Mix

Dar marufuku kushikana mikono, Ester Bulaya azua utata na Mgombea CCM ajeruhiwa kwa risasi…#StoriKubwa

on

THEE

MWANANCHI

Mgombea Udiwani wa Chama cha Mapinduzi kata ya Sangabuye Mwanza, James Katole amejeruhiwa na risasi na watu wasiofahamika.

Mgomgea huyo alipigwa risasi juzi akiwa kijijini kwake Nyangoka, Busega ambapo alikwenda kuwasalimia wazazi wake.

Katole alisema alikua nje ya nyumba yao majira ya saa 1 usiku akiwa na wazazi wake gafla walikuja watu ambao hawafahamu na alipowahoji ni kina nani hawakuzungumza lolote zaidi kukaa kimya.

‘Walikuwa wamevaa makoti meusi, nilipowauliza shida yao hawakusema loloyte nikaamua kuwafuata ndipo walipofyatua risasi ambayo ilinipata kwenye kidole na kumpiga mama yangu ubavuni na kutokea upande wa pili’ Katole.

Alisema watu hao ambao hawakuchukua kitu chochote baada ya tukio hilo waliondoka huku wakitembea kawadia na kutokomea gizani.

NIPASHE

Licha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuahidi mchakato wa uhakiki wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Mkoa wa Dar es Salaam kuanza jana, mchakato huo bado ni kizungumkuti kutokana na tume hiyo kushindwa kutuma majina ya waliojiandikisha katika daftari hilo katika kata husika.

Kwa mara ya kwanza Nec iliahidi kubandika majina hayo kuanzia Agosti 13 lakini haikufanya hivyo na kuahirisha hadi Agosti 18 na baadaye Agosti 19, mwaka huu, lakini tarehe zote hizo mchakato huo haukuwezekana kufanyika.

Nipashe ilitembelea ofisi zote za kata zilizotangazwa kubandikwa majina hayo na kukuta hakuna kinachoendelea huku wasaidizi wa watendaji wa kata hizo wakionekana kuendelea na shughuli zao za kawaida.

Aidha, baadhi ya maofisa hao katika Kata ya Ilala walisema watendaji wako katika kikao kilichoitishwa na Meya wa Manispaa hiyo bila kufafanua kikao hicho kilihusu nini.

Mmoja wa Maofisa Uhusiano wa Manispaa ya Temeke ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema Mkurugenzi wa Manispaa hiyo hakuwapo ofisini lakini Nec imetoa agizo la kusitisha mchakato wa uhakiki hadi itakapotangaza tena.

Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima, alisema kwa  Dar es Salaama bado tume iko katika mchakato wa kuchakata taarifa za waliojiandikisha katika daftari na mara baada ya kukamilika kwa uchakataji huo majina yote yatasambazwa kata husika.

Imeandikwa na Esther Mbussi (TUDARCo), Tabia Chilumba na Hussein Ndubikile

NIPASHE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya, amezindua kitabu chake kinachoitwa Daraja Juu ya Mto Nile, huku akiwataka wanaogombea nafasi mbalimbali za kisiasa kukisoma ili kufahamu tulikotoka na tuendako.

Baadhi ya mambo yaliyomo ndani ya kitabu hicho ni kuhusu historia ya Mto Nile, uhandisi na ujenzi wa mto huo, mikataba yake karne ya ishirini, falsafa ya Nyerere kuhusu nchi mpya kurithishwa mikataba, mifarakano na ushirikiano kuhusu maji ya Mto Nile na Sudan Kusini Taifa jipya katika bonde la Mto Nile.

Uzinduzi wa kitabu hicho chenye kurasa 443, ulifanywa na Waziri Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, jana jijini Dar es Salaam.

Prof. Mwandosya alisema anaamini kuwa moja ya sababu kwanini Mwafrika hajaendelea ni kutokana na kutojenga utamaduni wa kuandika historia yake na kwamba hata himaya zote zilizoendelea kulikuwa na uhusiano wa kuandika.

NIPASHE

Marais wastaafu, Ali  Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, wanatarajiwa kushiriki kwenye ufunguzi wa kampeni za kumnadi mgombea wa urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli Jumapili, jijini Dar es Salaam.

Pia uzinduzi huo unatarajiwa kupambwa na wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya wakiongozwa na Nasiib Abdul (Diamond) na bendi mbalimbali ikiwamo ya Tanzania One Theatre (TOT).

Kadhalika, wamo marais wastaafu wa Zanzibar, mawaziri wakuu wastaafu, viongozi wakuu wastaafu wa CCM na viongozi wa serikali, makada kutoka mikoa mbalimbali nchini na wananchi wanatarajiwa kuhudhuria.

Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu ndani ya CCM zinaeleza kuwa baada ya kampeni hizo kuzinduliwa jijini Dar es Salaam, ziara ya kumnadi itaelekea mikoa ya kusini.

Mikoa hiyo ni Lindi, Mtwara na Ruvuma na kwamba ratiba hiyo itafuata hadi kumalizika nchi nzima.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye , alipoulizwa, alisema ratiba kamili itatolewa baadaye kwa vyombo vya habari.

Kuhusu wageni mbalimbali wa heshima ambao wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo alisema hafahamu na kwamba mgeni rasmi ni mgombea mwenyewe ni Dk. John Magufuli.

Nape akizungumzia ilani ya uchaguzi ya chama hicho, alisema inatarajiwa kuzinduliwa siku ya kuzindua kampeni.

Nipashe jana ilishuhudia uwanja wa Jangwani ukifanyiwa usafi.

Magari ya ya kubeba mizigo yalionekana yakisomba taka na udogo uliokuwa ukichimbwa eneo hilo.

MTANZANIA

Siku chache baada ya mgombea ubunge wa Jimbo la Bunda Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Esther Bulaya kuteuliwa na chama hicho na kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo, hali ndani ya chama hicho wilayani  Bunda imekuwa tete.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa aliyekuwa mpinzani wa Bulaya katika kura za maoni ndani ya chama hicho, Pius Masururi, kujitoa katika chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tayari Masururi ametangaza kumuunga mkono Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira katika mbio za ubunge huku viongozi 11 wa Chadema katika jimbo hilo wakisimamishwa uongozi.

Inaelezwa kuwa sababu ya kusimamishwa kwa viongozi hao kunatokana na kile kilichodaiwa kuwa kusimamisha wagombea mamluki katika nafasi ya ubunge na udiwani.

Akizungumza jana mjini hapa kupitia Redio ya Kijamii ya Mazingira FM,  Masururi alitangaza kujiunga na CCM jana muda mfupi kabla ya kuondoka na kurejea jijini Nairobi nchini Kenya.

Alisema Kamati Kuu haikutenda haki kwa kumteua  Esther Bulaya na kumwacha yeye ameshinda katika kura za maoni licha ya kushiriki kwake kukijenga chama hicho kwa kipindi cha miaka minne.

Kutokana na hali hiyo, Katibu wa Chadema Wilaya ya Bunda, Rita Ikandire kwa niaba ya viongozi wanzake wanaotuhumiwa kukihujumu chama hicho wametangaza kujiuzulu nafasi zao za uongozi huku wakidai ofisi ya katibu wa Mkoa wa Mara na Taifa wamevunja katiba ya chama hicho.

“Mimi pamoja na viongozi wa jimbo na kamati  ya utendaji Jimbo la Bunda tumejiuzulu baada ya kutoridhika na  uamuzi wa Kamati Kuu lakini pia baadhi ya makatibu na wenyeviti katika  kata 20 za jimbo hili wamejiuzulu na watabaki kuwa wanachama wa kawaida wa Chadema,Rita.

Waliotangaza kujiuzulu mbele ya waandishi wa habari ni pamoja na Alfred Imanani (Mwenyekiti wa Jimbo), Emmnuel Malibwa(Katibu Mwenezi),  Dickson Kujerwa(Mwenyekiti BAVICHA), David Abogast (Mjumbe Kamati  ya Utendaji), Mwenge Webiro (Katibu BAWACHA jimbo) na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa,  Juma Omari.

Wengine ni Ng’wena Mwita (Mwenyekiti Baraza la Wazee jimbo), Damas Kunju, Kibago Kibago(Red Brigedia Mkuu) ambao wote wamedai kujiuzulu na kubaki wanachama wa kawaida.

Wakati viongozi hao wakidai kujiuzulu, mmoja wa kiongozi wa Chadema, Kaunya Yohana, alisema viongozi 11 tu ndio wamesimishwa uongozi na chama baada ya kupandikiza wagombea wasiokuwa na sifa.

“Viongozi hao hawakujiuzulu kama wanavyodai isipokuwa wamesimamishwa uongozi mpaka mambo yatakapokuwa sawa tangu tarehe 15/8/2015,” Yohana.

Alisema viongozi hao wamesimamishwa kwa barua yenye kumb. Na.C/HQ/ADM/KK/08 ya tarehe 19/08/2015 iliyosainiwa na Julius Mwita Katibu wa Vijana Taifa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Chadema Taifa.

Alisema wakati viongozi hao wakitumikia adhabu hiyo chama kimeunda nguvu kazi itakayosimamia shughuli zote za chama na kuratibu mchakato mzima wa uchaguzi katika majimbo matatu ya Bunda Vijijini, Bunda Mjini na Mwibara.

