Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anayewakilisha vyama vinavyounda Ukawa, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsindikiza wakati akienda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ni salamu kwa CCM na ‘wameisoma namba’ kwamba Watanzania wanataka mabadiliko.
Akiwahutubia mamia ya wafuasi wa vyama vinavyounga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Ofisi za Makao Makuu ya Chadema jana, Lowassa aliyeonekana kuwa na furaha muda wote, alisema maandamano waliyoyafanya hayajawahi kutokea katika historia ya Tanzania.
“Haijatokea katika historia ya nchi yetu maandamano makubwa ya aina ile, nimefurahishwa na vijana wametembea kutoka Buguruni hadi Kinondoni na hamjachoka nawapongeza sana, asante sana,” Lowassa.
Alisema ana mambo mawili ya kusema; kwanza kuwashukuru wafuasi na wapenzi wa Ukawa kwamba kwa kujitokeza kwa wingi wamepeleka meseji moja kwa wasiowatakia mema, wanaosema CUF na Chadema ni watu wenye fujo, wamethibitisha kwamba si kweli.
“Tumewahakikishia kuwa sisi ni watu wenye nidhamu na uwezo, Mwenyezi Mungu akipenda Oktoba tunachukua nchi asubuhi peupeee, kwa hiyo watu wasitafute visingizio, watafute vingine, watoto wa mjini wanasema wameisoma namba,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati wa watu.
Akizungumzia jambo la pili, mbunge huyo wa Monduli aliyejiondoa CCM siku 15 zilizopita, alisema anauchukia umaskini kiasi kwamba anauona kama ukoma.
Lowassa ambaye mara nyingi husema hajakutana barabarani na Rais Jakaya Kikwete, alisema rafiki yake huyo ndiye aliyeharibu uchumi wa nchi, lakini akasema asingetaka kutoa mashtaki bali kutoa takwimu za hali ilivyobadilika.
“Wakati Rais Benjamini Mkapa anaondoka madarakani, bei ya sukari ilikuwa Sh650, leo ni Sh2,300, kutoka 650 hadi 2,300 ameharibu uchumi, hajaharibu?” aliuliza na kujibiwa, “ameharibuuu.”
“Bei ya mchele ilikuwa Sh550 leo Sh2,200, ameharibu uchumi, hakuharibu? Sembe kilo ilikuwa Sh250 leo ni Sh1,200, ameharibu hakuharibu?” alihoji Lowassa na watu wakamjibu ‘ameharibuuu” na kisha akaongeza kuwa kwa sababu hizo, CCM haistahili kuendelea kutawala.
Lowassa alitumia fursa hiyo kuwaalika wanachama wa CCM wasioridhika na hali ilivyo kujiunga na Ukawa kwa kuwa inawezekana kutafuta mabadiliko nje ya chama hicho na kwamba wasione haya bali waangalie idadi kubwa ya vijana waliojitokeza jana.
Mgombea huyo, alisema Tanzania imeshuhudia uporaji mkubwa wa mali za Taifa, ambapo tembo wameuawa kuliko wakati mwingine wowote, hivyo kutokana na vitendo hivyo, CCM haistahili kuendelea kutawala.
Alisema amesikia maneno kuwa kuna mchezo wa watu wanapita mitaani wanachukua shahada za kupigia kura za wanajeshi, askari magereza wanachukua namba.
MWANANCHI
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe jana aliugua ghafla akiwa katika maandamano ya kumsindikiza mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa baada ya kuchukua fomu za kugombea urais katika Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC).
Mbowe alishiriki katika maandamano yaliyoanzia Makao Makuu ya CUF yaliyopo Buguruni wilayani Ilala kuelekea NEC na baada ya Lowassa kuchukua fomu, mwenyekiti huyo aliendelea na msafara kwenda Kinondoni yalipo makao makuu ya Chadema.
Wakiwa njiani Mbowe na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu walikuwa wamechomoza kwenye gari wakiwapungia wananchi waliojitokeza kwenye maandamano hayo.
