Magazeti

Rose MUHANDO matatani, Mama aua mtoto kwa sumu, UKAWA wamwonya JK, Kipindupindu..#StoriKubwa

on

GENERAL

MTANZANIA

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wamemuonya Rais Jakaya Kikwete, wakisema ndiye mwenye dhamana ya kulinda usalama wa wananchi na akiendelea kutumia vibaya vyombo vya dola, Novemba mwaka huu watamburuza Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague, Uholanzi.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Zanzibar na viongozi wa Ukawa, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Kibanda Maiti wenye lengo la kutafuta wadhamini kwa mgombea urais wa umoja huo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa.

Akizungumza katika mkutano huo jana mjini hapa Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalimu Seif Sharif Hamad, alisema CCM wanahubiri amani wakiwa majukwaani lakini wakishuka wao ndio wa kwanza kuivunja.

“Kama kuna watu wana nidhamu ni watu wa Ukawa, Mbeya, Arusha, watu wawalikuwa wanasubiri kwa amani, polisi wanapiga mabomu, wao ndiyo wanaleta tensheni katika nchi, X

3 wafuasi wa Ukawa.

“Namwambia Kikwete (Rais), atimize wajibu wake, akifanya vinginevyo watakwenda ICC, Kikwete ondoka kwenye nchi ikiwa salama kama ulivyokabidhiwa ikiwa salama, wananchi wakukumbuke kuwa umeiacha salama,” alisema Maalim Seif ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar kupitia umoja huo.

Akihutubia katika mkutano huo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amewataka wanasheria wa Ukawa, kuanza kuandika matukio yote yanayotokea nchini kwa sasa ili wayawasilishe katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu (ICC).

Alisema Watanzania kwa sasa wanataka mabadiliko kwa asilimia 99, na jeshi la polisi likiendelea kuvunja amani, Novemba mwaka huu watakwenda ICC.

Naye Mgombea Mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji, alisema ni bahati mbaya sana watawala wanadhani kutumia mabavu kutawasaidia kubaki madarakani  jambo  ambalo kwa sasa haliwezi kutokea.

Kwa upande wake Lowassa alisema kitendo cha CCM kumvua wadhifa wake Kamanda wa UVCCM, Kingunge Ngombale Mwiru kwa sababu tu mwanasiasa huyo mkongwe alitumia demokrasia kueleza hisia zake ni kuchuma laana.

Alisema Kingunge ambaye ni mmoja wa waasisi wa TANU na CCM, alikuwa amebaki kama mfano ndani ya chama hicho kutokana na historia yake.

MTANZANIA

Wananachi  na wagombea udiwani wa Chama  Cha  Demokrasia  na Maendeleo (CHADEMA)  katika  Kata nane  za Manispaa  ya Morogoro  wamevamia ofisi za  chama hicho wakitaka  ufafanuzi wa majina ya wagombea wa udiwani waliokatwa  wakiwa wameshinda katika  kura za maoni.

Ghasia  hizo  zilizuka  saa  9.00 mchana   baada  ya makundi  ya  wagombea  kutoka  katika  Kata  za Kionda, Kichangani, Kilakala, Lukobe, Mlimani, Boma, Mjimpya na Kiwanja  cha Ndege  kuvamia  ofisi  hiyo kupata ufafanuzi wa  sababu za majina  yao  kukatwa  wakati wakiwa wameshinda  katika  kura za maoni.

Wanachama  walivamia  gari  la mwenyekiti wa  Chadema  wa wilaya  na kumzuia  asiondoke  hadi atakapotoa  ufafanuzi  wa madai hayo.

Mmoja  wa  wagombea   aliyekatwa  jina  lake  huku akiwa  ameongoza  katika mchakato wa  kura  za maoni, Mwanahenzi Shaha  alisema  ameshangazwa  na  hatua hiyo.

“Mimi  katika  Kata ya Mlimani  nimeshinda  kura za maoni lakini nashangaa leo naambiwa  jina langu hakuna na tayari ameteuliwa mtu mwingine hii ni rushwa,” alisema  huyo  kwa  hasira.

Mmmoja  wa  wanachama aliyekuwapo  katika  msafara huo  aliyejitambulisha  kwa  jina  la Fiderik Boniface,  alidai    kitendo  cha viongozi wa  wilaya  na mkoa  kukata baadhi ya   wagombea  kitaleta madhara  makubwa katika  chama.

Juhudi za kuwapata viongozi wa Chadema ngazi ya wilaya na mkoa  hazikuzaa matunda baada ya simu zao kutokuwa hewani   jana.

