MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amesema idadi ya wanachama wa CCM waliojitokeza kuwania urais ni kubwa, hivyo ni lazima wawape viongozi muda wa kuwachuja lakini akawataka wasiwanunie baada ya kufanya uamuzi.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika hotuba yake ya kuvunja Bunge ambayo iliibua waziwazi ushabiki kwa wagombea, hasa baada ya kumtaja aliyekuwa waziri mkuu wake wa kwanza, Edward Lowassa kwa ajili ya kumshukuru.
Akitoa salamu zake kwa wagombea hao, Rais Kikwete aliwapongeza na kuwatakia mafanikio mema katika safari yao.
“Wale wanaogombea urais waliomo humu (bungeni) nawatakia kila la kheri na nawashukuru kwa kuonyesha nia ya kunipokea mzigo huu mzito. Nawatakiwa heri katika matamanio yenu,” alisema Rais Kikwete ambaye aliingia Ikulu mwaka 2005.
“Mko wengi, wote ni vigogo na mmetupa kazi kama kamati kuwachuja kwa hiyo msitununie tukifanya maamuzi.”
Wakati akihitimisha hotuba hiyo, Rais aliwashukuru watu mbalimbali waliofanya kazi kwenye Serikali yake, lakini hali ilikuwa tofauti alipomtaja Lowassa ambaye alifanya naye kazi kwa miaka miwili.
Alimshukuru pia, Makamu wake, Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na baadaye wabunge na viongozi wengine.
Alianza kwa kuwashukuru huku akiwataja majina. Kila alipotaja majina ya viongozi hao, wabunge walipiga makofi kwa kugonga meza zao. Hata alipomtaja Dk Bilal na Pinda, wabunge hao walishangilia kwa kawaida.
Hata hivyo, alipofikia kutaja jina la Lowassa, kelele za wabunge zilikuwa maradufu, wengi wao wakipiga meza kushangilia, hali iliyomfanya Rais Kikwete anyamaze kwa sekunde kama 50 na ndipo Lowassa aliposimama na kuinamisha kichwa kuonyesha kukubali shukrani hizo.
Wabunge waliendelea kumshangilia hadi alipoketi na ndipo Rais Kikwete akaendelea kutoa shukrani kabla ya kuhitimisha hotuba yake ya saa mbili na dakika 20.
MWANANCHI
Viongozi wa vyama vya siasa visiwani hapa wamekataa kusaini waraka wa maadili ya uchaguzi ya vyama vya siasa uliowasilishwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), vikitaka vyombo vya usalama vijumuishwe.
Makubaliano ya maadili hayo ya uchaguzi yalitakiwa yasainiwe kwenye kikao hicho baina ya ZEC, iliyoongozwa na mwenyekiti wake, Jecha Salum Jecha na viongozi wa vyama vya siasa kwenye Hoteli ya Grand Palace.
Maadili hayo yanatakiwa kuwa mwongozo kwa vyama vya siasa wakati wote wa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya uchaguzi kufanyika kwa uhuru na haki.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa alisema hawatasaini waraka wa maadili hayo hadi kitakapoingizwa kipengele kitakachoeleza wazi majukumu ya polisi na vikosi vya SMZ alivyodai vimeonyesha ishara mbaya katika siku za hivi karibuni.
Jussa alisema licha ya kuwa vikosi vya SMZ havitakiwi kisheria kusimamia uchaguzi, vimekuwa vikiingilia uandikishaji wa wapigakura na kukiuka haki za binadamu, sheria, kanuni na taratibu za uandikishaji, jambo ambalo limesababisha malalamiko makubwa kwa wananchi na wadau hao.
Alisema bila ya kuwekewa kipengele mahususi kwa polisi na vikosi vya SMZ, maadili hayo yatakuwa hayana maana yoyote kwa kuwa hivi karibuni Wazanzibari wameshuhudia baadhi ya askari wakiwa wamefunika nyuso zao.