MTANZANIA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, amepiga marufuku uuzwaji wa vyakula na matunda katika maeneo yasiyo rasmi pamoja na kushikana mikono.

Agizo hilo limelenga kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu unaoendelea kusambaa katika jiji la Dar es Salaam, ambapo hadi sasa watu watatu wameripotiwa kupoteza maisha.

Sadick alitoa amri hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema wagonjwa wa kipindupindu wamefikia 56.

“Wagonjwa wameendelea kupokelewa na hadi jana walikuwa wamefikia 56 wakitokea maeneo ya Makumbusho, Kijitonyama, Kimara, Saranga, Manzese, Kigogo, Tandale na Mwananyamala, maeneo yote yakiwa Manispaa ya Kinondoni.

“Wagonjwa 36 kati yao wamelazwa katika kambi maalum tulizotenga,17 wametibiwa na kuruhusiwa na watatu wamefariki hadi sasa,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo ni lazima jamii na serikali kwa ujumla ikachukua hadhari vinginevyo hali itazidi kuwa mbaya.

Alisema, ili kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, serikali mkoani humo imepiga marufuku uuzwaji wa vyakula mitaani pamoja na mikusanyiko katika misiba ya watu wanaopoteza maisha kwa ugonjwa huo.

Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwenye vituo vya afya vilivyokaribu nao iwapo watagundua mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.

Alitaja dalili zake kuwa ni pamoja na kutapika, kuharisha mfululizo choo cha majimaji meupe, ngozi kusinyaa, kiu kali, midomo kukauka, mapigo ya moyo kwenda mbio, kuumwa na misuli na mwili kukosa nguvu.

“Imefika wakati wananchi wanatakiwa kubadilika na kujua kwamba, suala la usafi ni la kila mtu.

“Tusisubiri  serikali ije itufayie tuone kuwa uchafu ni adui yetu, tuwe wa kwanza kusafisha mazingira yetu ili tuwe salama,” alisema.

Wakati Sadiki akieleza hayo, uchafu kwenye maeneo mbalimbali ya jiji umekithiri, huku pia vyakula vikipikwa na kuuzwa kwenye maeneo yasiyo salama.

Kwenye eneo la Buguruni Maruzuku Kata ya Mnyamani Wilaya ya Ilala, hali ya mazingira si nzuri kutokana na mitaro kujaa uchafu na kusababisha  maji taka kutuwama.

Fatuma Nasoro ambaye ni mfanyabiashara wa chakula na mjumbe wa nyumba 10 kwenye eneo hilo, alisema magari makubwa yamekuwa yakichangia kuharibu mitaro hali ambayo inachangia kutuwama kwa maji taka katika maeneo ya nyumba zao ambazo zimezungukwa na mitaro hiyo.

 

HABARILEO

Rais Jakaya Kikwete amesema tangu achukue kijiti cha uongozi mwaka 2005 hadi leo, utawala wake umefanya mambo mengi makubwa ya maendeleo. Amesisitiza kuwa watu wanaobeza maendeleo hayo, waendelee kusema kwa kujifurahisha, ila wakumbuke kuwa na mipaka ya kauli zao, kwani haki ya maoni au mawazo ni lazima iende sambamba na wajibu.

Alibainisha hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, waliomwalika kuzungumza nao, ikiwa pia ni sehemu ya kumuaga akielekea kumaliza muda wake wa utawala unaotarajiwa kufikia ukingoni baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

“Tena tumewaacha watu wanatumia haki yao ya kutoa maoni au mawazo yao, na wengine sasa ndio wanaomwaga radhi, uhuru wa habari nao upo, ila wakati mwingine unaleta shida, na serikali ina wajibu wa kusema hapana, kwa kuwa kila kitu kina mipaka yake,” Rais Kikwete.

Aliongeza, “Mtu akisema Kikwete nchi imekushinda, mwache aseme wee kwa kujifurahisha, nchi haijanishinda, hapa ilipo leo ni tofauti na ilivyokuwa mwaka 2005, nilipoichukua, lakini ni lazima tuwe na mipaka ya kusema”.

Uamuzi mgumu Akizungumzia mafanikio ya utawala wake, Rais Kikwete alisema kupitia uongozi wake amefanya uamuzi mgumu wa maendeleo, ambayo mara nyingi si rahisi kwa viongozi kuyafanya hasa ya kuamini utendaji kazi wa wanawake.

