MWANANCHI
Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe (pichani) amesema kuwa chama chake hakitashirikiana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), badala yake kitasimama chenyewe kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Kauli hiyo inazima minong’ono iliyotawala miongoni mwa wanachama wa ACT-Wazalendo waliokuwa wakimuuliza Zitto kuhusu chama hicho kujiunga na Ukawa.
Zitto alimaliza uvumi huo jana jijini hapa katika mkutano na viongozi wa chama, wanachama na watiania wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu.
Alisema ACT-Wazalendo haiwezi kuungana na Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwa vile sera ya chama hicho tofauti na vyama hivyo.
“Nawaomba niwatoe hofu, Chama cha ACT-Wazalendo kitasimama chenyewe kama kilivyo, hatutaki ushirikiano,” alisema Kabwe na kuongeza:
“Najua chama chetu bado ni kichanga, kina miezi mitano tangu kuanzishwa kwake, lakini si mnajua Timu ya Soka ya Mbeya City?” aliwauliza wajumbe waliojibu: “ndiyo.”
“Ile timu ilianza kama masihara, lakini mwisho wa siku ikawa tishio kwa timu za Ligi Kuu, basi chama hiki kitakuwa hivyo,” alisema Zitto na kushangiliwa na wajumbe waliohudhuria mkutano huo.”
Alibainisha kuwa chama chake kimedhamiria kuwatumikia Watanzania na kushika dola kwa njia halali.
Alisema ACT – Wazalendo kina azimio la Tabora, ambalo ndani yake kuna kipengele namba nne, kinachozungumzia miiko na mali za viongozi kabla ya kujiunga na chama hicho na kwamba chama chochote kitakachotaka kujiunga ACT, lazima kikubaliane na kipengele hicho ili kuzuia mianya ya rushwa na uroho wa madaraka ndani ya chama.
Aliwataka wanachama kutotishika na mtikisiko wa kisiasa utakaotokea muda wowote kuanzia wiki hii, kwani ni mambo ya kawaida.
“Mtikisiko huu usiwatie presha, mtulie tena mnyooshe miguu juu, huu ni upepo wa kisiasa na wala haututoi kwenye mstari. Narudia tena viongozi wangu ACT, mkoa msiyumbishwe na hali itakayojitokeza,” alisema.
“Hatuna presha kufanya vikao vya mara kwa mara, chama kwa masilahi ya watu fulani, tutafuata ratiba yetu vizuri,” alisema Zitto.
Alisema ACT-Wazalendo kinaendeshwa na wanachama na siyo viongozi, hivyo kila uamuzi hufuata kanuni na taratibu za chama.
“Ndiyo maana kuna chama kimoja (hakukitaja), hadi leo (jana) kinapiga danadana kumtangaza mgombea wake wa urais sijui wanamsubiri atoke kwenye Sayari ya Mars,” alihoji Zitto.
Zitto alisema kuwa atashirikiana na wagombea wote watakaopitishwa na chama hicho kugombea nafasi mbalimbali ili majimbo 10 ya Mkoa wa Dar es Salaam yaende ACT-Wazalendo.
“Juzi nilikuwa Jimbo la Kigoma Mjini, kuna chama kimoja kilikuwa kinatafuta mgombea atakayewakilisha jimbo hilo maana kila anayeambiwa anakataa, kwa sababu wanasema ni ngome ya ACT-Wazalendo,” alisema.
NIPASHE
Rais wa Marekani, Barack Obama amezungumzia safari yake ya kwanza aliyoifanya Kenya, mwaka 1988 na kupoteza begi lake baada ya kushuka katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Akizungumza na Wakenya katika Uwanja wa Kasarani, jijini Nairobi, Obama alisema anamshukuru dada yake, Auma Obama kwa kumpokea katika safari hiyo miaka kadhaa iliyopita.
Obama alisema anafurahia kufika nchini humo akiwa rais wa kwanza wa Marekani.
Obama alipokwenda Kenya wakati huo, begi lake lilipotea na baada ya kufuatilia aliambiwa kwamba lilisafirishwa hadi Afrika Kusini na ndege aliyokuwa amepanda.
Katika hotuba yake, Obama alimshukuru pia Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa ukarimu wake na mapokezi makubwa aliyoyapata.
