Magazeti

Issue ya wanaume kubambikiwa watoto, watakaopandisha ada, JPM afuta likizo TRA…#MAGAZETINI

on

MTANZANIA

Abiria waliotaka kusafiri kwenda wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, nusura wachapane ngumi wakigombea foleni ya kukata tiketi katika Kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo (UBT).

Gazeti hili lilishuhudia abiria hao wakiwa kwenye foleni wakisubiri kukata tiketi katika mabasi ya Kampuni ya Meridian yanayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Rombo mkoani Kilimanjaro.

Katika tukio hilo, baadhi ya abiria walivuruga utaratibu wa foleni kwa kuwavuka wenzao na kujisogeza mbele ili wakate tiketi, hali iliyosababisha kutoelewana miongoni mwao, huku wengine wakitoleana matusi wengine wakitaka kurusha ngumi.

“Msituchanganye bwana, kama vipi hapa ngumi zitapigwa, sisi tumepanga foleni wao wanataka kujifanya wana haraka sana wanavuruga foleni kwa kujipeleka mbele,” alisikika dada mmoja akilalamika huku wakatishaji wa tiketi za kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa wakichukizwa na hali hiyo wakida inawazuia kufanya kazi zao kwa uhuru.

Mfanyakazi wa Kampuni ya mabasi ya Osaka yanayofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Musoma, aliwalaumu abiria wanaokwenda mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kuwa wamekuwa kero kutokana na kung’ang’ania katika kituo hicho licha ya kuambiwa tiketi za kwenda katika mikoa hiyo zimekwisha.

“Yani hawa abiria wa Rombo wamekuwa kero sana, wanatufanya sisi tushindwe kufanya kazi kwani hawaamini kuwa tiketi zimekwisha wao wanang’ang’ania maofisini tu,” alisisikika akilalamika.

Abiria mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Elisha Ngowi, alisema kuwa tangu juzi alifika kituoni hapo kwa ajili ya kukata tiketi kwenda Rombo, lakini mawakala wa basi la Meridian walimtaka aondoke arudi siku iliyofuata.

Upatikanaji wa tiketi katika kituo hicho umekuwa kama donda ndugu kwani kila mwaka kuelekea Sikukuu ya Krismasi watu wengi hutaabika kutokana na usafiri wa kwenda katika maeneo mbalimbali nchini.

MTANZANIA

Salome Lukumay ambaye ni mke wa aliyekuwa kachero mkuu wa kitengo cha intelijensia cha Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), marehemu Emily Kisamo, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa ajili ya mahojiano.

Mbali na Salome, taarifa zinasema jeshi hilo linawashikilia watu wengine wawili kwa ajili ya mahojiano juu ya kifo cha Kisamo.

Vyanzo mbalimbali vya habari jijini hapa wakiwamo baadhi ya marafiki wa marehemu Kisamo, waliiambia MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, kwamba Salome na watu hao wawili wanashikiliwa kwa kuwa kuna dalili za wao kuwa na mawasiliano na kachero huyo kabla hajauawa kwa kuchinjwa.

Kisamo anadaiwa kuuawa Desemba 18, mwaka huu kwa kuchinjwa na kichwa kutenganishwa na kiwiliwili kisha mwili wake kuwekwa ndani ya buti ya gari yake iliyotelekezwa eneo la Kikwarukwaru, lililopo Kata ya Lemara jijini hapa.

Taarifa za mke huyo wa marehemu zilionekana kuwa za kweli baada ya  MTANZANIA kufika nyumbani kwa marehemu jana na kukuta waombolezaji wakiwa peke yao bila yeye kuwapo.

Hata MTANZANIA lilipotaka kuonana na mke huyo wa marehemu, mmoja wa ndugu zake wa karibu alisema hakuwapo nyumbani tangu mumewe alipouawa wiki iliyopita.

“Tangu jana watu wanakuja msibani kutoa pole, mama mwenye nyumba hayupo. Taarifa zilizopo zinadai bado anaendelea kulisaidia Jeshi la Polisi kwenye upelelezi wa mauaji ya muwe wake,” alisema rafiki wa marehemu akiomba asitajwe jina gazetini kwa kile alichosema yeye si msemaji wa familia.

Naye msemaji wa familia ya marehemu Kisamo, Wakili Mwandamizi wa Kujitegemea Colman Ngallo, alisema hana taarifa za mke wa marehemu kukamatwa.

“Hatuna taarifa yoyote mpaka sasa, polisi wanaendelea na uchunguzi wao,” alisema Wakili Ngallo.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas, alipotakiwa kuzungumzia taarifa hizo jana, aliwaambia waandishi wa habari kwamba tukio hilo ni la kesi ya mauaji, hivyo analazimika kujiridhisha katika utoaji wa taarifa.

Kisamo aliuawa wiki iliyopita na watu wasiojulikana, na polisi waligundua maiti yake ikiwa ndani ya gari baada ya kuendesha msako mkali wa kumtafuta.

MTANZANIA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, amepata kigugumizi kuweka hadharani orodha ya majina ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, licha ya kuliagiza Jeshi la Polisi limpatie.

Amesema hata akiwa na orodha hiyo, haitasaidia kukomesha biashara ya dawa za kulevya na badala yake wameunda mfumo utakaosaidia kudhibiti dawa hizo kuingizwa nchini.

Waziri Kitwanga, alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana, muda mfupi baada ya kumalizika kikao chake na maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi Makao Makuu kilicholenga kumpatia taarifa na maelezo ya mambo mbalimbali aliyoagiza, baada ya kufanya ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya jeshi hilo wiki iliyopita.

“Mtakumbuka hivi karibuni nilitoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kunipatia taarifa za mambo mbalimbali na leo (jana), nimekutana nao, wamenipatia maelezo ya kutosha na tumejadiliana namna watakavyounda mfumo mzuri wa kuhakikisha dawa za kulevya haziingii nchini, na hata zile zilizokamatwa zinateketezwa,” alisema Waziri Kitwanga.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kama amepatiwa orodha hiyo alisema: “Kuwa na orodha haiwezi kusaidia, tumejadiliana  namna ya kuweka mfumo mzuri wa kudhibiti uingizwaji na uuzwaji wa dawa za kulevya.

“Mimi sina ‘list’ (orodha) na sijui kama Rais anayo, nashangaa nyie (waandishi wa habari) mnaandika tu na hata ningekuwa nayo haisaidii kitu maana hatuwezi kwenda kumkamata mtu na kumshtaki bila kuwa na ushahidi.”

Itakumbukwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete katika utawala wake, aliwahi kuuambia umma wa Tanzania kuwa ana orodha ya wauza dawa za kulevya wakubwa.

Hadi anaondoka madarakani Novemba 5, mwaka huu, hakuwahi kuwataja kwa majina wahusika wakuu wa biashara hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Kitwanga alisema mfumo wa sasa wa kudhibiti biashara hiyo hautajali hadhi ya mtu, na kwamba atakayekamatwa atafikishwa kwenye vyombo vya sheria kama watu wengine.

“Mfumo hautajali ni mkubwa, mdogo, mwembamba au mnene, atakayekamatwa anachukuliwa hatua mara moja bila kujali cheo chake,” alisema Kitwanga.

Alisema mfumo huo pia umelenga kuzuia vitendo vya kigaidi na wizi katika bandari nchini.

Alisema kikao hicho pia kilizungumzia suala la ubambikaji wa kesi kwa wananchi, ambapo watahakikisha kabla ya mashtaka mtu aliyekamatwa anashtakiwa kwa kosa alilokamatwa nalo ni si vinginevyo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu, amekanusha taarifa zilizosambaa kuwa jeshi hilo limewasimamisha kazi askari 300, baada ya kubainika kughushi vyeti kisha kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Taarifa hizi hazina ukweli wowote, tunategemea mtu aliyesambaza atasakwa na atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” alisema IGP Mangu.

