Zaidi ya watu 70 wametoweka nchini Nigeria tangu Jumamosi, wakati boti iliyokuwa imebeba wafanyabiashara wa eneo hilo ilipozama kwenye mto kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, maafisa wa idara ya huduma za dharura wamesema.
Boti iliyokuwa imebeba takriban watu 100 wakiwemo wafanyabiashara na watoto ilipinduka siku ya Jumamosi katika jimbo la Taraba wakati ikielekea sokoni katika kijiji cha Mayo Ranewa wilayani Karim Lamido.
“Watu sabini na watatu hawajulikani waliko na miili 17 imeopolewa mtoni,” Ladan Ayuba, mkuu wa idara ya huduma za Dharura ya eneo hilo nchini Nigeria (NEMA), ameliambia shirika la habari la AFP.
Usafiri wa majini umeendelezwa sana nchini Nigeria, ambapo ajali hutokea mara kwa mara, hasa wakati wa msimu wa mvua, kwenye njia za maji zisizodhibitiwa, na boti zisizotunzwa vizuri na mara nyingi zimejaa kupita kiasi.
Mapema mwezi huu, watu 40 waliripotiwa kutoweka na kudhaniwa kuwa wamekufa baada ya boti iliyokuwa imebeba abiria 50 kupinduka katika jimbo la Kebbi kaskazini magharibi mwa Nigeria, kulingana na mamlaka za eneo hilo.