Pia aliwaomba radhi ndugu zake wa Kijiji cha Kogello kwa kutofika huko kwa ajili ya kuwasalimia.
Rais huyo alisema anatambua juhudi zilizofanywa na wazee wakati wa kupigania uhuru akiwamo babu yake ambaye alikuwa ni mmoja wa wapiganaji katika Jeshi la Kings African Riffles (KAR).
“Babu yangu alikuwa Burma akitumikia Waingereza. Baada ya vita alifungwa kwa muda kwa kupinga ukoloni,” Obama.
Rais Obama alisema ameona mabadiliko makubwa nchini humo, ikiwamo kukua kwa uchumi wa Kenya.
Alisema zamani Afrika Kusini ndiyo iliyokuwa na uchumi mkubwa, lakini sasa Kenya inakaribia kuifikia Afrika Kusini kiuchumi.
Rais Obama alisema rushwa imekuwa changamoto kubwa kwa nchi nyingi za Afrika na tatizo hilo limekuwa likisababisha ukiukwaji wa haki za binadamu na kuathiri shughuli za Serikali.
“Urasimu ni kikwazo cha utawala bora na mfumo wa utoaji haki, Serikali haina budi kujenga mazingira mazuri kwa watu wake na kupambana na rushwa,” alisema Rais Obama, huku akishangiliwa na watu waliohudhuria mkutano huo.
Alisema rushwa inarudisha nyuma maendeleo ya uchumi na aliwataka Wakenya kubadilisha mtazamo wao juu ya rushwa ili waweze kukabiliana na tatizo hilo.
Rais Obama alisema licha ya kuahidi kuwapatia kinamama na vijana mabilioni ya fedha, wasi wasi wake mkubwa ni rushwa ambayo imekuwa ikikwamisha ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo.
Pia, alizungumzia ugaidi na kuwataka Wakenya kuongeza juhudi za kupambana nao.
Obama ameahidi kushirikiana na Kenya katika kupambana na magaidi likiwamo kundi la Al-Shabaab ambalo limekuwa likiishambulia Kenya na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha.
Katika uwanja huo ambako maelfu ya watu walikusanyika kumsikiliza Rais Obama, alisema amezungumza na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu nchi hizo mbili zitakavyopambana na ugaidi.
“Kwa kiasi kikubwa tumepunguza nguvu ya Al Shabaab, lakini haimaanishi kwamba tumefanikiwa kutatua tatizo la ugaidi,” alisema Rais Obama.
Alisema Serikali ya Marekani inafurahia juhudi za Kenya katika kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi na kwamba atashirikiana na nchi hiyo katika kudhibiti makundi ya kigaidi nchini humo.
“Ugaidi ni mbaya, sasa tunaomboleza waliouawa Westgate na Garissa na katika maeneo mengine. Kenya ipo njia panda katika kufikia malengo yake,” alisema Rais Obama.
Rais Obama alilazimika kutoa kauli hiyo kutokana na mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea katika jengo la Westgate na kusababisha watu 67 kupoteza maisha na wengine 148 kufariki dunia Aprili mwaka huu kwenye Chuo Kikuu Cha Garissa baada ya Al-Shabaab kushambulia chuo hicho.
Mbali na hayo, Obama aliwataka Wakenya kuheshimu haki za binadamu na kuacha vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake, huku akionya raia wa nchi hiyo kuacha kuwaozesha wasichana wadogo.
“Mimi ni Mwafrika ninayeishi Marekani, naumia sana ninapoona watu wananyimwa haki zao kutokana na sheria kupindishwa, hili halikubaliki,” alisema.
Rais Obama aligusia suala la mapenzi ya jinsia moja, lakini Rais Kenyatta alisema kwamba suala la haki za binadamu katika upande wa mapenzi ya jinsia moja halikubaliki na kwamba, hoja hiyo haina mashiko kwa raia wa nchi hiyo.
Pia, aliwataka Wakenya kuimarisha demokrasia na kutumia fursa mbalimbali kuwawezesha vijana kuinuka kiuchumi.
Pia, aliwaonya Wakenya kuacha tabia ya kubaguana kwa majina yao ya mwisho na kutupilia mbali siasa za ukabila kwa sababu zinaharibu maendeleo ya Taifa hilo.
