Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, na Mlezi wa UVCCM Vyuo na Vyuo Vikuu Tanzania, Mohammed Ali Kawaida amewataka vijana kuacha kutumika kisiasa kwa mwamvuli wa ahadi za kupewa ajira, kwani tatizo la ajira ni la Dunia nzima na sio Tanzania pekee ambapo pia amewasihi vijana wote wenye sifa kujitokeza kugombea katika Uchaguzi utakaofanyika mwaka 2024 na 2025.
“Vijana amkeni, msikubali kutumika kusukuma ajenda za watu ili waweze kufanikisha mambo yao kwa maslahi yao binafsi. Serikali inaendelea kuchukua jitihada mbalimbali kuhakikisha vijana mnapata mikopo ili muweze kujikwamua kiuchumi”
Akizungumza na viongozi wa UVCCM mkoa wa Iringa Machi 14, 2024, Mohamed kawaida amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kina mpango mzuri na mwema kwa Vijana wote nchini, na UVCCM itawaunga mkono vijana wote watakaojitokeza kugombea katika ngazi ya Udiwani na Ubunge katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi wa Serikali Kuu 2025.
Baada ya kuwasili Mkoani Iringa, Kawaida ameongoza vijana wa UVCCM kushiriki mbio za kawaida za kupasha mwili (Jogging) ndani ya Manispaa ya Iringa kuanzia majira ya saa kumi na mbili asubuhi.
Kawaida yupo mkoani Iringa kwa siku 3 ambapo ataongoza semina na mafunzo kwa viongozi wa UVCCM Vyuo na Vyuo Vikuu Machi 15, 2024, pamoja na kufanya mkutano Mkuu wa Vyuo na Vyuo Vikuu UVCCM Taifa utakaofanyika Machi 16, 2024 maeneo ya Ihemi Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.