kura 94 na Dk Shoo kura 124. Kura moja ikiharibika.

Kabla ya kuanza kwa mkutano huo wajumbe wa Halmashauri Kuu walipitisha majina matatu ya maaskofu waliowania nafasi hiyo na kuyapeleka kwenye mkutano huo ili yapigiwe kura.

Wajumbe wa mkutano huo mara baada ya kupewa karatasi za kupigia kura walikwenda katika vyumba maalum kwa ajili ya kumchagua askofu wanayemtaka, mara baada ya kuchagua walitakiwa kurejea ukumbini na kutumbukiza karatasi hizo katika vifaa vilivyoandaliwa kuhifadhia kura hizo.

Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Dk Shoo alimshukuru Mungu huku akionyesha mshangao wa kuchaguliwa kwake.

“Sijui nimepataje nafasi hii, ni nguvu ya Mungu tu kwa kweli. Kwa ushirikiano wa waumumini wote nitaweza kufanya kazi hii, naomba mniombee,” alisema.

Akizungumza katika ibada ya kufunga mkutano huo uliomalizika saa 6:00 usiku, Dk Malasusa alisema anamuachia madaraka Dk Shoo katika hali ya amani na utulivu, huku akiwapongeza viongozi na maaskofu wote wa kanisa hilo.

Awali kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, mkutano huo ulimchagua Alice Mtui wa Dayosisi ya Konde kuwa mwandishi wa kanisa hilo kwa kipindi cha miaka minne.

Alice alipigiwa kura 201 na wajumbe wa mkutano huo, huku kura za hapana zikiwa 17 na kura moja ikiharibika.

MWANANCHI

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema uamuzi wa Jeshi la Polisi kuzuia misafara ya wagombea urais wakati wa kuchukua na kurejesha fomu batili, kinyume na Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa, na unalenga “kuionea huruma CCM” baada ya kufunikwa na vyama vinavyounda Ukawa.

Polisi imepiga marufuku misafara hiyo kwa maelezo kuwa imesababisha usumbufu kwa wakazi na kusimamisha shughuli nyingine za kila siku.

Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Abdulrahman Kaniki alitangaza uamuzi huo juzi baada ya watu wengi kujitokeza kumsindikiza mgombea urais wa CCM, Dk John Pombe Magufuli na baadaye wengi zaidi kujitokeza wakati mgombea wa Chadema, Edward Lowassa alipokuwa akienda kuchukua fomu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Jana naibu katibu mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya alisema chama hicho kitaendelea kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kama kawaida.

Alidai kauli ya polisi ni agizo la CCM baada ya kuona Watanzania wanajitokeza kwa wingi kwenye shughuli za kisiasa zinazofanywa na kwa pamoja na vyama vinavyounda UKAWA ambavyo ni CHADEMA, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF.

“Tumesikitishwa na kauli ya polisi. Nadhani wanacheza na amani na utulivu wa nchi yetu. Maandamano ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania na imeelezwa katika ibara ya 18(a) na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya muungano,” alisema Sakaya.

Alisema hata sheria ya vyama vya siasa, ibara ya 11 imefafanua kuhusu maandamano na kusisitiza kuwa kampeni haziwezi kufanywa kimyakimya.

Huwezi kuzuia maandamano na mikusanyiko katika shughuli za kisiasa,” alisema.

“Kwa sasa vyama vya upinzani vina wapenzi, mashabiki na wanachama wengi. Hizi ni njama za CCM kuzuia maandamano maana… katika mikutano yao watu ni wachache mno. Sisi (Ukawa) mikutano na maandamano yetu ina utulivu mkubwa. Polisi wasiwe na wasiwasi,” alisema. Alisema Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 watu walipoteza maisha kutokana na kauli kama hizo za kuzuia maandamano na mikusanyiko.

“Hii ni ishara kuwa polisi watatumia nguvu nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Wanataka kulazimisha bao la mkono. Wanatakiwa kulinda usalama wa wananchi katika mikutano na si kuizuia. Wasome katiba na sheria kwanza, si kuzuia tu kila jambo,” alisema.

Alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu msimamo wa CUF, kaimu mkuu huyo wa polisi alitaka atafutwe msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba ambaye alisisitiza kuwa amri hiyo inalenga kuimarisha usalama wa nchi na wananchi.

“Mambo yaliyojitokeza katika maandamano si sawa maana mwananchi walishindwa kufika katika shughuli zao. Tunaangalia usalama wa nchi kwanza. Tutafanya mkutano na kuwashirikisha wanasiasa ili kutafuta namna bora ya kufanya mambo yao bila kuathiri shughuli nyingine,” alisema.