MTANZANIA

Wakati shinikizo la kimataifa juu ya hali ya Zanzibar likipamba moto, Rais Dk. John Magufuli, amekutana na aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo kwa saa 2.

Hali ya kisiasa ya Zanzibar, tayari inatajwa kuiathiri Tanzania kwa kusababisha ikose zaidi ya Sh trilioni 1 zilizokuwa zitolewe na Marekani, ikiwa ni sehemu ya fedha za msaada wa Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC).

Taarifa iliyotolewa na Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema mazungumzo hayo yametokana na maombi ya Maalim Seif ya siku nyingi na kuwa yalihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

“Viongozi hawa kwa pamoja wamejadili hali ya kisiasa Zanzibar na wamefurahishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea. Rais Dk. Magufuli amewapongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Maalim Seif na viongozi wote wanaoshiriki katika mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano Zanzibar.

“Rais Magufuli pia amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu, wakati mazungumzo baina ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), yakiendelea huko Zanzibar,” ilisema taarifa ya Ikulu.

Taarifa hiyo, ilisema Maalim Seif amemweleza Dk. Magufuli juu ya hali ya siasa Zanzibar, huku kiongozi huyo wa Jamhuri ya Muungano akimshukuru kwa taarifa yake aliyosema ni nzuri na akamsihi waendelee na mazungumzo hadi mwafaka upatikane.

Ilisema majadiliano yanayoendelea yanatoa fursa ya kudumishwa kwa utulivu na sifa njema ya Tanzania.

“Wote kwa pamoja wamewaomba wananchi waendelee kuwa watulivu ili kutoa nafasi ya majadiliano yanayoendelea kufikia hatma njema. Wameelezea matumaini yao kuwa vyama vya CCM na CUF haviwezi kushindwa kupata suluhu ya mgogoro huo,” ilisema taarifa hiyo.

Maalim Seif pia amekutana takribani mara saba na Dk. Shein, huku mazungumzo yao yakiwa ni siri kubwa.

Baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi visiwani humo, Serikali ya Uingereza na ile ya Ireland Kaskazini zilipinga uamuzi huo.

Serikali hizo zilisema hazioni sababu ya kufutwa matokeo hayo, baada ya waangalizi wa kimataifa kufurahishwa na uchaguzi ulivyofanyika kwa amani.

HABARILEO

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeendelea kutamba katika chaguzi ndogo baada ya kushinda katika Jimbo la Masasi mkoani Mtwara huku ikiwa na kila dalili ya kutangazwa mshindi Ludewa mkoani Njombe.

Katika chaguzi saba zilizofanyika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, CCM imezoa viti sita huku kimoja cha Kijitoupele mjini Unguja kikisubiri tarehe mpya ya uchaguzi.

CCM imeshinda katika majimbo ya Lushoto, Handeni Mjini, Lulindi, Ulanga Mashariki, Masasi na Ludewa ambayo ingawa matokeo rasmi yalikuwa hayajatangazwa wakati tukienda mitamboni, lakini CCM ilikuwa ikiongoza kata 20 na zilikuwa zimebaki kata sita.

CCM imepoteza tena Jimbo la Arusha Mjini. Mgombea ubunge Jimbo la Masasi kupitia CCM, Rashid Chuachua ameibuka kidedea kwa kupata ushindi katika uchaguzi huo mdogo juzi kwa kumshinda mpinzani wake wa karibu kutoka Chama cha Wananchi (CUF).

Uchaguzi huo mdogo wa ubunge ulifanyika kutokana na kushindwa kufanyika Oktoba 25 baada ya mgombea ubunge wa jimbo hilo wa chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi kufariki dunia Oktoba 15, mwaka huu katika Hospitali ya Misheni ya Nyangao mkoani Lindi kutokana na tatizo la shinikizo la damu.

Akitangaza matokeo hayo usiku wa kuamkia jana, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Masasi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Masasi, Fortunatus Kagoro alisema wananchi 60,598 waliandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, huku Chuachua akipata kura 16,597 na mpinzani wake wa karibu kutoka CUF, Ismail Makombe (Kundambanda) akipata kura 14,069.

