Kocha Mkuu wa Ufaransa, Didier Deschamps amesema ‘alishangazwa’ sana na kiungo wa Juventus, Paul Pogba kufeli majaribio ya dawa za kulevya katika klabu ya Juventus.
Deschamps pia anasisitiza kuwa Pogba hangeweza kuchukua dawa iliyopigwa marufuku akijua.
Pogba anaweza kupigwa marufuku kwa muda mrefu baada ya testosterone kupatikana katika mfumo wa mwili wake wakati wa majaribio ya hivi karibuni ya dawa na Juventus.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 ana fursa ya kuwasilisha rufaa lakini anaweza kusimamishwa kazi kwa hadi miaka minne iwapo atapatikana na hatia.
Hata hivyo, Deschamps ambaye amefanya kazi nyingi na Pogba wakati walipokuwa pamoja katika timu ya taifa ya Ufaransa, pia alifichua kuwa tayari ameshawasiliana na nyota huyo wa zamani wa Manchester United.
“Ni wazi nimeshangaa sana lakini sina cha kuhukumu suala hilo,” Deschamps aliiambia TF1.
“Ana mambo mengi kwenye sahani yake, ni wakati mgumu sana. Nitapata muda wa kuzungumza naye siku chache zijazo, tayari nimeshamtumia ujumbe.”
Alipoulizwa kama anaamini Pogba angechukua dawa iliyopigwa marufuku, Deschamps aliongeza: “Siwezi kufikiria, nikimjua asingefanya hivyo.”