“Hatutangazi ugomvi wala malumbano na vyama, tunataka siasa kufanyika wakati huohuo watu wengine wasiathirike. Amani ya nchi haitaki ushabiki na inamhusu kila mmoja wetu.”

Wakati polisi inazungumzia maandamano kuwa yalisumbua wananchi wengine, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, walipongeza msafara wa Lowassa kwenda kuchukua fomu NEC, wakisema kama wataendelea hivyo, Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani.

MWANANCHI

Hatimaye kitendawili kilichokuwa kikisubuliwa kwa hamu na wananchi wa jimbo la Busega mkoani Simiyu, kimeteguliwa baada ya kamati ya siasa ya wilaya hiyo kumtangaza Dk Raphael Chegeni kuwa mshindi katika kura za maoni ndani ya chama.

Matokeo hayo yamekuja baada ya Kamati Kuu ya CCM kuagiza uchaguzi huo kurudiwa kwa kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu, huku wagombea wote wakilalamikia vitendo vya rushwa katika matawi na vituo vya kupigia kura.

Akitangaza matokeo hayo kaimu katibu wa CCM wa Busega, ambaye pia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Meatu, Jonathan Mabia alimtangaza Dk Chegeni kuwa mshidi baada ya kupata kura 13,838 akifuatiwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani aliyepata kura 11558.

Mabia alisema jumla ya wapiga kura 28,127 walijitokeza kupiga kura, lakini kura 457 ziliharibika na kubaki kura halali 27,700.

Dk Chegeni ambaye ndiye mshindi wa kura za maoni ya ubunge wa jimbo la Busega, akizungumzia matokeo hayo alisema hiyo imetokana na ufuatiliaji wake wa kuhoji viashiria vya udanganyifu wa matokeo alivyoviona.

Alisema makundi ndani ya CCM katika wilaya hiyo yaweza kukifikisha pabaya chama kutokana na baadhi ya viongozi kuwabeba wagombea, na kwamba kwa ushindi huo ni bora wakaunga kuhakikisha wanapata ishindi kwenye uchaguzi mkuu.

Kwa upande wake Dk Titus Kmani alionyeshwa kutokulidhishwa na matokeo hayo, na kudai kuwa matokeo aliyopata Dk Chegeni ni uhuni uliofanywa na baadhi ya wapambe wake wa kubadilisha matokeo katika vituo.

“Nimefika kwenye ofisi ya chama asubuhi ili kuweza kuingia katika chumba cha kuhesabia matokeo, cha kushangaza kamati ya siasa ilijifungia na mmoja wa wagombea hao ambaye hapa sasa wamemtanga mshindi, inaonyehsa ni dhahili kweli matokeo hayo wametengeneza,” alisema Dk Kamani.

HABARILEO

Rais Jakaya Kikwete amesema ukiona Waziri anajisifia kafanya mambo kadhaa kwa uwezo wake, huyo ana matatizo ya ufahamu na ni mpenda sifa, kwa sababu mambo anayoyafanya anatekeleza majukumu aliyopewa na Rais na kwa mujibu wa muongozo aliopewa.

Alisema hayo jana wakati akiagwa jijini Dar es Salaam na taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Ujenzi, huku akiongeza kuwa vuguvugu za kisiasa zinazoendelea, ni moto wa mabua ambao hauwaki ukadumu.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli ambaye pia ndiye mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), angekuwa kama mawaziri hao, angejisifia kwa mafanikio yote yaliyopatikana katika Wizara alizoziongoza, ikiwemo Wizara hiyo ya Ujenzi.

Katika hotuba hiyo amesema sifa moja ya Dk Magufuli ni kutambua kuwa akiwa Waziri, anafanya kazi kwa niaba ya Rais kwa mujibu wa muongozo na rasilimali alizopewa, ambavyo vimeeleza nini anatakiwa kufanya kama waziri.

“Sijawahi kukusikia ukijisifia binafsi maana na wewe ungeweza kabisa kufanya hivyo kwa sababu barabara zote hizi ungeweza kusema ni mimi nimejenga na sio Rais… Sasa bila Rais kukuteua na kukupa muongozo na rasilimali ungepata nafasi ya kujenga hizo barabara?”

Alihoji Rais Kikwete. Alisema baadhi ya watu wamediriki kusema waliyoyafanya ni wao na sio Rais aliyewapa muongozo huo kufanya yoliyofanyika na kuongeza: “Unadhani Rais atakuja kujenga nyumba? Amekwambia nimekupa hivi hapa na kila mtu niliyemteua nafanya hivyo na inatangazwa kwenye gazeti la Serikali.”

Rais Kikwete alisema Rais hana ushindani na Waziri wake na pia Waziri hana mashindano na Rais kwa sababu Waziri anafanya kazi kwa niaba yake maana ndiye aliyemteua.

