Papa Francisko Papa Mkuu wa Kanisa Katoliki la Roma amemfuta kazi Padre Wenceslas Munyeshyaka kutoka katika jimbo la makasisi kwa jukumu lake kubwa katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994 na kuzaa mtoto.
Taarifa inayosambazwa mtandaoni iliyotiwa saini na askofu wa Évreux inasema kwamba Wenceslas Munyeshyaka, 64, “anapoteza moja kwa moja haki za ukasisi” na “amezuiliwa” kutumikia “mahali popote” kama kasisi.
Ofisi ya Dayosisi ya Evreux imeithibitishia BBC uhalisi wa taarifa hiyo ambayo inasema kuwa inatokana na agizo la Papa la Machi.
Bw Munyeshyaka, ambaye alikimbilia Ufaransa baada ya mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994, hajazungumzia uamuzi huo.
Alisimamishwa kazi na Dayosisi ya Evreux mnamo Desemba 2021 baada ya kuibuka kuwa amekiri kisheria kuwa baba wa mvulana wa miaka 10.
Bw Munyeshyaka alitawazwa kuwa kasisi nchini Rwanda mwaka wa 1992 ambapo anatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya mamia ya Watutsi waliokuwa wamekimbilia kanisani kwake katika mji mkuu wa Kigali wakati wa mauaji ya kimbari.
Kanisa Katoliki nchini Rwanda limekuwa likipambana na jukumu lake katika mauaji ya halaiki, ambayo yalisababisha vifo vya Watutsi zaidi ya 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani, kwa miaka mingi. Kanisa hilo limekabiliwa na shutuma kwa kushindwa kufanya zaidi kukomesha mauaji hayo, huku baadhi ya makasisi wakuu wakishutumiwa kuunga mkono mauaji ya halaiki au kushiriki katika mauaji hayo.
Uamuzi wa Papa kumuondoa Munyeshyaka kutoka kwa makasisi umepongezwa na watu wengi wakiwemo manusura wa mauaji hayo ya kimbari. Inatuma ujumbe kwamba wale walioshiriki katika mauaji ya halaiki watawajibishwa kwa matendo yao, bila kujali wadhifa au hali zao.
Mahakama nchini Ufaransa zimemuondolea mashtaka ya mauaji ya halaiki.