MTANZANIA
Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Katavi imemuhukumu mwalimu mstaafu wa shule ya msingi Mpanda Ndogo , Rashid Ndogo mwenye miaka 65 kifungo cha maisha jela baada ya kumbala mjuu wake wa miaka mitano na kumuharibu vibaya sehemu zake za siri.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda, Chiganga Ntengwa baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa na pande zote mbili za mashtaka na utetezi.
Awali katika kesi hiyo mwendesha mashtaka alidai mahakamani kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba mwaka jana majira ya saa 2 na nusu usiku nyumbani kwake katika kijiji cha Majalila.
Siku hiyo mshatakiwa alidaiwa kumbaka mjuu wake wakati amelala chumbani akiwa na mtoto wa mshtakiwa ambaye alishugudia baba yake akitenda kosa hilo la kinyama.
Siku ya tukio mke wa mshatakiwa alimwaga mume wake kuwa amekwenda kufunga zizi la mbuzi lililokuwa jirani na nyumbani kwao na mumewe kutumia mwanya huo kuingia chumbani kwa mjuu wake na kuanza kumbaka huku mwanaye akishuhudia.
Mshakiwa alikamatwa na majirani siku hiyo na kupelekwa kituo cha Polisi ambapo alifunguliwa mashtaka huku mjukuu wake akikimbizwa hospitali kupatiwa matibabu.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Dar limebaini mabaki ya mwili wa mmiliki wa shule ya Mtakatifu Zion, Anna Mizinga aliyeuawa Desemba mwaka jana na kutupwa kwenye shimo la choo cha shule yake.
Kamanda wa Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam Suleiman Kova alisema mabaki ya mwili huo yalibainika Juni mwaka huu na tayari watu watatu wanashikiliwa na Polisi wakidaiwa kufanya unyama huo.
Akifafanua juu ya tukio hilo Kova alisema Februari mwaka huu mtu mmoja alitoa taarifa polisi juu ya kupotea kwa mmiliki huyo tangu Desemba mwaka jana saa 11 jioni na hakuonekana tena.
Alisema mmiliki huyo alindoka nyumbani kwake na gari dogo aina ya Verosa akiwa na mtu mmoja ambaye naye ni miongoni mwa watuhumiwa wanaoshikiwa na jeshi hilo na abada ya taarifa hiyo walifungua jalada la uchunguzi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.
Alisema mtuhumiwa wa kwanza alikamatwa Uchira, Moshi na kuwataja wenzake.
“Katika mahijiano mmoja alisema yeye na marehemu waliondoka hadi shuleni kwake na walipofika walivamiwa na watu wapatao wanne na kuanza kupigwa, lakini yeye alifanikiwa kutoroka na kujificha katika uzio wa shule, na aliwaona watu hao wakiendelea kumpiga mama huyo na kisha kumtupa katika shimo la choo kisha kutokomea na gari lake kusikojulika” Kova.
Watuhumiwa hao wanaendele kuhojiwa ili kupata undani wa tukio hilo, ikiwa ni pamoja na kuwatafuta na kuwakamata watuhumiwa wengine wanaohusika na tukio hilo.
MTANZANIA
Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa amemaliza safari yake ya kusaka wadhamini katika Mikoa yote ya Tanzania na kujikusanyia zaidi ya wadhamini laki 8.
Lowassa alianza safari ya kusaka wadhamini Juni 4 baada ya kuchukua fomu ya kugombea Urais kupitia CCM na jana amehitimisha safari yake hiyo katika Mkoa wa Morogoro.
Hata hivyo kwa mujibu wa kanuni za CCM, kada anayewania kugombea Urais, anatakiwa kuwa na wanachama waliomdhamini 450 kutoka Mikoa 15 ikiwemo mitatu kutoka Zanzibar.
Katika baadhi ya Mikoa ambayo Lowassa alipata wadhamini wengi ni pamoja na Dar es salaam, Arusha, Morogoro, Pwani, Iringa, Mbeya, Ruvuma , Kilimanjaro, Tanga na Singida.
MWANANCHI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeahirisha kwa muda uandikishaji wa wapigakura katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hadi hapo itakapotangazwa.