Hali ya Mbowe ilibadilika ghafla na aliamua kushuka juu ya gari na kukaa katika kiti, ndipo Lissu na watu waliokuwamo kwenye gari hilo wakaanza kumpatia huduma ya kwanza kwa kumfungua vifungo vya shati lake katika eneo la Kinondoni kwa Manyanya.
Wakati hali ya Mbowe ilipoanza kubadilika msafara wa Lowassa ulikuwa ukielekea katika Uwanja wa Biafra, Kinondoni na magari yalikuwa yakitembea mwendo mdogo kutokana na maelfu ya watu waliokuwa wakiandamana.
Wakati maandamano hayo yakiendelea, gari lililombeba Mbowe likiwa na walinzi wa Chadema walioning’inia milangoni, lilichomoka katika msafara huo ambao ulikuwa umeingia Barabara ya Kawawa na lilikunja kona katika barabara ya kuelekea Mahakama ya Kinondoni kwa ajili ya kumwahisha hospitali na taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa lilielekea katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Akizungumzia hali hiyo, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema kuwa Mbowe yuko salama na anaendelea vizuri.
“Ni uchovu, uchovu, uchovu tu but he is out of danger (hayuko katika hali ya hatari),” Lissu.
Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alisema walimpokea Mbowe saa 11 jioni na alikuwa anaendelea na matibabu katika hospitali hiyo, hata hivyo hakutaka kuweka wazi ugonjwa uliokuwa unamsumbua.
MWANANCHI
Mtoto wa miaka 11 anayesoma Shule ya Msingi Shauri Moyo mkoani Kilimanjaro, anadaiwa kuchomwa na pasi ya umeme sehemu mbalimbali mwilini na dada yake, kisha kufungiwa ndani kwa siku tatu mfululizo.
Mtoto huyo anayesoma darasa la sita alidai kuwa ukatili huo amefanyiwa na dada yake wanayechangia baba.
Alidai kuwa Agosti 6 baada ya kurudi kutoka shule, dada yake alimtuhumu kumuibia Sh30,000 na mafuta ya kupaka.
“Nilimweleza kwamba sihusiki na wizi huo, lakini yeye hakukubali alichukua pasi na kuanza kunichoma nayo kwenye mapaja, mgongoni na kifuani,” alisema mtoto huyo.
Mtoto huyo anadai kuwa, baba yake aliporudi alimweleza kuwa amechomwa moto, lakini cha kushangaza alijibiwa kuwa aache kwenda kwa watu.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Shaurimoyo, Felix Ngowi alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema yeye kama kiongozi wa mtaa amepinga ombi la baba mzazi wa mtoto huyo kutaka suala hilo kumaliza kifamilia.
“Tulipata taarifa na polisi walifika na kuwakamata watuhumiwa na kumpeleka mtoto hospitalini ambako anaendelea vizuri,” alisema.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Fulgens Ngonyani amekiri kupokea taarifa za ukatili huo na kusema tayari linawashikilia watuhumiwa wote wawili na uchunguzi ukikamilika watafikishwa kortini.
JAMBOLEO
Waziri wa Ujenzi na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema kuwa wana-CCM mwaka huu wanapaswa kufanya kampeni za kisayansi zaidi kuhakikisha wanapata ushindi wa tsunami utakaowezesha kuundwa kwa Serikali imara itakayowaletea maendeleo Watanzania wote.
Alisema kwa kufanya hivyo kutawasaidia kupata viti vingi na kusimamia shughuli zote za maendeleo na kwa manufaa ya wanaCCM na Watanzania wote kwani mahitaji yao na matarajio yao ni kupata maendeleo makubwa.
“Niwaombe wana CCM wenzangu, tushikamane tuwe wamoja. Kampeni za mwaka huu ni lazima tufanye kampeni za kisayansi zaidi, ni lazima kampeni zianze katika ngazi ya nyumba kumi, vitongoji kwa vitongoji, vijiji, mitaa, kata majimbo , wilaya, mikoa na baadaye urais kwa ujumla. Katika umoja huu nataka niwahakikishie ushindi wa mwaka huu wala si wa kimbunga, ni wa tsunami,” Dk Magufuli.
