MWANANCHI
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alihubiri akiwa katika kiti cha magurudumu na kusema hawezi kuwatupa Mbunge Edward Lowassa na Dk Wilbrod Slaa kwa kuwa ni marafiki zake wa siku nyingi.
Gwajima alisema kumekuwa uvumi kwamba kuhojiwa kwake na polisi kulitokana na kuwakaribisha wanasiasa hao kanisani kwake kwa nyakati tofauti na kuzungumza na waumini wake.
Askofu huyo amesema alifahamiana na Lowassa tangu mwaka 1996 na alifahamiana na Dk Slaa tangu mwaka 1994 kabla hajagombea nafasi ya Urais kupitia CHADEMA, baada ya hapo urafiki wao walikuwa kama familia.
“Hawawezi kunichagulia marafiki, hawa ni watu wangu wa karibu hata kabla hawajawa na ndoto za kugombea urais, nitaendelea kuwa nao karibu,”—Askofu Gwajima.
“Polisi walinihoji mambo mengi binafsi yanayonihusu mimi na hayakuhusiana kabisa na Pengo, maswali ya Pengo yalikuwa machache sana,”—Askofu Gwajima.
Hata hivyo, Gwajima alisema hana ugomvi na polisi wala Serikali kwa kuwa amekuwa akitoa ushirikiano kwa vyombo hivyo.
NIPASHE
Askari wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, PC Charles amejiua kwa kujipiga risasi, baadhi ya wananchi wanaoishi jirani na kituo hicho cha polisi walisema tukio hilo lilitokea Aprili 4 mwaka huu saa 1:00 usiku kituoni hapo.
“Suala hili limetushangaza, kwani sisi tulikuwa nyumbani. Ghafla tulisikia mlio wa bunduki katika kituo cha polisi. Tulipofika, tulimkuta askari huyo akiwa amekufa kwa kujipiga risasi,” alisema Lazaro ambaye ni moja wa mashuhuda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda alithibitisha kujiua kwa askari huyo; “Ni kweli askari huyo amejiua kwa kujipiga risasi wakati akiwa kituoni majira ya saa 1:00 usiku,” alisema Kamanda Kaganda.
Kamanda huyo alisema hakuna ujumbe wowote ulioachwa na askari huyo kuelezea sababu za kujiua na kuwataka askari wote kutatua matatizo yao kupitia viongozi wao badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Alisema uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha askari huyo kujiua.
MWANANCHI
Mtoto Abdul Mohamedi ambaye ni mlemavu wa viungo, amelazimika kuishi darini kwa miezi minne mfululizo kukwepa kudhuriwa na mafuriko kutokana mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Mtwara.
Bibi wa mtoto huyo Zainabu Lipuga alisema jana kuwa alimpandisha darini mjukuu wake Novemba mwaka jana baada ya mafuriko yaliyotekea kipindi hicho.
“Nilipoona mvua zinanyesha nikaona bora nimnusuru mjukuu wangu asisombwe na mafuriko kwa vile sina nguvu za kuweza kumpandisha na kumteremsha mara kwa mara,” alisema Lipuga
Bibi huyo amesema baba wa mtoto hajulikani alipo na jukumu la kumlea limeachwa mikononi mwake bila msaada.
Zaidi ya nyumba 200 zilizingirwa na maji kutokana na mvua kusababisha hasara kwa wananchi ikiwemo kuharibika mali zao zikiwamo nguo na vyakula.
MTANZANIA
Sakata la kufungiwa kwa miaka miwili kwa shindamo la Miss Tanzania limechukua sura mpya baada ya Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo kulirudisha suala hilo BASATA kwa kuandika barua ya kuomba msamaha.
“Tumeandika barua kuomba msamaha BASATA kama tulivyoelekezwa kutoka Wizarani, hivyo tunasubiri majibu..”—alisema Hidan Rico, Ofisa Habari wa Miss Tanzania.
Kampuni ya Lino International Agency ilikata rufaa ya kufungiwa kufanya mashindano hayo ya Miss Tanzania ambayo wao ndio walikuwa waandaaji.
Gazeti la TANZANIA DAIMA walifanya jitihada za kuwapata wahusika wa BASATA wazungumzie kuhusu suala la kuandikiwa barua lakini hakuna mhusika yoyote aliyepatikana.
NIPASHE
Zaidi ya watu 1,600 hawana makazi kutokana na mvua kubwa iliyonyesha Wilaya ya Busega, Simiyu pamoja na kuambatana na upepo mkali ambao umeangusha nyumba hizo.
Mmoja wa mashuhuda ambaye pia ni mmoja wa waathirika wa janga hilo amesema kuwa mvua hiyo ilianza kunyesha kidogo kidogo na baadaye ikaongezeka pamoja na upepo mkali ambao ulipelekea nyumba kuanza kuanguka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa ya Wilaya ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo pia, Paul Mzindakaya amesema tayari ameagiza wananchi waliokumbwa na maafa hayo kuorodhesha ili wapatiwe msaada pamoja na kuwahimiza waishio mabondeni kuhama ili kujiepusha na maafa.
Watu hao waliokosa makazi wameathirika pia kutokana na kukosa chakula na mavazi baada ya mvua kusomba kila kitu.
Kaa karibu na millardayo.com nitakachokipata nitakusogezea hapa muda wowote kuanzia sasa, unaweza kujiunga na mimi kwenye Facebook, Twitter na Instagram pia zitakufikia zote mtu wangu, jiunge nami hapa >>>twitter Insta Facebook