Uandikishaji huo unaofanywa kwa teknolojia inayochukua alama na taswira za mpigakura ‘Biometric Voters Registration’ (BVR)) ulipangwa kuanza Julai 4 hadi 16 kwa Dar es Salaam na Juni 25 kwa Mkoa wa Pwani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Mallaba alisema jana kuwa kazi hiyo imeahirishwa kutokana na kuchelewa kwa vifaa vinavyotumika kuandikisha wapigakura.
Alisema vifaa vilivyokuwa vinakusudiwa kutumika Dar es Salaam bado vinatumiwa katika mikoa ambayo wananchi wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“Mwitikio umekuwa mkubwa ndiyo maana tumeamua kusogeza mbele tarehe ili wamalizie huku tukiendelea kusubiri vifaa. Tunataka vikija tuishambulie Dar es Salaam kwa kipindi kifupi,” Mallaba.
Mallaba alisema tarehe ya kuanza tena kwa kazi hiyo kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani itatangazwa na NEC baada ya kupata vifaa kutoka mikoa itakayokuwa imekamilisha uandikishaji.
“Ninaomba wananchi wafahamu kuwa mwezi uliokuwa umepangwa na NEC kukamilisha zoezi hilo utabaki kuwa Julai. Tarehe tu ndiyo itabadilika,” alisema na kusisitiza kuwa wanataka uandikishwaji kwa jiji hilo uwe wa kipekee ukiwa na vifaa vya kutosha kutokana na idadi kubwa ya watu. Aliwataka wananchi wote wa mikoa hiyo miwili kuwa watulivu wakati huu.
Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), John Mnyika alisema NEC imedhihirisha hoja aliyowahi kuitoa bungeni kwamba Bunge liahirishwe ili wajadili suala hilo kwa dharura.
“Kuna udhaifu mkubwa kwa upande wa NEC na Serikali kuhusu BVR… hata baada ya madai kwamba umerekebishwa lakini ukweli ni kwamba hali ni tete hata katika maeneo mengine ambayo uandikishaji unaendelea,” Mnyika.
Alieleza kuwa Dar es Salaam ndiyo itakayoamua mshindi wa urais katika Uchaguzi Mkuu ujao kutoka na idadi kubwa ya wapigakura.
Alidai kwamba kubadilishwa huko kwa ratiba kutatoa mwanya kwa CCM ambayo ilishasema kupitia kwa Nape Nnauye kuwa inajiandaa kufunga goli la mkono kufanya hujuma.
MWANANCHI
Mahakama ya Mkazi Kisutu jana ilishindwa kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa milioni 207 kutoka kwenye akaunti ya madeni ya nje EPA kutokana na mshtakiwa wa tatu kulazwa katika hospitali ya Muhimbili, kitengo cha wagonjwa wa akili.
Hukumu ya kesi hiyo inayowakabiliwa makada watatu wa CCM, Rajabu Maranda na wenzake wanne, sasa itasomwa kesho kutokana na kulazwa kwa mtuhumiwa huyo, Iman Mwakosya ambaye alikuwa mkuu wa kitengo cha madeni ya nje cha benki kuu ya Tanzania.
Wengine kwenye jopo hilo ni Ignas Kitusi na Eva Nkya.
Mahakama itaandika barua kwa hospitali ya Muhimbili kabla ya Julai Mosi kwa ajili ya kupata taarifa kama mshtakiwa huyo anaweza kuelewa mwenendo wa kesi ili waweze kusoma hukumu.
NIPASHE
Magonjwa yasiyoambukiza yakiwamo ya kisukari, moyo na saratani, yanazidi kuongezeka kwa kasi na kuendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo duniani kote.
Aidha, inakadiriwa kuwa kisukari pekee kimeathiri maisha ya watu takribani milioni 371 duniani kote huku asilimia 80 ya idadi hiyo ikiishi katika nchi zenye uchumi wa kati na maskini.
Nchini Tanzania, takribani watu tisa kati 100 wana ugonjwa wa kisukari na kwamba mtu mzima mmoja kati ya watatu, ana tatizo la shinikizo la juu la damu.
Kaimu Mkurugenzi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Hauson Rweumbiza, alisema wakati wa semina ya siku moja iliyowashirikisha waandishi wa habari wa kutoka vyombo mbalimbali.
Lengo la semina hiyo lilikuwa ni kuzungumzia magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza.
Alisema gharama ya kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza duniani kote ni mabilioni ya dola na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa rasilimali finyu zilizopo.