MTANZANIA

Licha ya Chama Cha Mpinduzi (CCM) kuamuru kurudiwa  uchaguzi katika baadhi ya majimbo yakiwamo  yaliyokuwa yanaongozwa na mawaziri wa Rais Jakaya Kikwete, hatimaye chama hicho kimewatosa rasmi.

Kutoswa kwa mawaziri hao kunatokana na kushindwa kwao kwenye kura za maoni za marudio ambako pia wana CCM wamebwaga katika mchakato huo na kusubiri hatima ya Kamati Kuu ya chama hicho.

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema baada ya kurudiwa  uchaguzi katika majimbo kadhaa hatimaye Kamati Kuu imefanya uteuzi wa mwisho huku ikiwaweka kando mawaziri hao.

Alisema   kikao kilichofanyika jana chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kimefanya uteuzi huo kutokana na matokeo ya kura za maoni.

Katika matokeo hayo ya kura za maoni, mawaziri  waliojikuta wakiangukia pua ni pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus Kamani   na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith Mahenge.

Nape alisema katika kikao hicho cha CC pamoja na mambo mengine, kilikuwa na ajenda ya kupitisha majina ya wagombea katika majimbo yaliyorudia uchaguzi pamoja na Uchaguzi Mkuu

“Tumepitisha majina ya wagombea katika majimbo tisa  tuweze kusimamisha wagombea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu,” alisema Nape.

Aliwataja wagombea waliopitishwa katika majimbo hayo kuwa ni   aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry (UKONGA),  Edward Mwalongo (Njombe Kusini) na Venance Mwamoto (Kilolo).

Wengine ni Profesa Norman Sigala (Makete), Dk. Raphael Chegeni (Busega), Edwin Ngonyani (Namtumbo),  Martin Msuha (Chilonwa),  Joel Makanyanga (Mbinga Vijijini)   na Mohamed Mchengerwa (Rufiji).

Akizungumzia wanachama wa chama hicho wanaoendelea kulalamikia matokeo ya kura za maoni, Nape alisema wagombea hao walipaswa kuandika barua ya malalamiko yao kwa kamati kuu iweze kupitiwa na kutolewa uamuzi.

“Hakuna malalamiko yaliyowasilishwa kwenye kamati hii ambayo hayajafanyiwa kazi jambo ambalo lilisaidia baadhi ya majimbo kurudiwa   uchaguzi, hivyo basi wanachama wao wanapaswa kuacha malalamiko nje ya vikao.

“Kama wanaona chama hakijawatendea haki na kwamba CCM haiwezi kuwaletea maendeleo wanaweza kufanya uamuzi mgumu wa kujiunga na vyama vya upinzani ambako wanaamini wanaweza kutendewa haki.

NIPASHE

Aliyewahi Mbunge wa Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo (pichani), ambaye aligombea Jimbo la Mbinga Vijijini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kura za maoni, anadaiwa kudai arudishiwe vifa vyake alivyokipatia Chama kwa ajili ya kampeni.

Kayombo alikwenda ofisi za CCM wilayani humo Agosti 14 na kutaka arudishiwe vifaa vya matangazo, baada ya kushindwa kwenye kura za maoni Agosti Mosi 2, mwaka huu.

Mmoja wa makada alisema Kayombo alichukua hatua hiyo akisema viongozi wa Chama wilaya hawamtaki.

Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wamesikitishwa na kitendo hicho.

“Tunajua kitendo cha kutunyang’anya vipaza sauti ni hasira baada ya kushindwa, kwenye uchaguzi wa kura za maoni,” alisema Chinowa.

Alipotafutwa Kayombo, alisema kuwa madai hayo siyo ya kweli na kueleza kuwa Chama kimekuwa kikiviazima vifaa vyake mara kwa mara kwa kuwa yeye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).

“Siku za kwanza za kampeni hawakuvitumia vipaza sauti vyangu, walisema  vimeharibika. Baadaye walinunua vipya na wakavipeleka majimbo ya Mbinga Mjini na Vijijini,” alisema Kayombo na kuongeza:

“Majuzi nilikwenda nikakuta havijatunzwa vizuri , nikawaambia wanirudishie vifaa vyangu.”

Kadhalika, Kayombo alisema hakushindwa kura za maoni kwa kuwa matokeo ya kata mbili hayajajumuishwa.

Katibu wa CCM wa mkoa wa Ruvuma, Vellena Shumbusho, alisema amelazimika Chinowa kumkabidhi haraka Kayombo vifaa vyake anavyodai.

Alisema Kayombo alikuwa amevinunua na kuvikabidhi kwenye Chama kwa ajili ya kusaidia matangazo wakati wa kampeni za kura za maoni  Jimbo la Mbinga Vijijini lilikuwa na wagombea ubunge nane waliochuana katika kura za maoni.

Martin Msuha aliyeongoza kwa kura 13,354, Kayombo (12,068), Deodatus Ndunguru (7,060), Humprey Kisika (545) na Dk. Silverius Komba (3,941).

HABARILEO

Mkazi wa Chuo, tarafa ya Shimbi Kwandele wilayani Rombo, Kilimanjaro, Fidensia Salvatory (27) anashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumuua kwa kumnywesha sumu mwanawe wa miezi sita kwa madai ya kukerwa na wakwe zake.

Mwanamke huyo anadaiwa kumnywesha sumu ya panya mwanawe huyo kama sehemu ya kupunguza hasira zake baada ya kukerwa na manyanyaso kutoka ukweni anakoishi na mumewe.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema tukio hilo limetokea Agosti 15 mwaka huu majira ya saa 8.30 mchana nyumbani kwa wazazi wa mtoto huyo.

Akielezea tukio hilo Kamanda Ngonyani alisema siku ya tukio baba mzazi wa mtoto huyo, Salvatory Baltazary alifika nyumbani kwake majira ya mchana na kukuta mwanawe akiwa amelala kitandani akiwa anatokwa na povu mdomoni na puani hali iliyoashiria kupata madhara.

Alisema baada ya kuona hali hiyo alitoa taarifa Polisi ambao walifika nyumbani hapo na kumpeleka mtoto hospitali huku wakiokota baadhi ya vitu vilivyokuwa vimehifadhi sumu hiyo.

Kamanda Ngonyani alisema askari hao walikuta pakiti iliyokuwa na unga unaodhaniwa sumu ya panya iliyotumika kumuua mtoto huyo.

Alisema Polisi ilimkamata mtuhumiwa na baada ya mahojiano alikiri kumpa sumu mtoto wake kwa madai ya kuchoshwa na manyanyaso kutoka kwa wakwe zake.

HABARILEO

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa kitashinda Uchaguzi Mkuu mwaka huu kwa sababu kina mtandao mkubwa wa wanachama kuanzia ngazi ya chini na kwamba kufurika kwa wananchi katika mikutano ya Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa sio ushindi, kikisema kura ni mahesabu.

Aidha, kimesema kuwa mgombea huyo wa Chadema na umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), amedanganywa na wapambe wake kuihama CCM na kumkejeli ikisema gari la wagonjwa linapaswa kuwekwa nyumbani kwake siku ya uchaguzi kwani CCM itapata ushindi wa uhakika asubuhi.

Akitoa taarifa kuhusu kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisisitiza kuwa ushindi wa chama hicho tawala na kikongwe hauna shaka kutokana na mtandao wake kuanzia ngazi ya chini.

Akijibu swali kuhusu kufurika kwa wananchi katika mikutano ya mgombea huyo wa Chadema, Nape alisema: “Kwa walioanza siasa jana ndio watashituka. Mwaka 2010 Slaa (Dk Willibrod) katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni Mbeya alipata watu wengi kuliko wale aliopata Edward. Lakini kura alizopata Mbeya utashangaa.

“Kupata watu wengi mkutanoni hakutushangazi kwani kura ni mahesabu, hawa (Chadema na mgombea wao) wanatoka pointi moja kwenda nyingine. CCM ina mtandao, ukiondoka mjumbe wa nyumba kumi anapitia watu wake anasafisha nyayo zenu,” alisema kiongozi huyo.

Nape aliongeza kuwa wapinzani wote wametoka ndani ya CCM kuanzia kwa Augustino Mrema mwaka 1995 na hadi katika chaguzi nyingine zilizofuta na zote wapinzani walishindwa, na hata safari hii CCM itashinda.

Akimgeukia Lowassa, Nape alisema Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu kwa kashfa ya zabuni ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, amedanganywa na wapambe wake na kuondoka chama tawala, na kwamba licha ya kuhamia huko, CCM itamshinda asubuhi na kuwataka wanaotishia kukihama kufanya hivyo na si kuleta shinikizo.

“Katika mchakato wa uchaguzi si wote watakaoridhika na matokeo kwa sababu kuna wengi wanajiandaa kushinda na sio kushindwa, na matokeo yanapokuwa hivyo, wanakuwa hawaridhiki na hapo ndipo wanazungumzia kwenda upande wa pili, na hasa kwa shinikizo la wapambe.

