HABARI LEO
“TANGU nilipozaliwa mwaka 1990 sikupata nafasi ya kujiunga na masomo maana familia yetu ilikuwa ya kuhamahama na baba hakuonesha nia ya kunisomesha kabisa”— alianza kusimulia Aisha Ally mama mwenye umri wa miaka 25 na watoto watatu ambao anasoma nao Shule ya Msingi ya Meru, Arusha.
Mama huyo anasoma darasa la tano huku mwanawe Philomena mwenye miaka 9 akisoma darasa la nne, Giftgod (5) akiwa darasa la kwanza pamoja na Thecla (3) ambaye yuko shule ya awali katika Shule hiyo hiyo ya Meru.
Aisha amesema matatizo yaliyoikumba familia yao huko nyuma, yalichangia ashindwe kabisa kuhudhuria masomo na badala yake akajikuta akiolewa na kupata watoto.
Aisha alipanga kuanza darasa la kwanza kabisa lakini walimu wa Shule ya Msingi Meru walimshauri aanzie darasa la nne kwani umri wake ulikuwa mkubwa na pia binti yake mkubwa, Philomena wakati huo alikuwa darasa la tatu kwa hiyo kama angeanza darasa la kwanza, angekuwa amemzidi mama yake kwa darasa moja.
Aisha alisema umbo lake dogo na ufupi wa kimo, vimemsaidia kuonekana kama mwanafunzi wa kawaida kiasi kwamba baadhi ya walimu wasiojua historia yake na wageni, humchukulia kama wanafunzi wengine tu na kumchapa viboko pale anapokosea.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Meru, Mussa Luambo amesema kuna utaratibu maalumu wa kusaidia wanafunzi waishio kwenye mazingira magumu, wakiwemo wale waliokosa elimu utotoni na walimu wameamua kuchangia fedha kutoka mifukoni mwao ili kuwasaidia.
“Wakati mwingine huwa tunachapwa viboko pamoja na maumivu yakizidi mimi na wanafunzi wengine hulia machozi, lakini mama huwa halii kama sisi, tena haogopi wala haoneshi kujali kupewa adhabu”—alisimulia Philomena, mtoto mkubwa wa Aisha.
Aisha amesema kuwa viboko ndio suala linalomkera zaidi shuleni hapo, kama akishachapwa fimbo za mkononi, baadae inakuwa vigumu kwake kufanya kazi za nyumbani za kufua, kuosha vyombo na kupika.
HABARI LEO
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekamata kontena likiwa na rola 15 za nyaya za umeme mali ya TANESCO zenye thamani ya Sh milioni 150.
Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro amesema nyanya hizo ziliibwa Februari 26 zikiwa zinasafirishwa kuelekea Kagera kwa ajili ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambapo baada ya wizi wa kontena hilo, kesi ilifunguliwa Kituo cha Polisi Buguruni na watuhumiwa watano kukamatwa na kufikishwa Mahakamani.
Aliongeza kuwa wakati upelelezi ukiendelea Mei 25 mwaka huu, polisi walipokea taarifa kutoka kwa msiri kwamba maeneo ya Kibamba mtaa wa Kibengewe kuna kontena katika kiwanda cha kutengenezea matofali, askari wakafika katika eneo hilo na kumpata mmiliki wake, askari walifungua kontena hilo na kukuta rola 15 za nyaya.
Polisi wamemkamata na mtu mwingine anayehusika na kontena katika wizi wa kontena hilo, Prosper Mtei ambaye ni mfanyabiashara na upelelezi unaendelea.
NIPASHE
Mbunge Godbless Lema ameongea na watu katika Mkutano Arusha na kuwataka kuwabeba wagonjwa na kwenda nao kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
“Kila mmoja aende lakini usiende peke yako, mchukue na rafiki yako na hata wagonjwa waliolazwa, wabebeni wakajiandikishe… Habari ya mjini sasa hivi ni kujiandikisha kupiga kura, waamsheni vijana wenu, masela nanyi msiende klabu, nendeni kujiandikisha tuing’oe CCM kwa kura”—Godbless Lema.
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Israel Natse alisema watu waliojitokeza kutangaza nia kupitia CCM hawawezi kuoshwa hata kwa waya za chuma za kuoshea sufuria.
“Hata wakioshwa kwa ‘still wire’ hawawezi kuosheka kwa sababu wote ni wachafu.. Tazama wanavyoumbuana, mara utasikia huyu ni kibaka, mla rushwa….” – Israel Natse.
NIPASHE
Stamili Mponzi mkazi wa kijiji cha Ikule Wilaya Kilombero, Morogoro anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumchoma moto mwanae na kumjeruhi mikono kwa madai ya kuiba ugali.