Moto wa mabua Alisema CCM imemteua Dk Magufuli kugombea nafasi ya Urais kupitia chama hicho na ana imani atapita salama kwa sababu ni mtendaji kazi mzuri na kwamba vurugu zinazoendelea za kisiasa ni moto wa mabua tu. “Nina imani chama chetu kimekuteua kuwa mgombea wa urais kwa sababu ni mtendaji… Taifa litanufaika likipata kiongozi kama wewe, hao wengine ni moto wa mabua tu hauwaki ukadumu,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema ana imani Mungu akijalia Magufuli kuwa Rais basi yale mambo mazuri aliyoyafanya katika Wizara ya Ujenzi na sekta ulizopata kuongoza, atatumia maarifa na uzoefu huo kusukuma mbele gurudumu la taifa mbele. Alisema Dk Magufuli kila wizara aliyopelekwa alifanya vizuri, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Miundombinu na Ardhi ambapo alisaidia kuondoa ujanja ujanja na kuimarisha nidhamu lakini hakuwahi kusema ni yeye binafsi ameleta manufaa hayo.

“Kuna wakati sehemu fulani ina matatizo watu wanasema jamani kwa nini msimlete Magufuli, tunasema hawezi kuwa kila mahali… Na sekta hii ya ujenzi ni sekta muhimu na kubwa, nashukuru chini ya uongozi wako tumeifikisha mahali pazuri,” alisema Rais Kikwete.

Aidha Rais Kikwete alisema anajivunia kuunganishwa kwa barabara zote za mikoa na Wilaya nchini katika kipindi cha uongozi wake na hiyo ni kwa jitihada na usimamizi uliofanywa na Waziri Dk Magufuli.

“Katika uongozi wangu tumefanikiwa kuunganisha karibu mikoa yote nchini kwa kiwango cha lami. Jambo hili limewezekana kwa ushirikiano na wafanyakazi wote pamoja na wataalam wa wizara hii ya ujenzi.”

Kikwete alisema alipoingia madarakani, bandari ya Dar es Salaam ilikuwa inasafirisha jumla ya tani milioni 6.7 za mizigo kwa mwaka, lakini hivi sasa bandari hiyo inasafirisha mizigo zaidi ya tani milioni 15 hadi mwishoni mwa mwaka huu, bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kusafirisha zaidi ya tani milioni 18, kitu ambacho kitaongeza ukuaji wa uchumi na kuongezeka kwa pato la taifa.

Aidha alisema kukamilika kwa barabara zote nchini kwa kiwango cha lami kutawezesha uchumi kukua kwa haraka zaidi na kuifanya nchi kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwa siku za usoni. Rais Kikwete pia alisema katika kipindi chote cha uongozi wake ameweza kupambana na changamoto zilizokuwa zikiikabili wizara ya ujenzi na ndio maana mafanikio haya yamepatikana.

 

HABARI LEO

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imevitaka vyama vya siasa kuwasilisha majina ya watu saba watakaoambatana na wagombea wa urais na wagombea wenza wakati wa kurudisha fomu siku ya Ijumaa Agosti 21 mwaka huu.

Imetaka majina hayo yawasilishwe NEC kabla ya Agosti 20 mwaka huu ili kuratibu urudishaji fomu huo utakaoanza saa 1:30 hadi saa 10:00 jioni, ili wagombea wateuliwe rasmi na tume.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima, siku hiyo wagombea nafasi ya urais na wagombea wenza watarejesha fomu za urais.

Alisema wagombea hawaruhusiwi kwenda tume kwa maandamano, shamrashamra, nderemo wala vifijo kwa sababu vyama vya siasa vitakavyowasilisha fomu za kuomba kuteuliwa nafasi ya urais na makamu wa rais vitakuwa vingi.

Alisema iwapo kila chama kikienda kwa maandamano inaweza kutokea uvunjifu wa amani pia kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao pamoja na kuimarisha amani na utulivu katika jiji hili. Kailima alisema anawasihi wahusika wote kuzingatia maelekezo hayo.

Wiki hii, jeshi la polisi nchini limesitisha maandamano ya aina yeyote wakati wa uchukuaji au urudishaji fomu pamoja na harakati za kutafuta wadhamini mikoani kwa wagombea wa nafasi ya urais na ubunge. Hatua hiyo imechukuliwa ili kuweka hali ambayo haitaleta usumbufu au kuhatarisha usalama wa raia na mali zao.

HABARILEO

Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limefungia na kukitoza faini ya Sh milioni 200 kiwanda cha kusindika nyama ya punda cha Huwacheng kilichopo katika Kata ya Kizota, mjini hapa.

