Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza imetangaza kuwa zaidi ya malalamiko 70,000 kuhusu unyanyasaji wa kingono yamesajiliwa katika idara za polisi za nchi hiyo.
Ongezeko la visa vya ubakaji na uhalifu dhidi ya wanawake na wasichana nchini Uingereza na kutoshughulikiwa malalamiko yao, na hasa uhalifu unaofanywa na polisi, kumepelekea mashirika ya kiraia yanayotetea haki za wanawake nchini humo kukosoa na kulalamikia vikali jambo hilo.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza imetangaza kuwa kufichuliwa vitendo vya ubakaji na mauaji dhidi ya wanawake na wasichana vinavyofanywa na maafisa wa polisi kumekuwa kukigonga vichwa habari, ambapo katika kipindi cha miezi 6 iliyopita malalamiko 70,633 yamewasilishwa katika idara za polisi kuhusu unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake.
Wakati huo huo, takwimu kutoka Baraza la Wakuu wa Kitaifa wa Polisi ya Uingereza (NPCC) hivi karibuni zilionyesha kuwa kuanzia Oktoba 2021 hadi Aprili 2022, kulikuwa na madai 1,438 ya ukatili dhidi ya wanawake nchini, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kingono.
Malalamiko hayo yameripotiwa dhidi ya maafisa wa polisi 1,539 ambapo chini ya asilimia moja ya washtakiwa wamefutwa kazi.
Kwa mujibu wa takwimu za NPCC, kati ya malalamiko hayo, asilimia 9 ya malalamiko dhidi ya maafisa wa polisi yalihusiana na tabia ya unyanyasaji, asilimia 6 ubakaji na asilimia 5 walitumia vibaya nafasi zao ili kufikia malengo ya ngono.
Yvette Cooper, afisa anayehusika na masuala ya ufuatiliaji katika wizara ya mambo ya ndani wa Chama cha Labour cha Uingereza, hivi karibuni alisema kuwa wanawake 300 wananyanyaswa kingono katika nchi hiyo kila siku.