Waliosimulia tukio wamesema unyanyasaji huo ulishuhudiwa na majirani wa mwanamke huyo baada ya kusikia kelele za watoto ambao walimchukua mtoto huyo kumpeleka ofisi ya mtendaji wa kata, baadae wakaenda Polisi na kasha wakaenda hospitali.
Polisi walimkamata mwanamke huyo na mumewe Halidi Kiwenji ambaye inadaiwa alikuwa karibu wakati wa tukio hilo ingawa baadaye baba huyo aliachiwa ili akawaangalie watoto wengine waliobaki nyumbani.
Polisi walithibitisha tukio hilo ambalo uchuguzi unaendelea ili kumfikisha mahakamani mtuhumiwa.
NIPASHE
Mbunge David Kafulila amesema huu ndio wakati wa Serikali iliyopo madarakani kuachia ngazi kwa sababu imeshindwa kudhibiti rushwa na imewekwa mifukoni na mafisadi.
Mbunge huyo amesema nchi imegeuzwa gulio na hata fedha hazina zinatolewa kwa vimemo kutokana na kukosekana kwa utaratibu mzuri.
“Tatizo la nchi hii ni wizi.. Serikalini watu wanapiga mno hela huku uchumi wa nchi unavuja”—David Kafulila.
Kafulila alisema hayo huku akikumbusha sakata la ESCROW kwamba Bunge limetoa hukumu lakini hakuna kitu ambacho Serikali imekifanya mpaka sasa kwa wahusika.
Kafulila alikuwa akichangia mapendekezo ya Wizara ya Maji ambapo alisema Waziri Maghembe amedanganya watu na kumtaka arudi Chuoni kufundisha.
JAMBO LEO
Chama cha CCM kimewapiga marufuku wagombea wake kushiriki katika midahalo kwani inaweza kusababisha vurugu ambapo agizo hilo limekuja muda mfupi baada ya Watendaji Wakuu wa Makampuni Tanzania wakiwa wameandaa mdahalo wa wagombea watano wa Chama hicho ambao utafanyika Dar keshokutwa.
Makada waliotajwa kushiriki katika mdahalo huo ni pamoja na Samuel Sitta, Frederick Sumaye, Balozi Amina Salum, January Makamba, Lazaro Nyalandu na Mwigulu Nchemba.
Katibu wa Oganaizesheni wa CCM, Seif Khatib amesema iwapo makada hao wakishiriki inaweza kusababisha kushambuliana.
“Anayetaka kukuandaa mazungumzo hayo ni lazima awasiliane na Makao Makuu ya CCM”—Seif Khatibu.
Mwenyekiti wa waandaaji wa mdahalo huo, Ali Mafuruki amesema hana taarifa kuhusu Wagombea hao wa CCM kuzuiwa.
MWANANCHI
Jengo la Machinga Complex linatarajiwa kuuzwa kwa wafanyabiashara wa China kwa Bilioni 86 bilioni na Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam baada ya kushindwa kulipa kodi.
Makamu Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Machinga Complex, Gerald Mpangama amesema wamebaini njama za kuuzwa kwa jengo hilo ambalo linasimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
“Tunajua fika kuna kitu kilichofichika nyuma nacho ni suala zima la uuzwaji wa jengo la wafanyabiashara wadogo wadogo la Machinga Complex kwa wachina… hata agenda namba 7 ya kikao cha bodi kilichopita kilizungumzuia suala la uuzwaji wa jengo hili,”– Gerald Mpangama na kuongeza kuwa sababu walizoelezwa za kuuzwa kwa soko hilo ni kwamba linajiendesha kwa hasara.
Mpangama amesema wafanyibiashara hao hawatakubali soko hilo liuzwe na wanajipanga kugoma kupinga uuzaji huo.
Diwani wa Kata ya Upanga, Godwin Mbaga alikana kuhusu taarifa hiyo na kusema kuwa mwenye majibu mazuri ni Halmashauri ya Jiji kwani wao ndiyo waliokabidhiwa kusimamia.
Mkurugenzi wa Jiji, Wilson Kebwe alisema hana taarifa za uuzwaji wa jengo hilo na anazisikia kwa waandishi wa habari.
Unahitaji chochote ninachokipata kisikupite? jiunge na mimi kwenye Twitter, Facebook na Instagram kwa kubonyeza hapa >>> Twitter Insta FB na nitakua nikikutumia kila ninachokipata pia usisahau kusubscribe YouTube kwa kubonyeza hapa >>>Videos ili kila video ya AyoTV ikufikie.