Wagombea wengine ni Mustapha Swalehe wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alipata kura 512, Dk Peter Mrope wa ACT- Wazalendo kura 347 huku mgombea wa NLD akiambulia kura 70 pekee.

Wakala wa CUF ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma alisema mgombea wao ameshindwa kwa kura na kwamba Tume ya Uchaguzi imetenda haki kwa kuendesha uchaguzi wa uwazi na ukweli kuanzia kwenye vituo vya upigaji kura hadi kwenye majumuisho ya matokeo.

Katika Jimbo la Ludewa, mgombea wa CCM, Deo Ngalawa amewaacha kwa mbali wagombea wengine katika matokeo ya kata 20 zilizokuwa matokeo yake yamepatikana.

HABARILEO

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hana kinyongo na mtu yeyote kwa sababu alitangaza msamaha siku aliyokabidhiwa cheti kuwa Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na kusisitiza kuwa siasa ziliisha tangu Oktoba 25, mwaka huu.

Alitoa kauli hiyo juzi jioni wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mikutano wa Likangala wilayani Ruangwa mkoani Lindi. “Sina kinyongo na mtu yeyote na roho yangu iko huru, hivi ndiyo nilivyo.

Nilikwishatangaza msamaha kwa hiyo ninawaomba wale niliowakwaza nao pia wanisamehe… lakini ninawasihi kuwa milango iko wazi, wawe huru kurudi wakati wowote,” alisema huku akishangiliwa na wananchi hao.

Aliwaeleza wakazi hao wa Ruangwa na vitongoji vyake kwamba amekuja kuwashukuru kwa kumchagua na kumpa kura nyingi la sivyo asingefanikiwa kuwa mbunge wao. “Kipekee ninamshukuru Mungu aliyemuongoza Mheshimiwa Rais na kutupa sisi wana Ruangwa tusaidiane kulibeba jukumu hili.

Ninawahakikishia kuwa pamoja na jukumu hili la kitaifa, sitawaacha wala sitawaangusha. Nitakwenda mikoa mingine hapa nchini ili kuwasikiliza na kuwahudumia Watanzania huku nikijua kwamba mpo salama.”

HABARILEO

Rais Paul Kagame wa Rwanda amefurahishwa na hatua ambazo Rais John Magufuli anazichukua, hasa katika usimamizi na utendaji kazi wa bandari huku akimhakikishia kuwa Rwanda iko tayari kushirikiana na Tanzania, hasa katika kuitumia Bandari ya Dar es Salaam.

Siku chache baada ya kuingia madarakani, Rais Magufuli akimtumia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam, ambako alifichua ufisadi wa mabilioni ya shilingi kutokana na upotevu wa makontena, ambayuo hayakulipiwa kodi stahili kwa serikali.

Kutokana na ufisadi huo, Rais aliivunja Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi Massawe na kusimamisha maofisa kadhaa wa bandari hiyo na wengine wanaohusika na usimamizi wa bandari kavu.

Aidha, alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade na maofisa wengine wa mamlaka hiyo, ambao miongoni mwao tayari wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kutokana na ubadhirifu huo.

Kutokana na hilo, Rais Kagame kupitia kwa Balozi wake nchini, Uegene Kayihura, amempongeza Rais Magufuli kwa hatua alizochukua kusafisha uozo katika bandari hiyo, ambayo Rwanda inapitisha asilimia 70 ya mizigo yake. Dk Magufuli jana alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi Kayihura Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Kayihura aliwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais Kagame ambaye alimpongeza Dk Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Balozi Kayihura, Rais Kagame amefurahishwa na hatua ambazo Rais Magufuli anazichukua hasa katika usimamizi na utendaji kazi wa bandari na kumhakikishia kuwa Rwanda iko tayari kushirikiana na Tanzania hasa kuitumia Bandari ya Dar es salaam ambayo hupitisha asilimia zaidi ya 70 ya mizigo ya Rwanda.

