AyoTV

“Hakuna mwenye mimba atakayerudi shuleni” – Rais Magufuli

on

Leo June 22, 2017 Rais Magufuli amekamilisha ziara yake ya kikazi siku tatu katika Mkoa wa Pwani ambako mbali na shughuli nyingine, amezindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona Drink Ltd kabla ya kuzindua kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agric Company na kumaliza kwa kuzindua mradi wa barabara ya Bagamoyo – Msata.

Miongoni mwa mambo aliyoyazungumza kwenye Hotuba yake ni pamoja na suala la elimu akisema Serikali ilitenga fedha kwa ajili ya kugharamia elimu ambayo imeanza kutolewa bure kwa Watanzania wote.

“Nazungumza lingine ambalo tumekuwa tukishughulikia. Tulipoingia madarakani ndugu zangu, na hili nataka nilizungumze kwa sababu pamekuwa na yanazungumzwa mengi. Tuliamua kutenga Bilioni 18.77 kwa ajili ya kutoa elimu bure. Kwamba mtoto ataingia Darasa la Kwanza mpaka Sekondari asome bure.

“Na Serikali tunachukua Bajeti yetu katika hizi fedha kidogo tunazozikusanya tunazipeleka kwenye elimu bure kwa sababu watoto wetu – watoto wa Masikini walikuwa wanapata shida. Akienda shuleni anaambiwa huna ada anarudi nyumbani baadaye hasomi.

“Tukasema hawa watoto wa Masikini, watoto wa Watanzania lazima wasome bure. Sasa pametokea maneno mengine siku hizi nawasikia wanazungumza sana kwamba watoto wanapoenda Shule wakipata mimba akishatoka kuzaa arudi shuleni. Na unakuta hao wanaozungumza sijui nao walipata mimba wakiwa shuleni?

“Nataka niwaeleze, tukienda kwa mzaha wa namna hiyo kwa kusikiliza ma-NGOs yanakotupeleka yanalimaliza Taifa. Mtu ametoka pale amepata mtoto, amezaa, iwe kwa makusudi, iwe kwa raha yake iwe kwa bahati mbaya aende shuleni ameshazaa hawa wengine ambao hawajazaa, si atawafundisha?

“Halafu akipata mimba tena ya pili anaenda nyumbani akizaa tena anarudi shuleni. Anapata mimba ya tatu anaenda nyumba akizaa anarudi shuleni, yaani tusomeshe wazazi?

“Nataka niwaambie, na hizi NGOs na nyinyi wote mnaosikia, ndani ya utawala wangu kama Rais, hakuna mwenye mimba atakayerudi shuleni. Narudia, hakuna mtu mwenye mtoto katika elimu hiyo ya Darasa la Kwanza mpaka Sekondari atakayerudi shuleni.” – Rais Magufuli.

Soma na hizi

Tupia Comments