Alidai kuwa askari hao wamekuwa wakibeba silaha za moto na za kienyeji kama mapanga, nondo na misumeno ya kukatia miti na kuwatisha wananchi na waandishi wa habari.
“Mwenyekiti mimi na chama changu hatukubali kusaini maadili haya na ninawashawishi wenzangu wakatae hadi hapo kitakapoingizwa kipengele ambacho kitaeleza bayana majukumu ya polisi, majukumu ya vikosi vya SMZ,” alisema.
“Hivi juzi tu vimeonyesha mfano mbaya kwa askari kuvaa masoksi usoni kuwavamia na kuwapiga watu, kuvamia vituo vya redio na kufanya uhuni mkubwa. Kwa hivyo kama hawajaingizwa hawa kwenye mwongozo huu wa maadili hatuwezi kutia saini. Kikao kivunjwe, mkaingize na kisha tuitane tena kuja kusaini,” alisema.
Wajumbe hao walisema ni kweli kuna kila sababu ya polisi na vikosi vya SMZ kuwekewa utaratibu wa maadili kwa kuwa wao ndio waharibifu wa uchaguzi hivyo si vyema maadili yakawaacha nyuma.
MWANANCHI
Siku nne baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwahukumu kifungo cha miaka mitatu jela mawaziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Daniel Yona na Basil Mramba, upande wa mashitaka umewasilisha kusudio la kukata rufaa.
Kusudio hilo lililowasilishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wanapinga adhabu na hukumu iliyotolewa na jopo la mahakimu watatu, John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela, pamoja na kuachiwa huru kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja.
Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha alisema kusudio hilo limeshawasilishwa na upande wa mashitaka mahakamani hapo.
Wakati upande wa mashitaka ukichukua hatua hiyo, mawakili wa kina Mramba na Yona nao wameanza mchakato wa kutaka ‘kuwachomoa’ gerezani na kuwarudisha uraiani kwa kuomba wapatiwe dhamana wakati watakapokuwa wakisubiri rufaa yao kusikilizwa.
Mramba na Yona walihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia hasara serikali ya Sh11.5 bilioni.
Hata hivyo, wakili wa Yona, Elisa Msuya, juzi alisema kwasasa wanaandaa maombi ya dhamana na wakati wowote watafungua maombi hayo Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, wakati wakisubiri kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa.
Wakili wa Serikali, Charles Anindo alisema kwa mujibu wa kifungu cha 368 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, kinaruhusu mfungwa kuombewa dhamana wakati rufaa yake inasubiri kusikilizwa.
Hata hivyo, Wakili Anindo alibainisha kuwa kifungu hicho kinahusika tu kama kuna uwezekano mkubwa wa rufaa hiyo kushinda.
Hata hivyo, wakati Yona na Mramba wakitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo hicho, Mgonja aliachiwa huru baada ya mahakama kuridhika kuwa hana hatia kwa mashitaka kumi na moja yaliyokuwa yakimkabili.
MWANANCHI
Rais Jakaya Kikwete amelihutubia Bunge la 10 kwa mara ya mwisho, akijikita katika takwimu zinazoonyesha mafanikio ambayo Serikali ya Awamu ya Nne imeyapata tangu alipoingia Ikulu mwaka 2005, lakini akakiri kutofanikiwa kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Hali iliyokuwa mwaka 2010 wakati alipohutubia Bunge hilo kwa mara ya kwanza, ndiyo iliyojirudia jana baada ya wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao na kuwaacha wapinzani wachache.
Rais Kikwete, ambaye alihutubia kwa saa 2.20 alitangaza kulivunja Bunge la 10 lakini akasema litavunjwa rasmi Agosti 20, akieleza kuwa shughuli ya jana ilikuwa kama “kitchen party au send off”.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete alimmwagia sifa Spika Anne Makinda, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi mbalimbali wa Serikali, wananchi na chama chake kwa kumuamini, huku akisisitiza kuwa anaondoka madarakani na kuiacha nchi ikiwa salama.
Huku akishangiliwa na wabunge, Rais Kikwete alieleza kuwa Serikali yake ilipata mafanikio katika utawala bora, uhuru wa habari, vita dhidi ya rushwa, kukua kwa mapato ya Serikali, maadili ya viongozi, mihimili ya Serikali, uanzishwaji wa wilaya mpya, nyongeza ya mishahara, mifugo na uvuvi.
Ushiriki wa wanawake katika uongozi, kukuza uchumi, utalii, viwanda, madini, umeme, uchukuzi, huduma za kibenki, michezo, masilahi ya wafanyakazi, burudani, ajira, utamaduni, Muungano, amani na umoja ni masuala mengine ambayo mkuu huyo wa nchi ameeleza yalikuwa na mafanikio.
“Desemba 30, 2005 nilipozindua Bunge la Tisa nilielezea mtazamo wangu kuhusu nchi yetu na kutaja majukumu ya msingi na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nne. Nilisema tutatekeleza wajibu wetu na vipaumbele hivyo kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya,” alisema.
Alifafanua kuwa Julai 16, 2010 wakati wa kuvunja Bunge la Tisa alieleza mafanikio yaliyopatikana na changamoto zake na Novemba mwaka huohuo wakati akilizindua Bunge la 10, aliahidi kutekeleza vipaumbele vya Serikali kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi, jambo ambalo alisema amelifanya kwa kiwango kikubwa.
Alisema marais waliopita, Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi walifanya mambo mengi mazuri lakini hawakumaliza yote na kusisitiza kuwa kila jambo lina changamoto zake.
“Hata Baba wa Taifa hakumaliza yote na mimi ninamuachia Rais ajaye ayamalize yale ambayo mimi sikuyamaliza,” Rais Kikwete.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Rais alisema licha ya juhudi kubwa iliyofanywa na Serikali, bado kuna changamoto katika upatikanaji wa masoko ya uhakika na bei nzuri kwa mazao ya wakulima.
MWANANCHI
Baada ya vikao mfululizo wiki hii, hatimaye Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) unatarajia kumtangaza mgombea urais wake kesho.
Taarifa zilizopatikana jana zimeeleza kuwa baada ya kikao cha viongozi wa ngazi za juu wa Ukawa, umoja unaoundwa na NLD, Chadema, CUF na NCCR – Mageuzi kilichofanyika juzi, mambo kadhaa yameafikiwa na kama hakutokuwa na mabadiliko yoyote, mteule wa urais kupitia umoja huo atabainishwa.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi alithibitisha kuwa tayari makubaliano ya kugawana kata na majimbo kwa nafasi za udiwani na ubunge yamekamilika na kilichobaki ni utekelezaji.
“Tumeshakubaliana namna ya kugawana kata na majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka wazi kwa wananchi. Pamoja na hilo pia tutamtangaza mgombea urais na chama anachotoka,” Dk Makaidi.
Siku chache baada ya baadhi ya wabunge kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge na Spika Anne Makinda, Jumanne ya wiki hii Chadema ilifanya mkutano wa dharura kujadili mambo kadhaa ya kitaifa.
Siku moja baada ya kikao hicho, viongozi wa waandamizi wa Ukawa walikutana na kujadili mambo yanayohusu umoja huo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata baada ya vikao hivyo, mpaka jana Chadema iliendelea na vikao vyake vya ndani kujadili mambo kadhaa kabla ya kikao cha Kamati Kuu ya Ukawa kinachotarajiwa kufanyika leo kupitisha jina la mgombea urais.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika alithibitisha kuendelea kwa vikao vya ndani vya chama hicho na kueleza kuwa hawezi kusema chochote kwa sababu ajenda bado zinajadiliwa na kwamba kesho taarifa za uhakika zitatolewa kwa vyombo vya habari.