Aliongeza kuwa Rwanda na Tanzania ni nchi marafiki na majirani, hivyo kuna kila sababu ya kujenga ushirikiano madhubuti katika sekta ya uchumi. Rais Magufuli alimuomba Balozi Kayihura, kumfikishia Rais Kagame salamu za shukrani kwa kumpongeza kuchaguliwa kuwa rais wa Tanzania na kwamba amedhamiria kuimarisha zaidi ushirikiano na Rwanda.

Alimhakikishia Balozi Kayihura kuwa Serikali yake ya Awamu ya Tano, itaendelea kushirikiana na Rwanda ili wananchi wa nchi zote mbili wanufaike kimaendeleo. Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amemhakikishia Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Dk Tonia Kandiero kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na benki hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dk Magufuli alisema hayo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi huyo. Pamoja na kumhakikishia ushirikiano, Rais Magufuli alitoa mwito kwa benki hiyo kupunguza michakato ya kuelekea katika utekelezaji wa miradi na badala yake ameshauri uwepo utaratibu wa haraka unaowezesha kuanza kwa miradi katika kipindi kifupi baada ya fedha kutolewa.

Kwa upande wake, Dk Kandiero pamoja na kumpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya Tano, amemhakikishia kuwa benki iko tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maendeleo kama ambavyo imekuwa ikifanya na kwamba kwa sasa imetenga dola bilioni 2.3 kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema katika mipango yake, ADB imelenga kujielekeza katika utoaji wa mikopo katika sekta ya nishati na usafiri. Naye Dk Magufuli aliipongeza ADB kwa kuamua kujielekeza katika sekta hizo za nishati na usafiri na pia aliisisitiza kuangalia namna itakavyounga mkono mradi wa ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa.

HABARILEO

Serikali imesema itachukua hatua kali kwa baadhi ya walimu wakuu wa shule za msingi na wakuu wa shule za sekondari, wanaoendelea kutoza fedha za uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza na kutoza michango mbalimbali kwa wazazi kwa muhula unaoanzia Januari 2016.

Aidha, Waziri Mkuu amesema serikali imekwishatenga kiasi cha Sh bilioni 137 kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni mwakani, huku akionya kuwa atakayezitumia vibaya, atatumbuliwa jipu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya alisema wamepokea malalamiko kutoka kwa wadau wa elimu kwamba kuna baadhi ya shule bado zinatoza michango.

“Wanaofanya hivi wanakiuka maagizo ya serikali kwa makusudi, ikumbukwe kwamba Rais Dk John Magufuli alikwishatamka wazi kuwa kuanzia mwaka wa masomo 2016, elimu itatolewa bure bila malipo kwa shule zote za umma nchini. Agizo hilo liko wazi na halina mjadala,” alisema Manyanya.

Alisema kutokana na tamko hilo, wizara ilitoa Waraka Namba Tano wa Mwaka 2015 kuhusu utoaji wa elimu pasipo malipo na Waraka Namba Sita wa Mwaka 2015 uliotoa ufafanuzi na maelekezo ya utekelezaji wa jambo hilo.

“Nasisitiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wa wilaya, miji na manispaa zote nchini wafuatilie kwa karibu utekelezaji wa maagizo haya. Aidha watoe taarifa pale ambapo walimu wakuu na wakuu wa shule wanakwenda kinyume ili hatua stahiki zichukuliwe mara moja,” alifafanua Naibu Waziri.

Pia alitoa mwito kwa jamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa katika ofisi za elimu za Kata, Wilaya, Mkoa, Kanda au Makao Makuu ya wizara pale wanapobaini kuna shule zinazokiuka maagizo hayo. Katika hatua nyingine, Manyanya alisema serikali itaendelea na utaratibu wa utoaji wa mikopo kwa wote hasa wale wanaotoka kwenye familia duni na yatima waliotimiza vigezo.