“Kwa mwaka 2010, Shirika la Afya Duniani lilikadiria kuwa jumla ya gharama zinazohusiana na kisukari zilifikia Dola bilioni 378 duniani kote na kiasi hicho cha fedha kinaweza kufikia Dola bilioni 490 ifikapo mwaka 2030,” alisema.
Naye Mratibu kutoka Taasisi ya Kisukari hapa nchini, John Gadina, alisema utafiti uliofanyika mwaka 2012, ulionyesha kuwa asilimia tisa ya Watanzania waligundulika kuwa na kisukari huku Wilaya ya Temeke ikiongoza.
Alisema ugonjwa huo umewakumba vijana na watu wenye umri mkubwa na kwamba serikali mpaka sasa imefikia kutoa huduma hiyo kwa asilimia 75 ambapo kila palipo na hospitali panakuwa na kitengo cha kutoa huduma za ugonjwa huo.
Alisema sababu ya Wilaya ya Temeke kuwa na wagonjwa wengi imetokana na ulaji kwa wingi wa vyakula vya nazi, chapati, wali pasipo kufanya mazoezi.
JAMBOLEO
Serikali imekanusha taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii, kuwa kuanzia kesho na keshokutwa kutakuwa na uhaba wa mafuta kwenye vituo vya kuuza mafuta.
Kauli hiyo ya kukanusha imetolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Charles Mwijage wakatia kijibu swali lililoulizwa na Job Ndugai jana Bungeni, Dodoma.
Ndugai alimtaka Waziri kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa ambazo zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba kaunzia kesho kutakua na tatizo la upatikanaji wa mafuta na kusababisha shughuli nyingi kusimama.
Mwijage alisema taarifa ambazo wanazo kama Wizara ni kuwa hifadhi ya mafuta ipo ya kutosha na kuwa uhaba wa mafuta hauwezi kutokea kwa kuwa wana uhakika kuwa mafuta yapo ya kutosha.
Alisema hata yeye ameonakwenye mitandao ya kijamii na sasa wanafuatilia ili kujuab chanzo cha taarifa hizo ni nini.
lisema iwapo kuna msambazaji au mfanyabiashara atajaribu kufanya hivyo kanuni kanuni na sheria zilizopo zitatumika kuhakikisha wahusika wanawajibishwa.
HABARILEO
Walimu wawili wapya wa Shule ya Msingi Sang’ang’a kata ya Pemba tarafa ya Inchugu wilayani Tarime, mkoani Mara wanashikiliwa nchini Kenya kwa kosa la kuingia nchini humo bila kuwa na kibali.
Walimu hao wawili ambao ni Ahedius Orio kutoka mkoa wa Kilimanjaro na mwenzake Elias Nandi kutoka Lindi wanashikiliwa na polisi nchini Kenya walipokwenda nchini humo kwa matembezi.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Sweetbard Njewike alithibitisha kukamatwa kwa walimu hao wawili wapya wa shule ya msingi Sang’ang’a iliyopo umbali wa kilometa moja kutoka mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Kamanda huyo alisema walimu hao katika kipindi hiki cha likizo, mwishoni mwa wiki waliamua kwenda kutembelea kijiji jirani cha Nyametaburo Kipimo ambacho kiko upande wa Kenya.
Alisema wakati wakiwa kijijini hapo walikutwa na Polisi wa nchi hiyo na kuwapeleka, kituo cha Polisi na Uhamiaji cha Isebania kuwahoji ambapo ilidaiwa waliingia nchini humo bila ya kufuata taratibu za kuwa na vibali vya kuingia nchini humo.
“Tumewasiliana na wenzetu wa nchini Kenya ambapo wamedai kuwapeleka mahakamani kujibu shitaka la kuingia nchini humo bila vibali na wanatakiwa ndugu zao ama marafiki wakawadhamini huku juhudi za kuwasaidia walimu hao zinafanyika ili waweze kuachiliwa,” Njewike.
Awali habari zilizotangazwa na vyombo vya habari vya Kenya, ikiwemo televisheni na redio za Citizen zilitangaza kuwa walimu hao walidaiwa kuwakusanya na kuwashawishi vijana wakiwemo kutoka Tanzania na Wakenya kujiunga na vikundi vya kigaidi vya al Shabaab.
Unahitaji chochote nachokipata kikufikie? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook naInstagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie