MTANZANIA
Bunge limepitisha wenyeviti wake watatu, huku wabunge wa upinzani wakihoji kuhusu uadilifu wa Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM).
Wabunge wengine waliopitishwa kuwa wenyeviti ni wabunge wa viti maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa na Najma Giga wote kutoka CCM.
Wenyeviti hao walipitishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uongozi iliyokutana Januari 24 mwaka huu.
Chenge maarufu kama ‘Mzee wa vijisenti’ amekuwa akitajwa katika kashfa mbalimbali za ufisadi ikiwamo ya ununuzi wa rada mwaka 2008.
Chenge aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika utawala wa awamu ya tatu na Waziri wa Miundombinu katika awamu ya nne, alitajwa pia kuhusika katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyovuma kipindi cha mwisho cha uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Kupitishwa kwa Chenge anayejulikana pia kama ‘Nyoka wa Makengeza’ kugombea uenyekiti wa Bunge jana, kulizua mtafaruku hasa kwa wabunge wa upinzani wakihoji kuhusu uadilifu wake.
Spika wa Bunge, Job Ndugai alilazimika kumkingia kifua kutokana na baadhi ya maswali yaliyoulizwa na wabunge hao.
Akihoji uhalali wa Chenge kugombea nafasi hiyo, Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema), alisema kama Bunge likijadili suala la Escrow mwenyekiti huyo atafanyaje.
“Katika Bunge lililopita uliwajibishwa kwa kashfa ya Escrow, Je, siku kashfa hiyo ikiibuka bungeni utakuwa tayari kuisimamia?” alihoji Mwambe.
Hata hivyo, Spika Ndugai licha ya kuruhusu swali hilo kujibiwa alisema hilo siyo swali.
Akijibu swali hilo, Chenge alisema ikitokea suala la Escrow litajadiliwa bungeni atalazmika kukaa pembeni kuondoa makandokando.
“Bunge letu linaongozwa na kanuni… ikitokea kuna jambo linalokuhusu, unafuata kanuni, unakaa pembeni kuondoa makandokando katika Bunge,” alisema Chenge.
Swali jingine lililohusu kashfa ya Escrow liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Latifa Chande (Chadema), lakini akikuta akigonga mwamba baada ya Spika Ndugai kulikataa.
“Tunajua wewe ulitajwa katika kashfa ya Escrow na uliwajibishwa, sasa utawezaje kushika nafasi ya uenyekiti wa Bunge…” alisema Chande huku akikatishwa na kelele za wabunge wa CCM waliopinga swali hilo kuulizwa.
Kwa upande mwingine wabunge wa CCM nao waliinuka na kutaka kumhoji Chenge huku wakiepuka kugusa swali la Escrow, akiwamo Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM), aliyeuliza kuhusu Kanuni ya 64 inayokataza lugha za kuudhi bungeni.
“Kanuni ya 64 inayokataza watu kusema lugha za kuudhi au matusi imekuwa ikikiukwa na baadhi ya wabunge, utafanyaje kuisimamia?” aliuliza Mbogo.
Akijibu swali hilo, Chenge aliwataka wabunge kusema ukweli kwa kila watakayoyatoa.
Mbali na Chenge, Spika Ndugai pia alionekana kumbeba Najma Giga dhidi ya swali la Mbunge wa Babati Mjini, Paulina Gekul (Chadema), aliyeuliza kuhusu kanuni inayokwaza wabunge kuchangia mijadala ya bajeti.
Spika Ndugai aliingilia swali hilo baada ya Giga kuonyesha kusita kulijibu akisema kanuni zote zitasimamiwa kwa usawa.
Dk. Mary Mwanjelwa ambaye ni mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Mbeya ndiye aliyekuwa wa kwanza kujieleza na kuulizwa maswali akifuatiwa na Chenge kicha akafuatia Giga.
Baada ya kujieleza, Spika Ndugai aliwahoji wabunge kama wanaafiki na kusema walioafiki ni wengi hivyo wakapitishwa.