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na raia wa China, kimefungiwa kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni ufanyaji wa biashara kinyume na utamaduni wa Watanzania pamoja na mazingira yasiyoridhisha kiwandani hapo.

Ofisa Mwandamizi wa NEMC, Madoshi Makene, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa watatoa barua itakayokuwa na faini ya kiasi kisichopungua Sh milioni 200 kwa kuwa wamekiuka sheria nyingi ambapo aliwataka kuacha shughuli zote za uchinjaji wa punda.

“Wamiliki wa kiwanda hiki wamekiuka sheria nyingi za nchi. Wanatakiwa wafuate sheria za nchi. Ilikuwa wajue, je inaruhusu kuchinja punda? Wanatakiwa watafute mtaalamu ambaye atasema kama kuchinja punda kisheria inakubalika na jamii au la,” Dk Madoshi.

Naye mwanasheria kutoka Baraza hilo, Manchari Heche akizungumzia kufungwa kwa kiwanda hicho, alisema kuwa uwekezaji uliofanywa na raia hao kutoka nchini China umekiuka taratibu ambapo alidai kuwa nyaraka walizonazo haziruhusu kuchinja punda.

“Tumekifunga kiwanda hiki kutokana na kuwa na mazingira mabovu, kwanza hayaruhusu kuchinja punda, binadamu wanaishi humuhumu ndani ya kiwanda na eneo ni chafu, maji na damu zimezagaa. Hata nyaraka walizotuonesha hazieleweki na hazijaonesha kuwa kiwanda hiki ni kwa ajili ya matumizi gani lakini wenyewe wanachinja punda,” alisema mwanasheria huyo.

Aliongeza kuwa nchi ya Tanzania haina uwezo wa kuwalisha raia wa China zaidi ya bilioni 2 kwa kutegemea nyama ya punda kutoka mkoani Dodoma.

“Kwanza punda ni wanyama ambao hawapatikani kwa wingi hivyo tunaamuru kiwanda kufungwa na waliopo waachiwe huru na mitambo ya kiwanda hiki izimwe,” alisema Heche.

Maofisa hao wa NEMC walisema mbali na kufungia kiwanda hicho wataendelea kufanya ukaguzi endelevu utakaowezesha kufichua viwanda vingine vya aina hiyo.

 

HABARILEO

Mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, inatarajiwa kujulikana leo baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kupendekeza jina la mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho.

Jana Kamati Kuu ya chama hicho ilikutana jijini Dar es Salaam, kujadili majina ya wagombea wa nafasi ya urais na ubunge.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba alisema kamati hiyo imekutana kwa ajili ya kujadili ajenda tatu ikiwemo ya kujadili majina ya wagombea.

Alisema kujadiliwa kwa majina hayo ni baada ya kumalizika kwa kura za maoni zilizofanyika katika mikoa mbalimbali nchini.

NIPASHE

Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imetangaza kuboresha mitaala kuanzia darasa la tatu na la sita  na kupunguza idadi ya masomo kutoka 11 kufikia saba.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TET ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ubunifu na Ukuzaji wa Mitaala, Dk. Wilberforce Meena, aliwaambia waandishi wa habari wakati akizungumzia majukumu ya Taasisi hiyo na mafanikio katika kuandaa na kuboresha mitaala nchini.

Alisema kuwa mtaala huo utapunguza masomo na maudhuu yaliyopo kwenye masomo ili kumuwezesha mwanafunzi kufanya vizuri darasani.

Aliyataja masomo hayo saba kuwa ni Kiswahili, Kingereza, Hisabati, Sayansi na Teknolojia, maarifa na jamii, Uraia na maadili pamoja na dini. Alieleza kuwa kutakuwa na somo la michezo ambalo litatumika kama kuibua vipaji vya wanafunzi katika shule.

Alisema maboresho hayo ya mitaala wameyafanya kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa elimu   295 wakiwemo walimu, maafisa elimu, wanafunzi, watunga sera na bado wanaendelea kupokea maoni kuhakikisha mtaala unakidhi mahitaji.

Meena alisema yalitokea malalamiko ya wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza bila kujua kusoma ama kumaliza elimu ya msingi bila kujua kusoma wakafanya utafiti na hatimaye kubadili mitaala.

Meena alisema kwa shule ambazo zinafundisha kwa Kiingereza wanatakiwa kufuata mitaala  waliyowaandalia licha ya kudaiwa kufundisha mambo mengi.

Alisema tayari wametoa mafunzo kwa walimu 32,000 kuhusiana na mitaala hiyo kwani ya awali walishindwa kuitekeleza kwa kuwa hawakuwa na uelewa.

 

PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos

Tupia Comments