Leo January 15, 2019 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Wafanyabiashara sita kulipa faini ya Sh.50,000 au kwenda jela miezi 2 baada ya kukiri kosa la kuondoka nchini kwenda Afrika Kusini bila kuwa na Passport.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Wakili wa Uhamiaji, Novatus Mlay kuwasomea mashtaka yao washtakiwa hao ambao walikiri makosa na kusomewa maelezo ya awali (Ph).
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa January 14, 2019 walikutwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakiwa wameondoka kwenda Afrika Kusini bila kuwa na vibali (Hati ya Kusafiria).
Baada ya kusomewa shtaka hilo, wastakiwa hao ambao wapo tisa, wawili walikana na sita walikiri kosa na kusomewa maelezo ya awali ambayo nayo waliyakubali.
Kutokana na hatua hiyo, Hakimu Mashauri amesema anawahukumu washtakiwa kulipa faini ya Sh. 50, 000 ama kwenda jela miezi 2 kwa kila mmoja, ambapo washtakiwa watano kati ya sita waliohukumiwa waliweza kulipa faini na kuachiwa huru.
Kwa ujumla washtakiwa walikuwa tisa, ambapo sita walihukumiwa baada ya kukiri kosa ambao ni Mussa Njogo, Hemed Semi,Mohammed Moshi(27),Carlos Mhando (22), Lista Mlawi (20) na Abdallah Marola (25).
Waliokana makosa yao ni Shaibu Mohammed (26), Ibrahim Mketa (30) na Kassim Kitapi (22) ambapo wamerudishwa mahabusu, ambapo watarudishwa mahakamani hapo January 30, 2019 ili wasomewe maelezo ya awali kutokana na upelelezi kukamilika.