“Hili limetokea kwa Edward, amekwenda upande wa pili, amedanganywa na watu, tutampiga. Ushindi wa CCM ni wa uhakika, sio wa matumaini. Matumaini yapo Angaza, CCM ni ya uhakika. Tutashinda asubuhi. Tumesema ni mpambano kati ya wagombea na makapi,” alisema Nape na kuongeza: “Zipo mechi ambazo unajua hii utashinda. Yanga na Lipuli ya Iringa unajua matokeo yake.

Tunataka mgombea mwenzetu apelekewe ambulance (gari la wagonjwa) nyumbani kwake, kwani ushindi kwetu ni uhakika.” Kuhusu wanaolalamika na kutishia kuhama, alisema malalamiko hayawezi kutolewa barabarani kwani chama hicho kina utaratibu wake na yale yote yaliyolalamikiwa yakiwamo ya udiwani, yamefanyiwa kazi. “Tulisema wakati ule wa mchakato wa kutafuta mgombea wa urais kuwa hatutafanya kazi kwa shinikizo.

HABARILEO

Mwimbaji maarufu hapa nchini wa nyimbo za Injili, Rose Muhando anatafutwa na waandaaji wa tamasha la Injili wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa madai ya kutoonekana kutumbuiza kama jinsi walivyokubaliana.

 Zephania Simoni ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Uratibu alisema wameingia hasara ya Sh milioni 4.3 kutokana na tamasha hilo kuvurugika baada ya kutapeliwa na Muhando.

Alifafanua kuwa tayari walikuwa wameishamkabidhi kiasi cha Sh 1,700,000 muimbaji huyo na ameshindwa kufika na hivyo kuonesha wazi kuwa amewatapeli.

Alisema wameamua kuripoti tukio hilo kituo cha Polisi cha wilayani humo na kupewa RB namba ORK/RB 395/2015 kwa Rose na kuanza kumsaka popote alipo ili kukabiliana na kesi hiyo wilayani Simanjiro.

Wameshangazwa kwa mtumishi huyo wa Mungu kujiingiza katika masuala ya kutapeli na ndio maana wameamua kuchukua hatua za kisheria.

Awali, alisema siku ya tamasha wakati wakiwa wanamsubiri siku moja kabla ya tamasha alisema yupo njiani anakuja majira ya mchana mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Lucas alitupigia simu na kutuambia Rose hatakuja yupo kwa mgombea Urais anasaini mikataba ya kumnusuru katika kusaidia kampeni, “ alisema Simon.

Akafafanua kuwa baada ya kupata taarifa hiyo na kuingia shaka walianza kumtafuta Muhando bila mafanikio kupitia simu yake ya kiganjani siku nzima hadi anatoa taarifa hii hawajawahi kuwasiliana naye.

Hata hivyo, Muhando alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi ili kuthibitisha madai hayo simu yake iliita na wakati mwingine ilikuwa ‘busy’ na baadaye kwa mara ya nne ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mdogo wake, lakini hakutaka kujitambulisha na alipoulizwa juu ya madai haya alisema Rose ni dada yake hivyo akija atamwambia apige simu.

Hivi karibuni mwanamuziki huyo alikuwa akidaiwa Sh 6,000,000 na alilipiwa na promota mashuhuri wa nyimbo za Injili Alex Msama ambaye mara nyingi wamekuwa wakifanyakazi pamoja.

MAJIRA

Ugonjwa wa kipindupindu umeripotiwa katika Jiji la Dar es Salaam na watu wawili wamethibitika kufa. Wengine zaidi ya 30 wamelazwa katika hospitali za Mwananyamala na Sinza zilizopo Manispaa ya Kinondoni.

Kutokana na tishio la ugonjwa huo, shughuli za kampeni za kisiasa za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu wa Rais, wabunge na madiwani, zilizo kuwa zianze mwishoni mwa wiki hii, zimesogezwa mbele. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alithibitisha hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya ugonjwa huo kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC 1).

Alisema watu hao wawili waliofariki, mmoja ni mwanamume na mwingine ni mwanamke na wanatoka Manispaa ya Kinondoni. Mkuu huyo wa Mkoa alisema ugonjwa huo umethibitika baada ya vipimo vya maabara vya watu hao, kuthibitisha.

“Watu wawili akiwemo mwanamume na mwanamke wamefariki dunia baada ya vipimo vya maabara kuthibitisha ugonjwa huo. Hata hivyo, hakuna taarifa zozote za ugonjwa huo katika manispaa za Temeke na Ilala,” alisema Sadiki.

