Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapher Siyani, amewataka watumishi wa mahakama kutoa haki ili kuwajengea imani wananchi, hivyo kuondoa dhana iliyojengeka kwamba hakuna huduma inatolewa mahakamani bila kutoa rushwa.
Akizungumza jana wakati wa uzinduzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya ya Manyoni, Jaji Kiongozi alisema watumishi wa mahakama wanatakiwa kuwa mabalozi wazuri wa haki kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Watumishi wa mahakama tunao uwezo wa kubadili fikra hizo kutoka kwenye kutokuaminiwa kwenda kwenye kuaminiwa kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa haki lakini bila kufanya hivyo tutazidi kunyooshewa vidole kuwa hatutendi haki,” Siyani
Jaji Siyani alisema watumishi wa mahakama wanatakiwa kujivunia na kujisifu kwa kutoa huduma bora kila mmoja kwa nafasi yake na sio kujisifu kwa vitu vingine kama majengo mazuri na mengineyo.