NIPASHE
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amehoji kitendo cha kuchukuliwa kwa askari wa Tanzania Bara na kupelekwa Zanzibar kwa ajili ya kupiga kura.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Mbowe ambaye ni Mbunge wa Hai (Chadema), alisema kumekuwapo na utamaduni wa kuwatumia askari kutoka Tanzania Bara na kuwapeleka Zanzibar na kuwaandikisha wakati wa uchaguzi ili kuwatumia kupiga kura katika mazingira ambayo hayapo wazi.
“Je, waziri una taarifa ya upelekaji wa vikosi Zanzibar kwa jukumu moja la kupiga kura na baada ya hapo wanarudishwa bara?,” alihoji Mbowe.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussen Mwinyi, alisema jambo hilo haliwezekani kwani utaratibu wa kupiga kura upo wazi na unaeleweka.
”Huwezi kwenda leo Zanzibar na kuandikishwa kupiga kura, lazima uwe ni Mzanzibari mkazi, hilo lipo na ushahidi tunao wanajeshi wanaopelekwa Zanzibar ni kwa ajili ya kulinda usalama tu nyakati za uchaguzi si zaidi ya hapo,” alisema Dk. Mwinyi.
Alisema majeshi yaliyopo ni ya Muungano na kwa maana hiyo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania anaweza kupangiwa kufanyakazi sehemu yoyote ya Jamhuri ya Muungano.
Awali, akijibu swali la msingi la Mbunge wa Jimbo la Shaurimoyo (CCM), Mattar Salum, aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa utoaji ajira kwa vijana waliopata mafunzo ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU),
Dk. Mwinyi alisema Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania lina utaratibu wa kuandikisha askari wapya kupitia makambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU).
Alisema jeshi hilo hutoa nafasi za ajira katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, ambako vijana husajiliwa kwa utaratibu uliowekwa na wale wanaofaulu hupelekwa katika makambi ya jeshi hilo.
Katika swali jingine la nyongeza, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Sale, alimtaka waziri huyo kueleza kama ana taarifa ya kuwapo kwa rushwa kubwa zinazotolewa katika kutoa ajira kwenye nafasi za vikosi vya ulinzi.
Dk. Mwinyi alisema hana taarifa juu ya suala hilo na kumtaka Mbunge huyo kumpatia majina ya wanaohusika na upokeaji wa rushwa ili hatua ziweze kuchukuliwa.
NIPASHE
Baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, kuipiga chini kesi iliyokuwa ikimkabili mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Esther Bulaya, wadai katika kesi hiyo wanatarajiwa kupinga uamuzi huo Mahakama ya Rufani.
Akizungumza na Nipashe jana, mwanasheria wa wadai hao, Constantine Mutalemwa, alisema wateja wake hawajaridhika na hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Gwae.
Juzi katika mahakama hiyo, Bulaya aliwashinda wakazi wanne wa jimbo hilo waliofungua kesi ya kumpinga baada ya ushindi alioupata kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana. Katika uchaguzi huo, Bulaya olimshinda mpinzani wake, Stephen Wasira wa CCM.
Bulaya, katika kesi hiyo, alikuwa akitetewa na mwanasheria maarufu, Tundu Lissu.
Waliofungua kesi hiyo ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malagira, ambao walikuwa na mawakili wawili ambao ni Mutalemwa na Denis Kahangwa.
Mutalemwa alisema baada ya kutoridhika na uamuzi huo, wateja wake wamekusudia kufungua kesi Mahakama ya Rufani ili kupata ufafanuzi wa Jaji juu ya uhalali wao wa kutokuwa na mamlaka kisheria ya kufungua kesi kama hiyo.
Katika hatua nyingine, kesi ya madai iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na mbunge wa zamani wa Nyamagana (Chadema), Hezekiah Wenje, jana iliahirishwa hadi Februari 2, mwaka huu.
Uamuzi wa kuahirisha kesi hiyo, ulitolewa na Jaji Joaquine De Mello wa mahakama hiyo, aliposikiliza kwa muda kabla ya kupangiwa jaji wa kuisikiliza kesi hiyo ya kupinga ushindi wa Stanslaus Mabula (CCM).