MWANANCHI
Licha ya Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) kupokea taarifa ya Ukawa na kuamua chama hicho kiendelee kushiriki katika umoja huo, bado suala la mgombea urais wa vyama vinavyounda umoja huo limeendelea kuwa siri nzito.
Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya CUF jana, zilisema kuwa katika kikao chake kilichoketi juzi na jana mjini Zanzibar, baraza hilo lilipokea taarifa ya Ukawa, kuithibitisha na kuamua chama hicho kiendelee na ushirikiano huo.
Pamoja na hayo, jana kutwa nzima viongozi wa Ukawa walikuwa kwenye vikao mfululizo na hakukuwa na taarifa rasmi zilizopatikana na hata mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa jana jioni uliahirishwa bila kueleza utaitishwa tena lini.
Vyanzo mbalimbali ndani ya Ukawa, vilieleza kuwa ufunguo wa hatua hiyo ulikuwa unashikiliwa na CUF, ambayo hivi karibuni ilijitenga na umoja huo ili masuala yake yajadiliwe kwanza na vikao vyake vya maamuzi kabla ya kurejea kwenye meza ya majadiliano.
Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Jussa Ismail Ladhu alipoulizwa alisema ikiwa itaamuliwa mgombea mwenza wa Ukawa atoke CUF, hakutakuwa na shida kwa kuwa chama hicho kina wanasiasa wazuri, safi na makini na kwamba kitatoa mtu ambaye Watanzania wote watafurahi.
Hata hivyo alisema baada ya kuweka vigezo vya kuwa na mgombea wa Ukawa, sasa hakuna shida kwa kuwa majimbo machache yaliyosalia utaratibu wake utatangazwa hivi karibuni.
Kuhusu mgombea mwenza, Jussa alisema CUF ina nafasi kubwa ya kutoa mgombea huyo kwa sababu ndicho chama chenye nguvu Zanzibar na kina wanasiasa mahiri na makini.
Wagombea wetu tunataka wawe ni wale watakaohakikisha kuwa Katiba Mpya inapatikana mara baada ya uchaguzi ili kuyaweka sawa mambo yanayohitaji kuwekwa sawa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba, mgombea urais na mgombea mwenza wanapaswa kutoka chama kimoja, hivyo kama Chadema itamtoa mgombea urais inabidi pia mgombea mwenza atoke chama hicho.
Habari ambazo bado si rasmi zinasema kuwa mmoja wa viongozi wa CUF anaweza kuhamia Chadema ili kukidhi matakwa hayo ya Katiba.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema kuwa mambo katika Ukawa ni mazuri, wapo waliofikiri kuwa watavurugana, lakini wamekubaliana na sasa Watanzania wasubiri kupata wagombea safi katika ngazi zote.
Habari zaidi zilizolifikia gazeti hili zilisema mshirika mwingine wa Ukawa, Chadema jana viongozi wake walikuwa katika kikao cha dharura cha Kamati Kuu kilichoshirikisha wajumbe wachache, hasa wale wanaopatikana kwa kupigiwa kura ili kuweka mambo sawa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alikiri kuwapo kwa kikao hicho.
“Kamati Kuu ya Chadema inaendelea kukutana jijini Dar es Salaam kwa kikao maalumu cha dharura kujadili mambo mbalimbali,” alisema Makene katika taarifa yake fupi aliyotuma jana usiku.
NIPASHE
Wakati kazi ya kuandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu la wapiga ikielekea katika hatua ya mwisho,imebainika kuwa baadhi ya wananchi hawafahamu mipaka ya ya majimbo yao yaliyogawanywa.
Uchunguzi ambao umefanywa na NIPASHE katika vituo vya kuandikisha wapiga kura katika jiji la Dar es Salaam umebaini kuwa licha ya wananchi kujiotokeza kujiandikisha lakini bado hawajafahamu mipaka ya majimbo yao mapya yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
Majimbo mapya katika mkoa wa Dar es Salaam yaliyotangazwa na Nec ni jimbo la Mbagala lililomegwa kutoka jimbo la Kigamboni na Jimbo la Kibamba lililokuwa sehemu ya jimbo la Ubungo.
Ramadhani Abdul mkazi wa Ubungo alisema licha ya kwamba amejiandikisha lakini bado hafahamu mpaka wa jimbo lake jipya kwasababu Nec haijafanya jitihada za kuwaelimisha.
John Kaliweka mkazi wa Mbagala alisema serikali imefanya vizuri kugawa majimbo kwa kuwa yalikuwa makubwa lakini bado kuna tatizo kwasababu mamlaka zinazohusika hazijawaelimisha wananchi mipaka.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Nec, John Malaba, akizungumza na NIPASHE alisema tume ilishatoa elimu kwa wananchi kuhusu mipaka ya majimbo hayo.
“Kama kuna wananchi ambao hawafahamu mipaka ya majimbo wawasiliane na viongozi wa Halmashauri zao watapewa maelekezo,” alisema.
Nec ilitangaza majimbo mapya 26 ya uchaguzi baada ya kugawanywa kutokana na ukubwa.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damian Lubuva alitaja majimbo hayo mbali na ya mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni Jimbo la Handeni katika Halmashauri Mji wa Handeni (Tanga), Nanyamba katika Halmashauri ya Mji Nanyamba (Mtwara), Makambako Halmashauri ya Mji Makambako (Njombe), Bitiama Halmashauri ya Wilaya Butiama (Mara), Tarime mjini Halmashauri ya Mji Tarime (Mara).
Lubuva alitaja majimbo mengine kuwa ni Tunduma lililopo katika Halmashauri ya Mji Tunduma (Mbeya), Jimbo la Nsimbo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo (Katavi), Kavuu Halmashauri ya Wilaya Mpimbwe (Katavi), Geita mjini Halmashauri ya mjini Geita (Geita), Mafinga mjini Halmashauri ya Mji Mafinga (Njombe).
Majimbo mengine ni Kahama mjini Halmashauri ya Mji Kahama (Shinyanga), Ushetu kwenye Halmashauri ya Wilaya Ushetu (Shinyanga), Nzega mjini lililopo kwenye Halmashauri ya Mji wa Nzega (Tabora), Kondoa mjini Halmashauri ya Mji Kondoa (Dodoma).
Mengine ni Newala mjini Halmashauri ya mji Newala (Mtwara), Mbulu mjini Halmashauri ya Mji Mbulu (Arusha), Bunda mji Halmashauri ya mji Bunda (Mara), Ndanda Halmashauri ya Wilaya ya Masasi (Mtwara), Vwawa Halmashauri ya Wilaya Mbozi (Mbeya), Manonga Halmashauri ya Wilaya Igunga (Tabora).
Majimbo mengine ni Mlimba Halmashauri Kilombero (Morogoro), Madaba Halmashauri ya Wilaya Madaba (Ruvuma), Ulyankulu Halmashauri ya Wilaya Kaliua (Tabora) na Mbinga mjini Halmashauri ya Mji Mbinga (Ruvuma).
Pia, aliyataja majimbo 10 ambayo yaliyobadilishwa majina majina kuwa, Jimbo la Rugwe Mashariki (Mbeya) na kuwa Jimbo la Busekelo, Jimbo la Rugwe Magharibi (Mbeya) na kuwa Jimbo la Rugwe, Jimbo la Urambo Mashariki (Tabora) litaotwa Jimbo la Urambo.
Mengine ni Jimbo la Urambo Magharibi (Tabora) na kuwa Jimbo la Kaliua, Jimbo la Njombe Mgharibi (Njombe) na kuwa Jimbo la Wanging’ombe, Jimbo la Njombe Kusini (Njombe) kwamba litaitwa Jimbo la Lupembe.
Jimbo la Bariadi (Simiyu) litaitwa Jimbo la Itilima, Jimbo la Bariadi Magharibi (Simiyu).
NIPASHE
Serikali imesisitiza kuwa haitaweza kupunguza ushuru wa uingizaji wa mabasi nchini kutoka asilimia 25 hadi 10 kwa kuwa hayo yalikuwa makubaliano ya nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, alisema hayo wakati akizungumza na NIPASHE kupata msimamo wa Serikali kufuatia wamiliki wa mabasi nchini kuitaka ipunguze ushuru huo ama kinyume chake wataitisha mgomo nchi nzima.