MTANZANIA
Mbinu chafu zilizosukwa ndani ya CCM za kumuengua aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa zimevuja.
Chanzo cha kuaminika kilisema uongozi wa juu wa Chama hicho ulimwagiza jaji mmoja kuandika waraka mzito kumhusu Lowassa.
Jaji huyo alipewa maelekezo katika waraka huo kuhakikisha anaweka maelezo kuwa Lowassa amevunha sheria za uchaguzi.
“Huwezi kuamini kuna jaji mmoja amepewa kazi ya kuandika waraka mzito wa kuupeleka kwa kamati ya maadili na baadaye kamati kuu, eti Lowassa amekiuka sheria za Uchaguzi…tumeshangazwa mno na hatua hii, ndio maana kwa siku mbili mfululizo kamati ya amaadili zimeshindwa kukaa kwa sababu zinasubiri waraka huo”.
“Hatuelewi kinachoendelea baada ya Rais kulivunja Bunge, tuliambiwa kamati inakutana lakini mpaka sasa hakuna kinachoendelea,kuna siri gani ambayo imejificha kwenye kamati hizi?? walihoji.
Chanzo hicho kilisema huo ni mkakati mpya kw akina na watu kadhaa kumuengua Lowassa.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amesema baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho siyo waaminifu na wamejinufaisha na mali za chama hicho hali ambayo imekigeuza kuwa ombamba kwa wafanyabiashara.
Akifungua jengo jipya la mikutano la kimataifa la chama hicho, Dodoma Convention Centre, Rais Kikwete alieleza kusikitishwa kwake na ubadhirifu unaofanywa na viongozi hao, ambao wameanza kugawana viwanja, kujenga majumba, wengine kujimilikisha rasilimali za chama hicho na wengine kuweka mapato ya rasilimali zake mfukoni.
“Msitembee tu kwa matajiri kwenda kuombaomba, wanawadhalilisha bure. Inashangaza kuona chama hiki biashara yake kubwa ni kulaza magari ya watu na sijui mapato yake yanakwenda wapi…Tunazo rasilimali, tunayo mitaji, lakini hatuzitumii rasilimali hizo kupata mapato,”Rais Kikwete.
Kufuatia hali hiyo, Rais Kikwete amemwagiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdurahman Kinana, kuunda kitengo maalum cha ukaguzi wa mali za chama hicho, ikiwa ni pamoja na kumteua Mkaguzi Mkuu atakayezunguka nchi nzima kufanya uhakiki wa mali zake na kutoa taarifa kwa uongozi wa juu.
Alisema CCM imekuwa ikitumia sera ya ujamaa na kujitegemea, lakini hivi sasa wameipotezea kwa kutegemea wafadhili na wakati mwingine chama hicho kimejikuta kikienda kuchukua fedha za moto (rushwa), ambazo zinakilazimisha kutumia muda mwingi kujisafisha.
“Kama ni mtaji ni mtaji mfu, lazima tuitoe ile ‘dead capital’ iwe hai; sijui tumekutwa na nini au viongozi wetu wana maarifa mafupi. Kazi ya kujipanga foleni, kila siku ya kukimbilia kwa matajiri itaisha lini, wanawadhalilisha tu, mnapata aibu, sijui mtaondokana nao lini?” alihoji.
Alidai kwamba Jiji la Dar es Salaam peke yake, CCM ina viwanja zaidi ya 420, lakini haviendelezwi na matokeo yake vimegeuka karakana ya biashara ya kulaza magari.
“Watu wote pale wanaangusha magorofa na wanapata mapato. Viwanja vile biashara kubwa ni ya kulaza magari, mapato yenyewe ya kulaza magari sijui hata anachukua nani, lini tutazinduka kwenye usingizi huu…Tambueni kwamba ardhi ile ni mtaji,”alisisitiza Rais Kikwete.
