Papa Francis amesema wakati unaweza fika ambapo atahitaji kuachia ngazi – na atafanya hivyo ikiwa atahisi afya yake ina maana kwamba haiwezi kutumika kama inavyopaswa.
Akihitimisha ziara yake nchini Canada alipo kwenda kuomba msamaha kwa jamii ya watu wenye asili ya taifa hilo, kiongozi huyo wa Kanisa ambaye ana umri wa miaka 85 alisisitiza kwamba kwa sasa ana nia ya kuendelea na majukumu yake – na ataongozwa na Mungu kuhusu lini atang’atuka.
“Sio janga kumbadilisha Papa, na sio mwiko,” aliwaambia waandishi wa habari akiwa kwenye kitimwendo akitoka Arctic Canada akirejea Roma.
“Mlango [wa kustaafu] uko wazi – ni chaguo la kawaida. Lakini mpaka leo sijagonga mlango huo. Sijaona hitaji la kufikiria juu ya uwezekano huu – hiyo haimaanishi kwamba katika muda wa siku mbili huenda nisianze kufikiria juu yake.”
Katika miezi ya hivi karibuni Papa Francis amepata matatizo ya goti ambayo yameathiri uhamaji wake. Alitumia muda mwingi wa ziara yake nchini Canada akiwa kwenye kiti cha magurudumu.
Lakini hapo awali alitupilia mbali uvumi kuhusu magonjwa hatari zaidi, yanayotishia maisha.