Dk Magufuli aliyekuwa katika ziara ya mikoa ya kusini ya kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotelekezwa katika kipindi cha awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, alisema hayo hapo jana wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho nje ya ofisi za CCM mkoa wa Mtwara, ikiwa ni siku moja baada ya rais kukamilisha ziara yake na kuwaaga wananchi wa mkoa huo.
Mgombea huyo na mbunge wa Chato alibainisha kuwa amekuwa kiongozi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kipindi kirefu, hivyo anakifahamu vema chama, shida za wanaCCM na matarajio yao yanayojumuisha matarajio ya Watanzania wote na shida zao.
Alisema kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais, hatawasahau wanaCCM na Wanamtwara kwa ujumla, lakini wote hao wanapaswa kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa kuwa maendeleo hayana chama na akichaguliwa atakuwa rais wa Watanzania wote.
Alisema katika kipindi cha miaka 20 ya uongozi, amekuwa akifika Mtwara na hivyo ana uhakika endapo Wanamtwara wataamua kumpatia nafasi ataujua zaidi mkoa huo kuuendeleza katika kipindi cha miaka mingine zaidi.
“Wanamtwara nafahamu matarajio yenu, nataka niahidi kwenu na nimwombe Mungu nitapenda sana niwe mtumishi wa watu, nisiwe na majivuno wala kujiona, niwe mtumishi hasa wa wanyonge niweze kuwasikiliza na kusikiliza matarajio yao.
“Matarajio ya Watanzania na Wanamtwara ni makubwa, wanahitaji maendeleo makubwa na tunahitaji kuyasukuma. Nchi yetu imelelewa katika misingi ya umoja pasipo kubaguana kutokana na maeneo tunayotoka, dini, makabila hivyo tunahitaji umoja na palipo na umoja pana amani na palipo na amani pana maendeleo,” alisema Dk Magufuli.
HABARILEO
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal amekanusha taarifa za uzushi ziliposambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa anakihama Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katibu wa Makamu wa Rais, Zahor Mohammed Haji kwa niaba ya Dk Bilal, alisema taarifa hizo ni za uongo na uzushi wa aina yake. Zahoro alisema, Dk Bilal yupo nchini Uingereza katika shughuli za ujenzi wa taifa na kwamba hana mpango wa kuondoka CCM na wanaoeneza uzushi huo wana lao jambo.
Katibu huyo amemnukuu Dk Bilal akisema; “Ndugu zangu wa CCM, na Watanzania kwa ujumla, napenda kuchukua fursa hii kuwa taarifu kwamba kuna taarifa inayoenezwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwemo facebook na whatsApp kuwa nitaitisha mkutano na vyombo vya habari ili kujitoa CCM.
“Taarifa hizo ni uzushi na mzipuuze kwani sina mpango na sifikirii kufanya hivyo kwa sababu sina sababu ya kunifanya niondoke CCM.”
Aidha, Dk Bilal alisema yupo imara na mwenye siha njema na kuwa hivi sasa anajiandaa kushiriki kikamilifu kuzunguka majimbo yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kumnadi mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli kwa azma ya kumsaidia Rais Jakaya Kikwete aendelee kufanya kazi za kitaifa ili kukipatia CCM ushindi mnono katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu ili chama hicho kikongwe kliendelee kukamata dola.
Itakumbukwa kuwa mwishoni mwa wiki iliyopita kupitia mitandao ya kijamii ilikuwa ikisambazwa taarifa ya uzushi.
HABARILEO
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kiama kwa watumiaji vibaya na wahalifu wote wa mitandao nchini, kuwa siku zao zinahesabika kwani ifikapo Septemba mosi, mwaka huu, Sheria ya Uhalifu wa Mitandao itaanza kutumika na wengi huenda wakaishia gerezani.
