Katibu tawala mkoa wa Njombe Judica Omari, amewataka wananchi mkoani humo kutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali za mitaa na vijiji ambao wameanza kazi baada ya kukamilika kwa zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa lililofanyika Novemba 27 mwaka huu.
Judica ametoa wito huo wakati wa sherehe za maadhimisho wa miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara zilizofanyika kimkoa katika viwanja vya posta mjini Njombe kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kupanda ya matunda na vivuli,kufanya mazoezi pamoja na usafi kwenye kituo cha afya Njombe mjini.
Judica pia ametumia fursa hiyo kuishukuru kamati za ulinzi wa usalama za mkoa na wilaya kwa kuhakikisha zoezi hilo linafanyika katika hali ya usalama bila vurugu.
“Viongozi wetu wote wamechaguliwa kwa haki na ushiriki wa wananchi ulikuwa ni mkubwa sana na kwa asilimia kubwa, lakini viongozi katika ngazi zetu zote za vijiji, mitaa, vitongoji zoezi lilienda vizuri,” amesema Judica.
Aidha Katibu Tawala, amesema kuwa uongozi mpya umeanza kufanya kazi kwa kutekeleza majukumu ya kuendeleza maendeleo katika nchi yetu.
“Ninachoomba tutoe ushirikiano wa hali ya juu, tushikamane pamoja na hawa viongozi waliochaguliwa katika mamlaka zetu za serikali za mitaa ili kuhakikisha kwamba serikali yetu inaongozwa salama lakini maendeleo zaidi yanaenda kupatikana,” amesema.
Alifafanua kuwa wananchi wanachohitaji hivi sasa ni maendeleo na kuishi kwa usalama ili kazi zao za uchumi ziweze kwenda vizuri.
Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Njombe, SACP Rashid Mangara amewapongeza wananchi mkoani humo kwa kufanikisha zoezi la uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu.
Mangara ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake ambayo amekuwa akiyatoa ikiwemo kupanda miti ili kulinda mazingira.
kwa upande wake, Mkuu wa Dawati la Uelimishaji kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Njombe, Eliadh Mdegela ametoa rai kwa wanachi na watumishi kutojihusisha na vitendo vya rushwa ili kuweza kuwa na ustawi katika taifa.
Naye Meneja wa Mamlaka ya Mapato Nchini TRA mkoa wa NJOMBE Spesioza Owure amesema miaka 63 ya Uhuru inaonekana hadi kwa wafanyabiashara ambao kwa sasa wapo huru kufanya biashara na kulipa kodi hali inayorahisisha kwa watumishi wa TRA kukusanya mapato kwa wakati.
Katika maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara zaidi ya miti 100 ya matunda na kivuli imepandwa mkoani Njombe.