“Nasisitiza wanafunzi wote waliopatiwa mikopo waitumie vizuri ili iweze kuleta tija ili wanafunzi wanaonufaika waweze kujisaidia wao wenyewe, familia zao na waweze kuchangia maendeleo ya nchi,” alisema na kuongeza kuwa watachukua hatua kwa vyuo vikuu vitakavyobainika kuchelewesha mikopo kwa wanafunzi wake baada ya kuipokea kutoka Bodi ya Mikopo kwani ni kinyume cha maagizo ya Rais na linaleta usumbufu usio wa lazima.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa mjini Ruangwa juzi, alisema; “Kazi ya utumbuaji majipu imezaa matunda kwani tumeweza kupata fedha za kugharimia elimu ya bure, ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa kampeni.

Fedha hiyo tunayo, na tumeshaanza kuisambaza kwa sababu tunataka shule zikifunguliwa Januari 2016 watoto waanze kufaidika.” “Atakayezigusa fedha hizi na kuzitumia vibaya ni lazima tutamtumbua tu! Tumeshawapa maelekezo wakurugenzi wa halmashauri pamoja na maafisa elimu wao na kuwaonya kuhusu matumizi ya fedha hizo,” alisema.

“Hatuhitaji mwanafunzi achangishwe hela ya mitihani, na zile shilingi 10,000 kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma sekondari nazo pia tutazipeleka. Na huu ni mpango wa dharura ambao haukuwemo katika bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa hiyo tutalazimika kuziombea kibali,” alisema.

Alisema Serikali imekwishafanya hesabu za kubaini kiasi kinachohitajika kwa ajili ya milo ya watoto shuleni kwa wale walioko bweni na wale wa kutwa. Hesabu tunazo na tumebaini kuwa tutazimudu,” alisema huku akishangiliwa.

“Serikali ilitoa ahadi kwa wananchi na sisi tumedhamiria kuzitekeleza. Tuliahidi elimu bure nasi tutaitekeleza.” Imeandikwa na Hellen Mlacky, Dar na Mwandishi Maalumu, Ruangwa.

MWANANCHI

Kasi ya Rais John Magufuli kuitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imewalazimu kufuta likizo kwa wafanyakazi wake wote ili kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa kiwango cha juu.

Wakati uongozi wa mamlaka hiyo ukifuta likizo hizo, tayari Rais Magufuli ameipongeza kwa kukusanya mapato ya zaidi ya Sh1.3 trilioni mwezi huu.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi, Richard Kayombo alisema lengo ni kuhakikisha kuwa mapato zaidi yanakusanywa.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa kufutwa kwa likizo hizo kutokana na mtikisiko ulioikumba mamlaka hiyo ukiwamo wa kuibuliwa kwa ufisadi katika ukusanyaji wa mapato uliosababisha watumishi 35 kuchukuliwa hatua mbalimbali, wanane kati yao wakifikishwa mahakamani akiwamo Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki.

Wafanyakazi wa TRA wataungana na wenzao wa Tanesco ambao pia likizo zao zilifutwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kwa lengo la kushughulikia tatizo la umeme nchini huku akisisitiza kuwa hataki kusikia kukatika katika kwa nishati hiyo nchini.

Mkoani Kilimanjaro nako, mkuu wa mkoa huo, Amos Makalla alipiga marufuku likizo za wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa idara kwenye mkoa wake ili kutekeleza kwa vitendo hotuba na maagizo ya Rais Magufuli. Msimamo wa Tucta.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Desemba 2, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Hezron Kaaya alitaka ieleweke kuwa likizo ni haki ya mfanyakazi na kama kuna mwajiri anataka kuzuia likizo hiyo, anapaswa kufanya majadiliano na mwajiriwa ili wakubaliane kulingana na taratibu za sheria zilizopo.

MWANANCHI

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema ataanza kuwatimua wafanyakazi wazembe, wavivu na wasiokuwa na tija kwenye Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika muda wa siku 90 zijazo.

Pamoja na kuwataka watendaji wake kwenda na kasi yake ili asiwepo atakayeshindwa hivyo kulazimika kuachia ngazi, Profesa Muhongo ametoa maagizo matatu kwa Tanesco.

Akizungumza juzi katika Kituo cha Somanga, Lindi wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku tano ya kutembelea vituo vya kuzalisha umeme kuanzia Hale mkoani Tanga, Nyumba ya Mungu mkoani Kilimanjaro Mtera (Dodoma), Kihansi (Iringa), Kidatu (Morogoro), Mamlaka ya Bodi ya Maji ya Mto Rufiji (Rubada), Somanga (Lindi) na mitambo ya gesi ya Madimba ya kuchakata gesi mkoani Mtwara, Profesa Muhongo alisema: “Siko tayari kubaki na wazembe.

Afadhali nibaki na watumishi wachache wanaojituma. Sasa ifikapo Februari mwakani, mfanyakazi atakayebainika kashindwa kwenda na kasi yangu atalazimika kuitema nafasi ili ichukuliwe na vijana.

Maagizo matatu Akiwa Somanga Profesa Muhongo aliamuru Tanesco kuwasha mashine zote zilizokuwa zimezimwa kwa ajili ya dharura ili zipeleke umeme katika maeneo yenye uhaba akisema wizara yake imedhamiria kumaliza tatizo hilo. Agizo hilo lilitolewa baada ya kupewa taarifa na Meneja wa Somanga, Mhandisi Job Leonard kuwa kati ya mashine tatu za kituo hicho, moja ndiyo inafanya kazi, ya pili imepumzishwa; ya tatu inasubiri kufanyiwa matengenezo mwakani.

“Kila mara nawaambia Tanesco mmekosa ubunifu, mnajifanya mnabana matumizi huku Watanzania wanalalamikia umeme. Endapo mngewasha mashine iliyobaki si ingeweza kupeleka umeme katika gridi ya taifa ili tupunguze adha kwa wananchi?” alisema. “Suala hili halipo hapa Somanga nimetaarifiwa hadi Biharamulo lipo. Huko nako nitakwenda kuangalia mitambo iliyowekwa bila kufanya kazi,” alisema Profesa Muhongo na akataka tatizo la mashine kutowashwa litatuliwe kuanzia wiki hii na waache visingizio vya kukauka kwa Bwawa la Mtera. Agizo jingine alilolitoa ni kwa wakulima wenye mashamba makubwa kufungiwa maji ili yaelekezwe katika mabwawa ya kuzalisha umeme.

Agizo hilo linatarajiwa kuathiri mashamba makubwa ya mpunga ya wawekezaji wa Kapunga na Mbarali, na wakulima wadogo wadogo wa Madibira.

Shamba la Kapunga linachukua asilimia 70 ya maji ya Mto Ruaha na Mbarali limechukua maji ya Mto Balali wakati Madibira wanatumia maji ya Mto Lyandembela, mito ambayo hutiririsha maji katika Bwawa la Mtera.

Katika agizo la tatu, Profesa Muhongo ametaka Tanesco na Shirika la Mandeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kukaa pamoja kujadiliana namna ya kumpatia umeme mwekezaji wa kiwanda cha saruji, Alhaji Aliko Dangote.

Alisema kiwanda hicho kimeshaanza uzalishaji wa sarujii lakini kimelazimika kukodi mitambo nje kwa ajili ya kuzalisha umeme, mbali na kuwa na mitambo inayohitaji gesi asilia na makaa ya mawe ili kujizalishia umeme wa megawati 75. “Wakipatiwa makaa ya mawe au gesi watazalisha megawati 75, ambazo wataipa Tanesco 35 na wao kubaki na 45 kama wanavyohitaji,” alisema Profesa

 Unataka kutumiwa MSG za habari zote kubwa kutoka kwa Millard Ayo? ukiwa na line ya tiGO andika ‘AYO’ tuma kwenda 15510, msg utayotumiwa jibu OK ili uanze kupokea matukio yote kwa sms, pia ungana na Millard Ayo kwenye Twitter, FB, Instagram na YouTUBE wa kubonyezahapa>>>INSTAGRAM TWITTER FB YOUTUBE.

Tupia Comments