Mamlaka hiyo imebainisha kuwa kwa sasa Tanzania inaongoza kwa kuwa na watumiaji vibaya wengi wa mitandao ya kijamii, jambo linalosababisha taarifa za mitandao mingi kutoaminika hadi nchi za nje kutokana na kujaa uzushi, uongo, uchochezi na lugha na picha za matusi.
Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy alikiri kuwa pamoja na kwamba mamlaka hiyo imefanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya utumiaji sahihi wa mitandao hiyo, bado matumizi yake si mazuri hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na kwa watu maarufu.
“Napenda kuwatahadharisha Watanzania na watumiaji wa mitandao hii kwa ujumla kuwa sheria hii si ya kupuuzwa, kwani kwa hali ilivyo wengi watatozwa faini na watashindwa kulipa na kuishia gerezani,” alisisitiza.
Alisema kutokana na kukithiri kwa matumizi mabaya ya mitandao nchini, kwa sasa nchi nyingi haziamini tena taarifa za mitandao ya kijamii na wala hawazitumii hali inayopaswa kubadilishwa.
“TCRA tumebaini kuwa watu wengi wanatumia mitandao hii lakini hawajui hasa matumizi yake sahihi, tunashauri kabla mtu hajafungua mtandao wake kama vile blogu, ukurasa wa facebook au hata whatsApp lazima wajielimishe kwanza kuwa wanafungua kwa malengo gani, na wataitumiaji kwa manufaa yao na si vinginevyo,” Mungy.
Alisema mamlaka hiyo kazi yake kubwa ni kusimamia matumizi ya mitandao hivyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, itahakikisha inadhibiti kwa kuelimisha na kuwabaini wale wote wanaotumia vibaya mitandao hiyo.
“Kazi yetu sisi si kuwakamata hawa wahalifu, sisi tunasimamia na tuna uwezo wa kuwatambua wale wote wanaotumia vibaya mitandao hii hata kama watabadilisha kadi zao za simu mara 300 na kubadili majina, tuna uwezo wa kuwatambua na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria pale tunapotakiwa kwa mujibu wa taratibu,” alisisitiza.
Alisema tayari wameshaanza kampeni ya kuelimisha matumizi sahihi ya mitandao kupitia vipindi na semina zinazojumuisha kada mbalimbali muhimu kama vile wasanii na vyombo vya habari juu ya kujihadhari na matumizi mabaya ya mitandao.
“Hivi karibuni tulifanya semina ya wasanii ambao ndio waathirika wakubwa wa matumizi haya ya mitandao na kuwaelimisha namna ya kuitumia mitandao hii, pia vyombo vya habari tumevielimisha na kuvisisitiza kutotegemea taarifa za mitandao hasa kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuwa nyingi si sahihi,” alisema bosi huyo wa TCRA.
Tayari Rais Jakaya Kikwete ameshasaini Sheria hiyo ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na inatarajiwa kuanza kufanya kazi rasmi Septemba mosi, mwaka huu. Sheria hiyo katika eneo la adhabu kwa wahalifu wa mtandao pamoja na wasambazaji wa picha za utupu na ngono, wasambazaji wa taarifa za uongo, za kibaguzi na matusi na watu wengine wanaofanya udanganyifu unaohusu kompyuta, adhabu ni kwenda jela hadi miaka 10 au kulipa faini isiyopungua Sh milioni 50.
HABARILEO
Zaidi ya waumini 4,000 wa Kanisa kongwe la Watch Tower lenye umri wa zaidi ya miaka 100, wamenyimwa haki yao ya msingi ya kikatiba ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Waumini wake hawaruhusiwi kupiga kura, kuwa wanasiasa, kusoma zaidi ya darasa la saba na pia hawatakiwi kuwa matajiri. Ni kutokana na makatazo yao, waumini wote wenye umri wa kupiga kura, hawakujiandikisha katika Dafatari la Kudumu la Wapigakura katika mfumo wa BVR kutokana na imani na makatazo ya kanisa hilo.