Alisema endapo hali hiyo itaendelea kuwa mbaya, itabidi mamlaka za Dar es Salaam kusogeza mbele kampeni za kisiasa, zinazotarajiwa kuanza mwisho mwa wiki hii ili kuepusha mikusanyiko ya watu.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty, alisema wagonjwa wengine 30 wapo chini ya uangalizi maalumu katika hospitali za Mwanayamala na Sinza, ambapo 19 wapo Sinza na 11 Hospitali ya Mwananyamala. Wengine wanne wameruhusiwa na kurudi nyumbani.

“Sampuli za wagonjwa sita zilizochukuliwa, wanne kati yao wamethibitika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo,” Natty.

Alisema wamepata dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo. Jitihada mbalimbali zinaendea kuchukuliwa ikiwemo kupulizia dawa kwenye madimbwi ya maji.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Dk Jackson Makanjo, aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kuchukua tahadhari, ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni kabla ya kula, na unapotoka chooni. Alitoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam, kuhakikisha wanachemsha maji ya kunywa na kuepuka kula ovyo vyakula vya mitaani.

Alisema ugonjwa huo ulianzia eneo la Kwa Ali Maua huko Kijitonyama na kisha kuenea maeneo ya jirani ya Tandale, Manzese na Mwananyamala.

MWANANCHI

Sintofahamu imetanda ndani ya Chama cha ACT – Wazalendo juu ya hatima ya mgombea wa urais baada ya mgombea aliyependekezwa na kuchukuliwa fomu ya kuomba uteuzi, Profesa Kitila Mkumbo kuikataa nafasi hiyo.

Mapema jana saa 4.30 asubuhi, Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba alitinga katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu bila ya kuwa na Profesa Kitila na kueleza kuwa mgombea wao huyo yupo safarini.

Mwigamba alisema alikwenda kuchukua fomu hiyo kwa niaba ya chama na bila kusindikizwa na viongozi wengine kwa kuwa walikuwa kwenye vikao vya ndani vilivyokuwa vikiendelea.

Muda mfupi baada ya Mwigamba kuchukua fomu hizo, Profesa Mkumbo aliandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa anawashukuru makada na Kamati Kuu ya chama hicho kumwamini na kumtaka agombee urais lakini kwa sasa hayupo tayari.

Katika ujumbe huo ambao baadaye alikiri kuuandika, Profesa Mkumbo alisema Kamati Kuu ilituma ujumbe maalumu nyumbani kwake juzi kuzungumza na familia na jamaa zake juu ya ombi hilo na kubainisha kuwa amekuwa akitafakari uwezekano wa kugombea nafasi hiyo baada ya juhudi za kutafuta mgombea kushindikana.

“Nimefanya mawasiliano mapana katika familia, ndani ya chama, chuoni ninapofanyia kazi, kanisani kwangu na kwa watu na taasisi mbalimbali ninazohusiana nazo.

“Baada ya tafakari na mawasiliano mapana, nasikitika kusema kwamba sina utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia na kisiasa kuniwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huu,” alisema Profesa Mkumbo.

Alisema anajua bayana amewaangusha lakini anaamini kwamba wafuasi hao wataheshimu uamuzi wake, hivyo hawataacha kuthamini mchango alioutoa katika chama hicho kwa sababu amekataa kugombea urais.

Alishauri chama kiwaombe wanachama wengine waandamizi kuchukua jukumu hilo, akiwamo Mwenyekiti, Anna Mghwira, huku akiwataka makada wa ACT –Wazalendo kutomtuhumu kwa lolote juu ya uamuzi wake.

Kukataa kwa Profesa Mkumbo kunakipa kazi chama hicho kutafuta mbadala wa mgombea huyo ambaye ni moja ya waasisi wa chama hicho chenye makao yake makuu, Kijitonyama jijini hapa.

Baada ya taarifa ya Profesa Mkumbo kukataa kuzagaa, makada zaidi ya 200 wa ACT – Wazalendo walitinga katika ofisi cha chama hicho wakiwa katika maandamano wakishinikiza agombee.

Maandamano hayo yalianzia jirani na Ofisi ya Tume ya Sayansi na Teknolojia Kijitonyama, wilayani Kinondoni hadi katika ofisi za chama hicho zilizopo umbali wa kilomita moja.

Waandamanaji hao wakiwa na bendera za chama hicho walifika katika ofisi za chama hicho saa 6.10 mchana na kutishia kuvunja mlango wa ofisi lakini walizuiwa na wenzao waliokuwa ofisini.

PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos

Tupia Comments