Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu imeonya juu ya kuzorota kwa huduma za afya huko Gaza ikionyesha kuwa ni hospitali kumi na mbili tu kati ya 36 zinazofanya kazi kwa sehemu katika eneo lililokumbwa na migogoro.
Chombo hicho cha Umoja wa Mataifa kilisema hata kukiwa na hospitali za ziada zinazofanya kazi hakuna “mahali popote karibu vya kutosha” miundombinu ya afya kukabiliana na makumi ya maelfu waliojeruhiwa katika vita.
Afisa wa Masuala ya Kibinadamu wa OCHA Gaza Yasmina Guerda alisema kuwa “mfumo wa huduma za afya uko magotini” huko Gaza.
“Wengi wamepoteza viungo vyao, wengi wana majeraha ya kiwewe ya ubongo, na maelfu wamepoteza uwezo wao wa kusikia kwa sababu ya milipuko ya mara kwa mara,” aliongeza.
Guerda alisema kuwa pamoja na hayo “kumekuwa na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya vituo vya kutolea huduma za afya, hospitali hasa, katika ukiukaji wa moja kwa moja wa sheria za kimataifa za kibinadamu”.
Mhudumu mmoja wa afya alisema yeye na timu yake walishambuliwa walipokuwa wakitoka hospitalini kwenye ‘barabara iliyoteuliwa’, akiongeza kuwa anatumai kuwa ataweza kuondoka Gaza kuendelea na matibabu.
Israel ilianza mashambulizi yake baada ya shambulio la Hamas Oktoba 7 ambapo wanamgambo walivamia kusini mwa Israel, na kuua takriban watu 1,200, wengi wao wakiwa raia, na kuwateka nyara takriban 250.