Papa Francis aliwasili Papua New Guinea siku ya Ijumaa kutokea Indonesia, ambapo kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 87 wa Kanisa Katoliki duniani ataendelea na ziara kabambe ya siku 12 katika Asia ya Kusini-Mashariki na Oceania.
Ndege ya Garuda Indonesia iliyombeba papa na wasaidizi wake iliwasili Port Moresby, mji mkuu wa Papua New Guinea, ambapo atakaa kwa siku tatu zijazo.
Papa huyo, akiondoka kwenye ndege kwa kutumia kiti chake cha magurudumu, alikutana na Waziri Mkuu James Marape na waumini waandamizi wa Kanisa Katoliki nchini.
Watoto wa eneo hilo walimpa zawadi huku bendi ya kijeshi ikicheza wimbo wa Vatican.
Tukio lake la kwanza la hadhara nchini litakuwa hotuba kwa viongozi wa kisiasa Jumamosi asubuhi.
Akiwa PNG Francis atafanya safari ya siku moja hadi mji wa kaskazini-magharibi wa Vanimo, kabla ya kuondoka nchini Jumatatu. Kisha ameratibiwa kuzuru Timor Mashariki na Singapore kabla ya kurejea Roma mnamo Septemba 13.