NIPASHE
Tanzania ni kati ya nchi tatu barani Afrika zenye watoto wengi wenye utapiamlo.
Takwimu hizo zilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Rukia Kassim Ahmed.
Mbunge huyo, alitaka kujua serikali inachukua hatua gani mahususi za kuhakikisha inapambana na tatizo hilo la watoto kudumaa kiakili.
Akijibu swali hilo, Dk. Kebwe alisema tatizo la watoto kudumaa kiakili lipo katika nchi nyingi duniani na linatokana na ulaji duni wa vyakula vyenye virutubisho vya kutosha.
Alisema watoto milioni 199 sawa na asilimia 33 duniani wa chini ya miaka mitano walikuwa wamedumaa hadi kufikia mwaka 2000. Alisema juhudi zinafanyika kupunguza tatizo hilo hadi kufikia watoto milioni 161 sawa na asilimia 25 kwa mwaka 2013.
Dk. Kebwe alisema kutokana na utafiti wa Kidemografia wa Afya wa mwaka 2010, asilimia 42 ya watoto chini ya miaka mitano walionekana kuwa na udumavu kutokana naa urefu wa kimo kutolingana umri wao.
Mbali na Tanzania, alitaja nchi nyingine zenye tatizo hilo kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Ethiopia.
Dk. Kebwe alitaja njia pekee ya kuondokana na utapiamlo kuwa ni wazazi kupata elimu ya kuwapatia lishe watoto wao.
Alisema ni muhimu mama kumnyonyesha mtoto wake kwa muda wa miezi sita bila kumpatia chakula kingine.
Alisema kwa sasa serikali inaendelea na utoaji wa elimu kwa jamii ili kuhakikisha watoto wanapatiwa lishe bora katika makuzi yao yote.
“Iwapo jamii itapata elimu inayotolewa na serikali kwa ajili ya kuwapatia lishe bora watoto waliopo chini ya miaka mitano ni wazi tatizo hilo linaweza kupungua kwa kiasi kikubwa” alisema.
HABARILEO
Serikali imetangaza kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Songwe na wilaya mpya sita zikiwemo Ubungo, Kigamboni na Tanganyika. Mkoa wa Songwe ulikuwa sehemu ya Mkoa wa Mbeya.
Licha ya Ubungo na Kigamboni za Dar es Salaam, Tanganyika ya Kigoma, wilaya nyingine zilizoanzishwa ni Kibiti mkoani Pwani, Songwe mkoani Songwe na Malinyi mkoani Morogoro .
Akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 20 wa Bunge jana mjini hapa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema ugawaji wa maeneo hayo unafanyika kila baada ya muda kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo ongezeko la idadi ya watu na pia kuharahisisha utendaji wa serikali.
Kuongezwa kwa Mkoa wa Songwe kunafanya idadi ya mikoa ya Tanzania Bara kufikia 26.Mikoa mingine iliyoongezwa katika Serikali ya Awamu ya Nne ni Geita, Katavi, Njombe na Simiyu.
Awali, mikoa ya Tanzania Bara ilikuwa 21, ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.
Zanzibar ipo mikoa mitano, ambayo ni Kaskazini Pemba, Kusini Pemba, Mkoa wa Mjini, Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Waziri Mkuu alisema pia Serikali imepandisha hadhi Halmashauri za Wilaya Malinyi, Buchosa, Madaba, Manyoni, Mpimbwe, Nsimbo, Mlale, Itilima, Buhigwe, Kakonko, Uvinza, Kyerwa, Chemba, Mbogwe, Nyang’wale, Butiama, Mkarama, Kaliua, Bumbuli na Msalala.
Alizitaja halmashauri za miji na Manispaa zilizoanzishwa ni Chalinze, Ifakara, Newala, Kondoa Mafinga, Nanyumbu, Mbulu, Mbinga, Bunda, Tunduma, Nzega, Handeni, Kasulu, Geita, Masasi, Ilemela, Kahama na Nzega.