“Ni katika utawala wangu nimefanya mambo magumu ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza uwiano wa jinsia kwenye ngazi ya maamuzi jambo ambalo mara nyingi wanaume hawawaamini wanawake, ila ni kupitia uongozi wangu nimeteua zaidi ya majaji 44, wanawake kwenye ngazi ya maamuzi”, alisema Rais Kikwete.

Gesi na umasikini Aliongeza kuwa katika utawala wake kiwango cha umasikini nacho kimepungua kwa asilimia 28, na kwamba mategemeo yake ni kuwa huenda yeye akawa Rais wa mwisho kuongoza Tanzania yenye umasikini, kwani fedha za gesi zilizo mbioni kuja zitamsaidia Rais ajaye kuongoza.

“Pengine nikawa rais wa mwisho kuongoza nchi masikini kwa sababu mapesa ya gesi tunayotazamia kuja yatamsaidia Rais ajaye na nchi itaondokana na umasikini na fedha hizo matokeo yake yataanza kuonekana mwaka 2020”, alisema Rais Kikwete.

Alisisitiza kuwa, ni lazima fedha hizo za gesi ziwekwe akiba, kwani rasilimali gesi ni kitu kinachokwisha, hivyo vizazi vijavyo na wao wana haki ya kuja kukuta matunda ya gesi hiyo.

Suala la albino Akizungumzia uhalifu dhidi ya walemavu wa ngozi (albino), Rais Kikwete alisema vitendo vya uvunjifu wa haki ya kuishi kwa kundi hilo ni jambo lisilovumilika, kwani albino nao wana haki ya kuishi kama binadamu wengine.

Tatizo hapa ni ushirikina, imani hii imewafanya watu wanaua wenzao kisa eti utajiri, jambo ambalo halina ukweli wowote, ila tunaendelea kupambana nalo kwa kuwaelimisha watu na wanaopatikana na hatia vyombo vya sheria vinachukua mkondo wake”, Rais Kikwete.

Alisema tangu aingie madarakani hajaidhinisha hukumu ya kunyongwa kwa wenye hukumu hizo, kwani hukumu hiyo sio nzuri na kuwa muda uliobaki anaamini hataidhinisha hukumu hizo.

“Nasoma hukumu za kunyonga wakosaji wakati mwingine unasoma hukumu mtu kaua wazazi wake kwa kuwakatakata mapanga vipande na kuvitumbukiza chooni kimoja baada ya kingine, unakasirika wee, unasema ngoja nilale kesho nitapata jibu jingine, ila ukweli adhabu ya kifo sio nzuri, ndio maana tunawafunga kifungo cha maisha,” alisema Rais Kikwete.

Aliongeza kuwa, mauaji ya albino ni tatizo linalotia aibu nchi na kuifadhaisha, ila serikali itaendelea na juhudi za kuelimisha jamii kuondokana na dhana potofu ya kwamba viungo vya albino vinaongeza utajiri.

HABARILEO

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene amesema zipo dalili njema za kugundua gesi katika maeneo mengine nchini baada ya kugundulika kwa gesi asilia futi za ujazo trilioni 55.08 katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.

Simbachawene alitaja maeneo ambayo yameonesha dalili ya kuwepo gesi asilia mbali na mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa ni Morogoro na Pangani .

Alisema hayo hivi karibuni Makao Makuu ya Wizara, wakati akitoa nyaraka za ufadhili wa masomo kwa Watanzania 22 waliopata ufadhili kusomea masuala ya mafuta na gesi katika ngazi za Shahada za Uzamivu na Uzamili , nchini China.

Alisema kuwa, uwepo wa gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na dalili ambazo zimeonekana katika maeneo mengine ni kiashiria kuwa, Tanzania inaingia katika uchumi wa gesi .

Alisema taifa linatarajiwa kunufaika na rasilimali hiyo kwa kuwa kiwango kilichopatikana ni kikubwa cha kuifanya nchi kupiga hatua kubwa kimaendeleo kupitia rasilimali hiyo.

“Kuna nchi zina gesi futi za ujazo 10 tu lakini wamepiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia gesi asilia. Kwa kiasi tulichonacho na ambacho tunaendelea kugundua ni wazi kuwa tunaingia katika uchumi wa gesi na ndio sababu tumeanza kutayarisha wataalamu wetu wenyewe,” Simbachawene.

Akizungumzia Sheria zilizosainiwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete, alisema zinaondoa wasiwasi wa namna taifa litakavyonufaika na rasilimali hiyo. Sheria hizo ni Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia, Uwazi na Uwajibikaji na Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi Asilia.

PAPO KWA PAPO zipate habari zote zinazonifikia za siasa muziki, michezo, maisha, Breaking news na nyingine kwa kujiunga hapa na mimi >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos

Tupia Comments