Mbunge wa Jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani ameiomba Serikali kuiondoa kodi ya asilimia 2 kwa wakulima wa mazao nchini suala ambalo linakwenda kuwaathiri na kuongeza gharama kubwa kwa wakulima.
Akiongea Bungeni jijini Dodoma Mhe. Cherehani wakati akichangia Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 amesema kuwa “Sifa kubwa ya wataalamu ni kutengeneza uchumi na kodi ambayo ni rafiki na sio kuwa na maumivu kwa wananchi hivyo niendelee kukuomba Mhe. Mwenyekiti tuondoe kodi kwa wakulima ili wakalime watengeneze fedha, hakuna mkulima mdogo anayezalisha zaidi ya Milioni 10 kwa mwaka”.
“Ninaliongea suala hili kwa uchungu kwasababu kelele tunazokwenda kuzipata kwa wakulima wetu ni kubwa sana, wakulima wa tumbaku bei ilishuka leo hii imepanda kwasababu Mhe. Rais ametengeneza soko hivyo tulindeni uchumi wa wakulima wetu” ameongeza Mhe. Cherehani.