Pia alisema kuna tarafa mpya tano ambazo ni Mchemwa iliyopo Newala, Mchichila, Mangombwa, Mambamba na Mangombya, zote zipo Tandahimba. Pia kuna kata mpya 586 zimeanzishwa sehemu mbalimbali nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, yapo maeneo ambayo ni chini ya utawala wa Rais moja kwa moja na yapo ambayo yapo chini ya mamlaka ya Waziri mwenye dhamana ya serikali za mitaa.
Pia alizungumzia uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura na kusema kuwa unaendelea vizuri na uchaguzi utafanyika Oktoba 25 kama ilivyopangwa.
Alisema uandikishaji unaenda vizuri na kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeshaandikisha watu milioni 11.2, kati ya watu milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa. Mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar uandikishaji haujaanza.
Alisema uchaguzi utakuwa huru na wa haki, amani na utulivu, hivyo wananchi wajiandae kuchagua viongozi watakaoona wanafaa.
HABARILEO
Misemo na mifano aliyotoa Rais Jakaya Kikwete wakati anahutubia Bunge jana ilikuwa kivutio kikubwa kwa wabunge hao.
Katika kila mfano aliokuwa anatoa katika hotuba hiyo ulionekana kuwagusa wabunge na kupiga meza kwa nguvu kumshangilia na hivyo kusababisha mara kwa mara hotuba hiyo iliyochukua karibu saa mbili na nusu kusimama mara kwa mara.
“Wewe ndiwe mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu wa juu kabisa katika mhimili huu wa kutunga sheria na umeidhihirishia dunia kuwa wanawake wakipewa nafasi wanawezaaaa,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na wabunge hao alipokuwa akimuelezea Spika wa Bunge, Anne Makinda.
“Hata hivyo, tahadhari kubwa lazima iendelee kuchukuliwa kwani watu wenye nia mbaya kwa nchi yetu au na umoja wetu hawajaisha na hawajafurahi kwamba hawajafaulu. “Huenda wakajaribu tena. Tunachotakiwa kufanya ni kuendelea kushikamana ili hata wakijaribu tena washindwe na walegee,” alisema Rais Kikwete.
Pia Rais aliwafurahisha wabunge aliposema idadi ya wanawake imeongezeka kwa kiasi kikubwa na kutania kuwa ndiyo maana wengine wanaoa wawili wawili.
“Mtakubaliana nami kuwa katika kipindi hiki uhuru wa habari na uhuru wa watu kutoa maoni yao umepanuka sana. Tanzania kuna magazeti ya kila siku 16 na kati ya hayo ya Serikali ni mawili tu, Daily News na HabariLeo. Je, hakuna uhuru hapo?“ Rais Kikwete.
“Mwisho lakini sio mwisho wa umuhimu, naishukuru sana familia yangu. Namshukuru mke wangu Bi Salma Kikwete kwa mchango wake mkubwa ulionipa utulivu wa kutekeleza majukumu yangu. “Upo msemo kwamba, “kwa kila mwanamume mwenye mafanikio, yuko mwanamke”, nawaambia ni kweli.
Shukrani zangu, pia, kwa wanangu na wajukuu zangu kwa kunivumilia pale walipomkosa baba yao na babu yao. Karibuni mambo yatakuwa tofauti mtaniona mara kwa mara kiasi kuwa huenda mkanichoka,” alisema Rais Kikwete na kushangiliwa na wabunge.
“Ninapoagana na Bunge letu natambua kuwa baadhi ya Wabunge mnarudi kutetea viti vyenu nawatakia kila la heri. Wale wanaogombea Urais waliomo humu nawatakia kila la heri, na nawashukuru kwa kuonesha nia ya kunipokea mzigo huu mzito. Nawatakia heri katika matamanio yenu,” alisema.
Unahitaji chochote nachokipata kikufikie? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook naInstagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.