Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Operesheni za Amani Jean-Pierre Lacroix, amesisitiza mahitaji ya uungaji mkono mkubwa, endelevu na wa pamoja kutoka kwa nchi wanachama ili umoja huo uweze kutimiza malengo yake makuu ya kulinda amani.
Bw. Lacroix amesema mambo ya ulinzi wa amani na usalama sasa yanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kuongezeka kwa mgawanyiko kati ya nchi wanachama pamoja na utatanishi kwenye migogoro ya sasa duniani.
Ingawa shughuli za ulinzi wa amani sio njia ya miujiza inayoweza kurejesha mara moja utulivu katika nchi fulani , lakini kutokana na juhudi za pamoja za jumuiya ya kimataifa, michakato ya kisiasa na makubaliano ya amani vimeweza kutekelezwa.
Katika maeneo ambapo suluhisho la kisiasa bado halijapatikana, walinda amani wanaendelea kulinda maisha ya mamia ya maelfu ya raia.