Mkuya alisema Serikali ya Tanzania iliiomba EAC kupunguza kodi kufikia asilimia 10 kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kasi kwa ajili ya jiji la Dar es Saalam, makubaliano ambayo yaliishia Juni mwaka huu.
“Waagizaji wa mabasi walikuwa na muda wa mwaka mzima wa kuagiza magari kwa kutumia ushuru wa asilimia 10 ambao Tanzania iliiomba jumuiya kuipunguzia ulioishia Juni mosi mwaka huu,” alisema.
Alisema baada ya kipindi hicho kumalizika hakuna namna yoyote ambayo Serikali kufanya kwani hayo ni makubaliano ya nchi wanachama na sio makubaliano ya Serikali.
Hata hivyo, Waziri Mkuya alikanusha madai ya kuwa kuna msamaha wa ushuru kwa waingizaji wa maroli nchini na kusisitiza kuwa hakuna msamaha kwa waingizaji hao kama ilivyodaiwa na baadhi ya wamailiki wa mabasi kupitia mkutano wao, isipokuwa Serikali imefuta ushuru kwa viwanda vya ndani vinavyounganisha maroli hayo.
Naye Katibu Mkuu wa wamiliki wa mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu, alisema msimamo huo wa serikali utasababisha kusimama kwa huduma.
Alisema Serikali ingetumia ushuru wa asilimia 10 ili wafanyabiashara waweze kuyaondoa mabasi yao yaliokwama bandarini kutokana na gharama kubwa za uingizaji wa mabasi kupandishwa gafla.
“Bandarini kuna mabasi zaidi ya 44 kutoka China ambayo yaliingia nchi kati ya Julai Mosi hadi 10 ambayo yamekwama kutokana na kutozwa ushuru mkubwa, serikali ingetushirikisha toka awali haya yote yasingetokea,”alisema.
Tabao walifanya mkutano mkuu uliokuwa na majadiliano kuhusu kupanda kwa gharama za ushuru wa uingizaji wa mabasi nchini ambao walikubaliana kuwa endapo Serikali isiposhusha gharama hizo wataitisha mgomo nchi nzima.
Katika mkutano huo walikubaliana kuunda kamati ya watu watano itakayoonana na Waziri wa Uchukuzi na Waziri wa Fedha kwa lengo la kujadiliana kupanda kwa gharama za ushuru wa uingizaji wa mabasi
NIPASHE
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, vimepata kigugumizi na kutupiana mpira kuhusiana na ufafanuzi juu ya madai kuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, anakiuka sheria na kanuni za uchaguzi mkuu kwa kuanza kampeni kabla ya wakati.
Dk. Magufuli amekuwa katika ziara kwenye maeneo mbalimbali nchini katika kile ambacho chama chake kinaeleza kuwa ni kumtambulisha kwa wananchi baada ya kuibuka mshindi katika mchakato mkali wa kumpata mgombea urais wa CCM uliohusisha makada 38 kitendo kinacholalamikiwa na baadhi ya wapinzani kwa madai kuwa huko ni kuanza kampeni kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanjyika Oktoba 25, mwaka huu.
Baada ya kuteuliwa kwake, Magufuli ameshafanya mikutano ya hadhara ya kujitambulisha katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Shinyanga, Morogoro, visiwani Zanzibar na pia mkoani Pwani na mara kadhaa amesikika akiahidi mambo mazuri kwa Watanzania, huku ahadi yake kubwa kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine ikiwa ni “Sitawaangusha”.
Katika kufahamu kama kinachofanywa na mgombea huyo kipo ndani ya kanuni na sheria ya uchaguzi, NIPASHE iliwasiliana na viongozi wa Nec na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa nyakati tofauti, ambao walitoa maelezo ya kutupiana mpira.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva, alipoulizwa kama kinachofanywa na mgombea urais huyo CCM ni sahihi, alisema mikutano inayofanywa na Dk. Magufuli ni ya ndani ya chama, hivyo tume hiyo haina mamlaka ya kuingilia.
Lubuva alisema NEC itaanza kuzifuata sheria na kanuni za uchaguzi Agosti 21 baada ya tume hiyo kupitisha rasmi uteuzi wa wagombea wa vyama vyote kufanyika.
“Kinachofanywa na mgombea urais wa CCM ni suala ambalo lipo ndani ya chama chao, kama tume hatuwezi kuingilia ni mambo ya ndani ya chama, uteuzi ukifanyika ndipo tume itaanza kuangalia kama kanuni na sheria zinafuatwa na wagombea, wa kuwauliza kwa sasa ni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa,” alisema.
Wakati Nec wakitoa maelezo hayo, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Sixtus Nyahoza, alisema suala la wagombea na kampeni siyo kazi ya ofisi yake bali ni Nec.
“Kwa upande wetu tunaona anayepaswa kulielezea suala la kama mgombea urais CCM anakiuka sheria ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi sababu wao ndio wanahusika na masuala ya kampeni na wagombea,” alisema.
Nyahoza alisema ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inachofahamu ni kwamba kama kuna mambo yanafanyika ndani ya chama kama vile kuitisha mkutano wa hadhara, wanachotakiwa ni kutoa taarifa polisi na hivyo suala hilo lipo chini ya ofisi hiyo.
“Sheria ya uchaguzi inasema ukitaka kufanya mkutano unatoa taarifa polisi. CCM wamekuwa wakifanya hivyo na hata Chadema wanafanya hivyo na hivi majuzi waliitisha (Chadema) mkutano Mwanza,” alisema.
Licha ya kuwapo kwa maelezo hayo ya Nec na Msajili wa Vyama vya Siasa, NIPASHE inatambua kuwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, Nec imepewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi kupitia vifungu vya 35B(1), (3) (a), 37 (1) (a) na 46 (1) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, ambayo inabainisha kuwapo kwa ratiba ya uchaguzi ikiwamo kuanza kwa kampeni. Aidha, msajili wa vyama huhusika pia na masuala ya uchaguzi kupitia Sheria ya Gharama za Uchaguzi 2010.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia amepita bila kupingwa katika mchakato wa kumtafuta mgombea ubunge jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro kupitia chama hicho.
Mbatia amepitishwa baada ya vikao vya Kamati ndogo kwenye ngazi ya matawi, kata na jimbo kumpa alama ‘A’ sawa asilimia 100 baada ya kuwa mgombea pekee aliyejitokeza kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania ubunge.
Katibu wa NCCR Mageuzi jimbo la Vunjo, Mathew Temu alisema Mbatia alipitishwa na vikao hivyo wiki iliyopita hasa kutokana na mchango wake katika chama, uwezo na nia ya kulikomboa jimbo kutoka mikononi mwa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP).
Alisema Mbatia alichukua fomu na kuirejesha Juni 29, mwaka huu.
“Waliompitisha ni wajumbe wa kikao halali cha jimbo la Vunjo; kwa kuwa mchakato huo ulianzia kwenye ngazi za matawi na Kata,” Temu.
Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR-Mageuzi, Hemed Msabaha alisema kamati ndogo zilipewa mamlaka ya kufanya uteuzi kwa niaba ya Halmashauri Kuu na hivyo jina la Mbatia lilishapitishwa rasmi.
Mbatia anakuwa kiongozi wa pili mwandamizi wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupita bila kupigwa katika mchakato wa kura ya maoni ya kiti cha ubunge baada ya juzi wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi Wilaya ya Hai, kumchagua Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kwa kura 269.
Mbowe naye alipita bila kupingwa katika mchakato wa kura ya maoni ya ubunge wa jimbo la Hai, baada ya kuvuna kura 269 sawa na asilimia 98.2.
Wakati huo huo, Mkutano Mkuu Maalum Wilaya ya Mwanga, ulimchagua Hendry Kilewo kwa kura 109, kuwa mgombea wake wa kiti cha ubunge.
Kada huyo aliwashinda Mdimu Ngoma aliyepata kura 25, Joyce Mfinanga kura 38, Mengi Kigombe kura 2 na Nurdin Jela aliyeambulia kura moja.
MTANZANIA
Mgombea Ubunge kupitia CHADEMA Zanzibar Bikwao Hamad amefariki dunia muda mfupi baada ya kumaliza kujieleza kwa wapiga kura wake.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mjini Unguja Janeth Fusi alisema alianguka ghafla wakati akitoka nje ya ukumbi baada ya kujieleza kwa wapigakura.
Alisema uchaguzi huo wa viti maalum ulikuwa ukifanyika katika makao makuu ya chama hicho.
