Bandari ya Tanga kwa mara ya kwanza imepokea Meli ambayo imebeba mzigo wa magari pamoja na shehena nyingine za mizigo kutoka Nchini China.
Meli hiyo ijulikanayo kwa jina la Della imepakia shehena ya mizigo katika Bandari ya Zhanjiangang iliyoko Shanghai, China na kusafirisha mizigo katika Bandari mbalimbali ikiwemo ya Tanga.
Akiongea wakati wa upokeaji wa shehena hiyo ya mzigo Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema ujio wa Meli kubwa za mizigo unatokana na maboresho makubwa yaliyofanyika ya ujenzi wa gati mpya yenye urefu wa Mita 450.
“Hii Bandari ndio moyo wa uchumi wa Mkoa wa Tanga hivyo huu ni mwanzo tuu wa ujio wa Meli kubwa kwani tutaendelea kuvunja rekodi kila mara na niwaombe Wafanyabiashara kuitumia Bandari ya Tanga kwa ajili ya uhakika wa usafirishaji wa mizigo “
Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha amesema kuwa Meli hiyo yenye urefu wa Mita 176 imeweza kutia nanga katika gati na itaweza kuhudumia kwa siku moja pekee–“Uwepo wa vifaa vya kisasa umerahisisha shughuli za upakuaji wa shehena ya mizigo ikiwemo kupunguza muda wa kuhudumia shehena katika Bandari yetu”