Shirika la Nyumba NHC limesema limelipa kodi mbalimbali inayofikia takriban shilingi bilioni 22.0 kwa mwaka 2021/2022. Aidha, Shirika limelipa Gawio Serikalini la shilingi milioni 750 kwa mwaka 2021/2022.
Gawio hili ni kiwango kinachopaswa kulipwa na Shirika kila mwaka kutokana na maelekezo ya Msajili wa Hazina.
Shirika limekuwa likichangia kila Mwaka Gawio la Serikali na kulipa kodi za Serikali pamoja na kujiendesha lenyewe kibiashara bila ya kupata ruzuku kutoka Serikalini.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHIRIKA la Nyumba NHC Nehemia Mchechu ameeleza hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waadishi wa habari akieleza ufanisi wa shirika hilo katika utekelezaji wa majukumu yake.
Amesema kuwa shirika hilo licha ya kwamba ni la Umma lakini halipati ruzuku kwani kwa mujibu wa sheria zao za 2005 zinawataka kujiendesha kibiashara.
‘Ni jambo jemaa kuona kuna baadhi ya mashirika machache ambayo yanatoa huduma,mengine yanasimamia biashara ndani ya serikali hivyo sisi tupo kwenye kundi la mashirika yanayotakiwa kufanya biashara- amesema Mkurugenzi huyo
Akizungumzia mipango ya shirika hilo amesema shirika limejipanga kuendelea kukamilisha ujenzi wa miradi iliyokuwa imesimama ikiwemo mradi wa Morocco Square ambao ujenzi wake upo kwenye hatua za mwisho kukamilika ambao unatarajiwa kuanza kutumika rasmi mwishoni mwa mwezi Machi 2023.
Ameitaja mipango mingine kuwa ni utekelezaji wa mradi wa Samia Housing Scheme (SHS) katika maeneo mbalimbali nchini na tumeanza ujenzi wa nyumba 560 eneo la Kawe Jijini Dar es Salaam na tutaanza Ujenzi wa nyumba 240 eneo la Medeli Jijini Dodoma kwa ajili ya kuuza.
Amebaisha kuwa programu ya nyumba za Samia Housing Scheme(SHS) imelenga kutatua changamoto ya Makazi bora kwa watu wa kipato cha chini kati.
Wanatarajia kuwa asilimia 50 ya nyumba za program hii zitajengwa Jijini Dar es Salaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine nchini asilimia 30.
Programu hii inayotekelezwa kwa awamu itakuwa na jumla ya nyumba 5000 zitakazogharimu takriban TZS 466 bilioni.
“Programu hii inaenzi kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuijenga nchi yetu kiuchumi na kijamii ambapo kutakuwa na ujenzi wa Shopping Mall ya kisasa Jijini Dodoma ili kuweza kuwapa wakazi wa Jiji hilo eneo zuri na kubwa la kujipatia huduma mbalimbali za kijami,” Amesema Nehemia Mchechu
Aidha Mchechu amesema kuwa kuhusu mizania ya Shirika hilo imefikia kiasi cha Shilingi Tril 5.04 ambapo sehemu kubwa ipo katika Ujenzi wa majengo Mbalimbali.
Ameendelea kueleza kuwa mizania hiyo imekuwa kwa asilimia 12 sambamba na mtaji wao kukua kutokana na thamani ya Mali na uzalishaji ndani ya shirika hilo kuongezeka na kufikia Tril 3.4.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika huduma za Jamii Shirika hilo limejikita katika kurudisha kwa Jamii kwa kuwezesha Wananchi kupanga nyumba na hivyo kujipatia mahitaji mbalimbali.
Kuhusu sekta ya Elimu Mchechu amesema shirika hilo limesaidia Ujenzi wa Madarasa lakini pia Afya wamesaidia Ujenzi wa baadhi ya vituo ambapo kiasi kilichotumika katika huduma hizo za Jamii ni Shilingi Mill 415.