Kanisa hilo lililopo katika Kitongoji cha Kitika, tarafa ya Kasanga wilayani Kalambo, mkoani Rukwa lina hadhi ya kuwa makao makuu ya Kanisa la Watch Tower duniani.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa licha ya kanisa hilo kuanzishwa miaka 100 iliyopita lakini bado halijasajiliwa rasmi kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kukinzana na imani na makatazo ya kanisa hilo yaliyoanishwa na mwasisi wa kanisa hilo.
Kitongoji cha Kitika, kijijini Kasanga ndipo yalipo makazi ya kudumu ya Baba Mtakatifu au “Papa” wa kanisa hilo maaarufu kama “Vatican City“ likiwa na waumini walionea hadi nchi jirani ya Zambia.
Kadhalika uchunguzi huo umebaini kuwa kanisa hilo lililoanzishwa na Baba Mtakatifu wa Kwanza, Enock Sindani akitoka Marekani alikokuwa anaishi na kufanya kazi, umebaini kuwa kwa sasa limegawanyika, na kusababisha kuwapo Baba Watakatifu watatu, kila mmoja akiwa na waumini wake, lakini wote wakibakiza makao makuu kijijini hapo.
Tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo, karne moja iliyopita limeshakuwa na Baba Watakatifu watano ambao ni pamoja na mwasisi Sindani, Samwel Mwimanzi, John Chamboko, Edwin Simugala na Sikazwe; kwamba hadi sasa hakuna Baba Mtakatifu wa kanisa hilo anayetoka nje ya nchi hii.
Mmoja wa “Papa” wa kanisa hilo, Jonas Simulunga (67) akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni alikiri zaidi ya waumini 4,000 wa kanisa hilo wakiwemo viongozi wa kiroho hawakujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura hivyo wamepoteza sifa ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Alisisitiza siasa kwa waumini na viongozi wa kanisa hilo ni mwiko. Kwa mujibu wao waumini na viongozi wao wanazuiwa kujiunga na chama chochote cha siasa au kushika nyadhifa za kisiasa licha ya kuwa hawatashiriki katika kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu, wanakiri kuwa hawajawahi kupiga kura katika uchaguzi wowote ukiwamo Uchaguzi Mkuu tangu nchi hii ijipatie Uhuru miaka 53 iliyopita.
Hata hivyo, wote wamekiri kuwa waumini na viongozi wao hawakuweza kujitokeza kujiandikisha katika Sensa ya Watu na Makazi Agosti 26, 2012 kwa kuwa wao wanachodai walitaka wahesabiwe tu bila kuulizwa maswali tena yasiwe ya siri kwa kuwa hawako mahakamani.
NIPASHE
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, jana alikiri mahakamani kwamba alishindwa kuhifadhi bastola yake mahali salama, hali iliyosababisha washtakiwa wenzake kukutwa nayo.
Mbali na Gwajima washtakiwa wengine ni Askafu Msaidizi wa kanisa hilo, George Mzava; mfanyabiashara, Yekonia Bihagaze na Mchungaji Georgey Milulu ambao wanakabiliwa na mashitaka ya kukutwa na bastola bila kibali.
Gwajima alikiri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi, Cyprian Mkeha wakati akisomewa maelezo ya awali na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Joseph Maugo katikam Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Pia, alikiri kwamba Machi 23, mwaka huu alilazwa na kuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi, katika hospitali ya TMJ.
Hata hivyo, askofu msaidizi na wenzake walikanusha kufanya jaribio la kumtorosha askofu Gwajima akiwa chini ya ulinzi wa polisi katika hospitali hiyo pamoja na kukutwa na begi lililokuwa na bastola, risasi tatu za bastola na risari 17 za bunduki aina ya Shortgun.
Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri Septemba 10, mwaka huu.
NIPASHE
Vurugu na malalamiko ya uchaguzi wa kura za maoni za udiwani ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata ya Kahangara wilayani Magu mkoa wa Mwanza, vimesababisha matokeo yake kutangaziwa katika kituo cha polisi.
Matukio ya vurugu na malalamiko kama hayo yamekuwa yakitokea katika maeneo mengi nchini baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa ubunge na madiwani.
