Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania imechambua rufaa zingine 34 za ubunge kati ya hizo, 13 imewarejesha kugombea ubunge, 21 imezikataa.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk. Wilson Mahera imesema rufaa hizo 13 zinahusu majimbo ya Singida Magharibi, Madaba, Ilemela, Namtumbo, Bagamoyo, Liwale, Tunduma, Bukene na Kigamboni.
NEC imekataa rufaa saba za wagombea ambao hawakuteuliwa kutoka majimbo ya Singida Magharibi, Bahi, Handeni Vijijini, Madaba, Singida Mashariki, Ileje, Meatu na Bukene.
Mahera amesema, tume hiyo baada ya uchambuzi, imekataa rufaa 14 za kupinga walioteuliwa kutoka majimbo ya Mwanga, Mafinga, Ilala, Manonga, Igunga na Kisesa.
“Idadi hii inafanya jumla ya rufaa za wagombea ubunge zilizofanyiwa uamuzi na tume kufikia 89, hii inafuatia taarifa kwa umma iliyotolewa jana tarehe 8 Septemba 2020 ambapo tume ilitangaza uamuzi wa rufaa 55″ Mahera
“Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo kila siku. Wahusika wa rufaa hizo watajulishwa kwa barua juu ya uamuzi wa tume” Mahera
Katika uamuzi wa rufaa hizo 55, tume iliwarejesha wagombea 15 wa ubunge na 40 ikizikataa, ambapo kati ya hizo 15 ikikubali uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi wa kutowateua na 25 za kupinga kuteuliwa.