NIPASHE
Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, imetoa uamuzi wa kusimamisha mchakato wa bomoabomoa kwa siku 60 kwa wakazi wa mabondeni zaidi ya 600, ili wajitathimini kama wanaweza kufungua kesi ya msingi dhidi ya serikali.
Uamuzi huo ulitolewa jana mahakamani hapo jijini Dar es Salaam mbele ya Mwanasheria wa Serikali, Grace Mbunda na Wakili wa waombaji, George Mwalali na Jaji Penterine Kente, kuhusu maombi ya wakazi hao ya kupinga kubomolewa nyumba zao pamoja na kutaka kufungua kesi ya msingi.
Awali, Jaji Kente alisema uamuzi wa maombi hayo utatolewa kwa njia mbili kutokana na mgawanyiko wake, ukiwamo wa kutoa amri kwa Manispaa ya Kinondoni, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), kutobomoa nyumba hizo.
Katika uamuzi huo uliochukua takribani saa moja, Jaji Kente alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, mahakama imekubali ombi la wananchi hao kufungua kesi ya msingi, lakini limekubaliwa kwa masharti.
Alisema kutokana na ugumu uliopo katika shauri hilo, mahakama imetoa siku 60 zitakazoisha Machi 27, mwaka huu kwa ajili ya walalamikaji hao kuangalia uwezekano wa kufungua kesi dhidi ya serikali.
Jaji Kente alieleza kuwa hatua ya kutoa uamuzi huo inatokana na mahakama kufuata misingi ya haki za binadamu kutokana na wakazi hao kushindwa kutimiza baadhi ya masharti yaliyotolewa.
Akibainisha masharti hayo, Jaji Kente alisema la kwanza ni kuhusu waombaji hao kama wanaonyesha wana kesi dhidi ya serikali, pia kama kuna uzito wa kufungua kesi hiyo kwa misingi ya haki kwamba inaangukia wapi sambamba na waombaji hao kama watapata hasara isiyopingika.
Baada ya kueleza hayo, alisema kuwa katika masharti yote waombaji hao wamekidhi sharti la mwisho la kwamba kama watapata hasara isiyopingika kutokana na kuvunjiwa nyumba zao.
“Katika hayo, suala kubwa ni hilo la kupata hasara kutokana na kupoteza nyumba na mali, lakini pia tunaweza kujiuliza kutokana na hoja za serikali kama nyumba ni muhimu kuliko binadamu,” alisema.
Pia, alieleza kuwa inajulikana kama mchakato huo utasababisha maumivu makali kwa watu hao kutokana na kukosa makazi na kwamba itaumiza sana kuona familia za kipato cha chini zikiwa zinahangaika kwa kuvunjiwa nyumba.
Kuhusu serikali mara baada ya kuisha kwa siku hizo 60, Jaji Kente alisema inaweza kuendelea na mchakato huo mara baada ya kuisha kwa siku hizo, Machi 27, mwaka huu.
NIPASHE
Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), inatarajia kuwafikisha makahamani watumishi wa umma na wafanyabiashara kwa tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya Sh. trilioni 22.
Miongoni mwa watuhumiwa hao ni waliohusika katika kashfa ya kifisadi ya malipo tata ya dola milioni sita (Sh. bilioni 12.6) kwenda kwa Kampuni ya EGMA.
Uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo umeshakamilika na kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuombewa kibali cha kuwafikisha mahakamani.
Kadhalika, Takukuru imekamilisha uchuguzi wa sakata la ununuzi wa mabehewa feki ya kubebea kokoto ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na kuomba kibali cha DPP kuwafikisha mahakamani watuhumiwa waliobainika kujihusisha na rushwa na ukiukwaji wa sheria, taratibu na Sheria ya Ununuzi wa Umma katika mabehewa hayo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola, aliyasema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu kesi kubwa 36 za rushwa na ufisadi zinazowahusu vigogo wa serikali na wafanyabiashara, ambapo kati ya hizo nne wameshazikamilisha.
Mlowola alisema miongoni mwa kesi hizo ni ya hati fungani, inayoihusiha Kampuni ya EGMA na Benki ya Stanbic, ambapo katika uchunguzi wamebaini kwamba fedha hizo zilitakatishwa na watumishi wa umma wasio waaminifu wakishirikiana na baadhi ya watu kutoka sekta binafsi huku wakifahamu fedha hizo wamezipata kwa njia haramu.
EGMA ni kampuni iliyopewa kazi ya ushauri elekezi katika mauzo ya hati fungani za dola milioni 600 (Sh. trilioni 1.3) ambazo Serikali ya Tanzania iliziuza kwa Benki ya Standard ya Uingereza, wamiliki wake wakiwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, Gasper Njuu na aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Mitaji ya Umma Tanzania, Dk. Fratern Mboya, ambaye kwa sasa ni marehemu.
“Tuko kwenye hatua nzuri kukamilisha uchunguzi huu na watuhumiwa wote bila kujali hadhi au nafasi ya mtu pamoja na taasisi zilizohusika watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria,” alisema Mlowola.
Fedha hizo, dola milioni sita (Sh. bilioni 12.6), ziliingizwa kweye akaunti ya EGMA na ndani ya siku 10, zilitolewa kupita Benki ya Stanbic kinyume cha taratibu za kibenki.
Baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya ukaguzi katika Benki ya Stanbic, ilitoa taarifa kwa Serikali ya Uingereza kupitia Taaasisi ya Kupambana na Rushwa Kubwa Uingereza (SFO) ambayo ilianzisha uchunguzi uliosababisha kesi kufunguliwa.
Mahakama hiyo iliamuru Serikali ya Tanzania irejeshewe dola za Marekani milioni saba (Sh. Bilioni 15.03) baada ya kubainika kuwapo kwa udanganyifu huo.
Baada ya kesi hiyo kufunguliwa kwenye mahakama hiyo na SFO, ilibainika kwamba asilimia moja ya mkopo huo ambayo ni dola milioni sita (Sh. bilioni 12.6) zililipwa kwa EGMA.
Hadi sasa BoT imeitoza Benki ya Stanbic faini ya Sh. bilioni tatu kwa kosa la kukiuka taratibu za kibenki.
Kuhusu kesi ya mabehewa ya kokoto ya TRL, shauri hilo limeshakamilika uchunguzi wake na jalada limeshapelekwa kwa DPP kuomba kibali cha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote waliobainika kujihusisha na matendo ya rushwa.
Mabehewa hayo 274 yaliingizwa nchini kupitia kandarasi ya Kampuni ya M/S Hindustan Engeneering and Industrial Ltd ya India yaliyokuwa na thamani ya dola 28,487,500 (Sh. bilioni 61.2).
MWANANCHI
Mwili wa kijana, Abel Machanga mwenye miaka 24, aliyefariki dunia Desemba 31, mwaka jana katika Hospitali ya Colombia Asia, India umekwama baada ya ndugu wa marehemu kukosa fedha za kulipa deni la Sh35 milioni wanazodaiwa na hospitali hiyo.
Takribani siku 27 zimekatika tangu kijana huyo afariki na kwa muda wote huo, baba yake; Revocatus Machanga amekuwa akihaha kuomba msaada.
Abel alifariki dunia baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe wa kichwa aliogundulika kuwa nao tangu 2015 na Julai mwaka jana, gazeti hili lilichapisha habari ya maradhi yake hatua iliyosaidia kupatikana kwa dola 7,700 za Marekani zilizohitajika kwa ajili ya matibabu yake India.
Mara baada ya kufika India na kufanyiwa vipimo, uongozi wa hospitali hiyo ulitaka kuongezewa dola 5,000.
“Tulijichangisha nikatuma fedha hizo matibabu yakaanza. Novemba 30 mwaka jana, alifanyiwa upasuaji alipokuwa bado kwenye uangalizi waligundua kuwa ana degedege, bakteria karibu kila sehemu ya mwili wake na shinikizo la damu kushuka kupita kiasi,” alisema na kuongeza wakati wakiendelea kumhudumia, waligundua maradhi mengine hivyo kudai kuongezewa dola 16,396 sawa na Sh35milioni.
“Nilikwenda Wizara ya Afya kuomba msaada, waliniahidi kuna taarifa walimuagiza mwambata wao aliyekuwa India kufuatilia.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Nsachris Mwamaja alisema hana taarifa kuhusu suala hilo na kuahidi kulitolea ufafanuzi wa kina leo.
MWANANCHI
Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) waliokumbwa na ‘operesheni tumbua majipu’, walikutwa na mali nyingi “kupita maelezo”, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.
Operesheni hiyo, ambayo inatekelezwa tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, juzi ilimkumba Dickson Maimu, ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Nida, Joseph Makani (Mkurugenzi wa Tehama), Rahel Mapande (Ofisa Ugavi Mkuu), Sabrina Nyoni (Mkurugenzi wa Sheria) na George Ntalima ambaye ni Ofisa Usafirishaji.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alisema hatua ya kutengua na kusimamisha watumishi hao imechukuliwa baada ya uchunguzi wa hali ya juu kwenye mamlaka hiyo.
Ingawa hakutana kuingia kwa undani akihofia kuingilia uchunguzi, Kitwanga alisema katika uchunguzi wao, moja ya hatua ilikuwa ni kukamata mali za wafanyakazi hao wa Nida.
“Walipoulizwa, walisema wamepata mali hizo kutokana na mikopo, hivyo uchunguzi utajielekeza katika kulinganisha kiwango cha mikopo na mali walizonazo,” alisema.
Waziri huyo alisema uchunguzi zaidi unajielekeza katika ni jinsi gani Sh180 bilioni zilitumika kusajili watu milioni sita tu na kati yao kuwapata vitambulisho watu milioni 2.5 tu.
“Ninayo taarifa niliyopewa na Nida ikionyesha kwamba imepanga ofisi nyingi Dar es Salaam zisizo na matumizi na wakati fulani walinunua ‘seva’ 100 zisizo na matumizi,” alisema.
“Haielezeki, NEC ilitumia kiasi kama hicho kuandikisha watu milioni 20 katika miezi isiyozidi mitano, lakini Nida wametumia Sh180 bilioni kuandikisha watu milioni 2.5 kwa miaka mitatu.”
Mbali na kuwaweka kando watendaji hao, Rais aliagiza vyombo mbalimbali kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha katika mamlaka hiyo.
Vyombo vilivyoagizwa ni pamoja na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti ya Ununuzi ya Umma (PPRA).
Vyanzo mbalimbali vilivyozungumza na gazeti hili vilisema suala la Vitambulisho vya Taifa lilikuwa linazungumzwa katika maeneo mengi nchini, hasa kutokana na vitambulisho hivyo kutopatikana haraka na kuonekana vya kawaida.
HABARILEO
SERIKALI imezindua rasmi mradi unaofadhiliwa na Global Fund kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 13 (Sh bilioni 27.3) unaolenga kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi na Kifua Kikuu (TB) katika mikoa 14 yenye kiwango cha juu cha maambukizi.
Akizindua mradi huo Dar es Salaam jana kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Afya katika wizara hiyo, Dk Hellen Semo alisema mradi huo utasimamiwa na Shirika la Kimataifa la Save the Children na taasisi nyingine nne zinazojishughulisha na afya.
Alisema mradi huo umelenga kufanikisha malengo makubwa mawili ambayo ni kuzuia maambukizi na huduma za tiba kwa ugonjwa wa Ukimwi na kupunguza kasi ya maambukizi kwa asilimia 25 na vifo vnavyotokana na magonjwa ya TB na ukoma kwa asilimia 50 hadi ifikapo mwaka 2020.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Save the Children, Steve Thorne alisema shirika hilo litasimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na mashirika mengine matatu ambayo ni Taasisi ya Benjamin Mkapa, Shirika la Utafiti wa Tiba na Afya barani Afrika (AMREF) na Shirika lisilo la Kiserikali la AFRICARE.
Alitaja baadhi ya mikoa ambayo mradi huo utatekelezwa kuwa ni Rukwa, Kigoma, Kagera, Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Mbeya, Njombe, Tabora, Mwanza, Dar es Salaam na Pwani.
Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.