Baadhi ya wafuasi wa CCM waliokuwa wameandamana kupinga matokeo yaliyompa ushindi, Deus Machibula, diwani aliyemaliza muda wake, walisema hawakubaliana na matokeo hayo kutokana na uchaguzi kutawaliwa na vurugu na rushwa.
Hata hivyo, wana-CCM hao waliokuwa wamebeba mabango mbalimbali yaliyokuwa yameandikwa ujumbe tofauti yakiwamo yaliyosomeka,Tunamtaka Mussa Samson diwani wa kata ya Kahangara kwa maendeleo ya wote
.
Mmoja wa mawakala wa mgombea Samson, Joel Ally, alisema chanzo cha vurugu na matokeo kutangaziwa kituo cha polisi ni viongozi wa CCM kata na wilaya kushindwa kutenda haki kwa wagombea wote kitendo kilichosabisha baadhi ya wananchi na wana CCM waliochoswa na viongozi mzigo, kufanya fujo.
Ally alisema uchaguzi huo uligubikwa na wizi wa wazi wazi na upendeleo pamoja na fomu za kupigia kura kuchakachuliwa, wajumbe kupiga kura mara tatu kinyume cha kanuni na taratibu za uchaguzi wa chama.
“Mawakala wa Samson hatufahamu namna Machibula alivyoibuka mshindi, hatuelewi kabisa na hatukubaliani na matokeo hayo yaliyotangaziwa kituo cha polisi na mawakala hatukupewa taarifa,” Ally.
Katibu wa CCM kata ya Kahangara, Cravery Makologoto, alithibitisha kuwapo kwa vurugu hizo na matokeo hayo kutangazwa polisi ni kutokana na wafuasi wa Samson kusababisha vurugu.
Hata hivyo, licha ya kudaiwa kuongoza katika uchaguzi huo wa kura za maoni, lakini Machibula hajatangazwa licha ya kudai kuaminiwa na wana-CCM kuwaletea maendeleo katika kata hiyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa hakupatikana kuzungumzia taarifa hizo kutokana na simu yake kutokuwa hewani hadi tunakwenda mitamboni.
NIPASHE
Mkuu wa Interpol nchini, SACP Gustavus Babile, amesema Jeshi la Polisi bado linachunguza tukio la kukamatwa kwa nyara za serikali kilo 262 za pembe za ndovu na kilo moja ya kucha na meno ya simba, zilizokuwa zinasafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Beijing, China kupitia uwanja wa ndege wa Kimataifa Zurich, Uswisi.
SACP Babile aliiambia Nipashe jana kuwa baada ya kufanya mawasiliano na Mamlaka ya Forodha ya Uswisi, imewathibitishia kuwa nyara hizo zinatoka Tanzania.
“Bado tunaendelea na uchunguzi,” alisema Babile na kuongeza kuwa hakuna mtu anayeshikiliwa kwa kuhusishwa na tukio hilo.
Tukio la kukamatwa kwa nyara hizo liliripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa wiki iliyopita.
Pembe hizo zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani 412,000 (Sh. milioni 873.4) zilikamatwa Julai 6, mwaka huu zikisafirishwa na raia watatu wa China, waliokuwa wanasafiri kutoka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwenda Beijing, China kupitia Zurich.
Mkuu wa Idara ya Forodha kwenye viwanja vya ndege nchini Uswisi, Heinz Widmer, alikaririwa akieleza kuwa inakadiriwa meno hayo yanatokana na kuuawa kwa tembo 40 hadi 50.
Meno hayo ya tembo yaligundulika yakiwa yamekatwa katwa vipande 172 na kuhifadhiwa kwenye mabegi nane yaliyokuwa yamebebwa na raia hao wa China pamoja na meno 21 ya simba na kucha 35 za simba ambazo bado thamani yake haijajulikana.
Baada ya ripoti hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akieleza kuwa Wizara yake inafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na vyombo vya ulinzi na usalama.
Takwimu zinaonyesha kuwa majangili huua tembo 35,000 kila mwaka nchini.
PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos