Uchunguzi unaoendelea wa sakata la usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil Neymar kwenda Barcelona umesimamishwa baada ya FIFA kukataa kuwasilisha baadhi ya vielelezo kwa ajili ya kesi hiyo kuendelea.
Jaji a mahakama moja nchini Spain Pablo Ruz alitoa ombi la ushahidi wa vielelezo kadhaa vinavyohusisha uhamisho huo wa Neymar kutoka Santos kwenda Catalunya, vielelezo hivyo vilikuwa vinahusisha hati kadhaa kutoka FIFA pia mkataba wa Neymar na kampuni ya N&N (kampuni inayomilikiwa na wazazi wa mchezaji), mkataba wake na pamoja na hati zingine za masuala ya kifedha kutoka kwenye kampuni ya Deloitte.
Hata hivyo uchunguzi huo ulishindikana kufuatia FIFA kukataa kutoa taarifa hizo zilizohitajika wakisema ni vitu vya siri na inabidi vikachukuliwe kwenye mamlaka za nchi ya Uswis yalipo makao makuu ya FIFA.
Jaji Ruz sasa atatuma barua kwenda kwenye mahakama nchini Uswis kuomba msaada wa kupatiwa vilelezo vya ushahidi vinavyohitajika, jambo linawekana kufanikiwa.
Sakata la usajili wa Neymar tayari limemuondoa Sandro Rossell katika urais wa klabu ya FC Barcelona, baada ya kufunguliwa kwa kesi ya matumizi mabaya fedha yaliyolizunguka suala la uhamisho wa mchezaji huyo.