“Bikwao alikua akitoka nje ghafla tulisikia mtu kaanguka…tulimpatia huduma ya kwanza lakini hali yake iliendelea kuzorota na tukaamua kumkimbiza hospitali na bahari mbaya alifariki dunia” Janeth.
Ripoti ya daktari ilieleza kuwa Bikwao alipata mshtuko wa damu na kumuathiri kichwani na kabla ya kifo chake alipatiwa matibabu katika hospitali ya Al0-Rahma na baadaye kuhamishiwa hospitali ya rufaa ya mnazi mmoja.
MTANZANIA
Undikishaji wapiga kura umeibua sura mpya baada ya baadhi ya wnaanchi kuanzisha biashara ya kuuza namba za nafasi za kujiandikisha katika daftari la kupiga kura BVR Dar es salaam kwa shilingi 5,000 hadi 20,000.
Baadhi ya wakazi wa Dar wamesema vitendo vya rushwa vimechangia baadhi ya wnaanchi kukata tamaa ya kujiandikisha.
Walisema baadhi ya wananchi wanajitokeza na kuwahi namba za mwanzo kisha kuanza kuziuza kwa waliochelewa waweze kujiandikisha.
“Kuna watu wamewahi alfajiri na kuchukua namba kosha kuanza kuziuza kwa watu waliochelewa kwa 500o hadi 20,000, jambo ambalo ni kinyume na sheria…Serikali inapaswa kuliangalia hili kwa makini”.
Mwenyekiti wa mtaa wa chakula bora, Hamdani Habibu alisema kutokana na mwenendo wa mchakato huo, anaiomba NEC iwe inatembelea vituo hivyo na kutatua changamoto zinazojitokeza kwa wananchi.
HABARILEO
Mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es Salaam umekamilika na wiki ijayo gesi itakuwa na uwezo wa kufika jijini Dar es Salaam.
Aidha kazi ya kufua umeme kwa kutumia gesi asilia na kuuingiza katika mifumo ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) itaanza mwezi ujao.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Kapuulya Musomba juzi wakati bodi ya shirika hilo ilipofanya ziara ya kutembelea mradi huo kwa lengo la kujionea hali halisi kabla ya gesi kuanza kusafirishwa kutoka Mtwara kuja Dar es alaam.
Musomba alisema kwamba Agosti mosi mwaka huu, gesi itakuwa na uwezo wa kufika katika mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi One na Tegeta, Dar es Salaam.
Alisema licha ya kuwa na uwezo wa kufika wiki ijayo, lakini wanatarajia gesi kwa ajili ya kufua umeme kufika katika mitambo hiyo Septemba 6 au 7 kutokana na hoja za kitaalamu za hatua ya mwanzo ya kuchakata na kusafirisha gesi.
Musomba alisema hayo akiwa katika kituo cha Somanga Fungu ambapo kuna mitambo maalumu ya kupokea gesi kutoka Songosongo na Mtwara, kisha kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam. Alisema hatua hizo zinafuatwa kwa siku 45 ili kuhakiki vifaa vyote kuwa havina tatizo kuanzia kuchimba, kuchakata na hata kusafirisha.
Alisema baada ya majaribio hayo ya kupeleka gesi Dar es Salaam kufanikiwa, Septemba 15 wataanza kuingiza umeme uliozalishwa kwa gesi asilia Tanesco ili watanzania waanze kuona matunda ya gesi na bomba lenyewe.
“Kwa sasa Tanesco wana mitambo ya kuzalisha megawati mia mbili za umeme, lakini hazifanyi kazi hivyo sisi tutaanza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi na kuingiza Tanesco megawati mia moja hamsini za umeme” alisisitiza Alisema tayari mpaka sasa wameshaajiri wafanyakazi 30 katika vituo vya mitambo ya Kinyerezi na 11 Somanga Fungu tayari kwa kuanza usafirishaji na uzalishaji katika mitambo.
Alisema katika bomba hilo la kilometa 504 ambazo ni umbali wa mradi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam una valvu zaidi ya 100, lakini kuu zipo 16 na kukitokea tatizo kwenye valvu zinafungwa kwa ajili ya usalama.
Nitakutumia stori zote ukibonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.