Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Afrika lazima ishirikiane katika kuleta mageuzi ya kiteknolojia ili kufanya kilimo cha Kahawa kuwa cha kisasa, chenye tija, na kinachovutia kizazi kipya ili wapate nao kushiriki kikamilifu kukuza uchumi.
Amesema hayo wakati wa kilele cha Mkutano wa Tatu wa Nchi Zinazozalisha Kahawa Barani Afrika tarehe 22 Februari 2025, jijini Dar es Salaam ambapo pia Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo aliongoza kikao cha Mawaziri wa nchi hizo tarehe 21 Februari 2025.
Kwa sasa, takribani asilimia 90 ya mapato ya Kahawa inayouzwa katika soko la nje ya Bara la Afrika yanatokana na Kahawa ghafi. Nchi wazalishaji bado ni waagizaji wa Kahawa kutoka nje, hali inayosababisha upotevu wa fursa za kiuchumi.
Hivyo, Rais Samia alisema kuwa ifikapo mwaka 2030, nusu ya Kahawa inayozalishwa Afrika iuzwe ndani ya Bara la Afrika kabla ya kusafirishwa nje, ili kuongeza thamani ya Kahawa na kuleta faida kwa wazalishaji wa Kiafrika badala ya Mataifa ya kigeni kunufaika zaidi.
“Ili kufanikisha mageuzi haya, Serikali ya Tanzania imechukua hatua madhubuti kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Dola za Marekani Milioni 107.9 mwaka 2021 hadi Dola za Marekani milioni 473.3 mwaka 2024. Hatua hii inalenga kuimarisha Tasnia ya Kahawa kwa kutoa ruzuku, upatikanaji wa mbegu bora, pembejeo za kisasa, na utafiti wa kilimo,” amesema Rais Samia.