Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Waziri Mteule wa Uchukuzi), Prof Makame Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Tanga-Pangani-Saadani-Mkange pamoja na ujenzi wa daraja la Mto Pangani ambapo amesema daraja la muda limekamilika 100%.
Kukamilika kwa daraja hilo la muda kunatoa nafasi nzuri za kuendelea kwa ujenzi wa daraja la kihistoria la Mto Pangani lenye urefu wa Mita 525, litakalounganisha barabara ya Tanga – Pangani hadi Bagamoyo Mkoani Pwani kupitia Saadani (Tanga – Pangani – Saadan – Bagamoyo), barabara zinazojengwa pamoja na daraja hilo vinatarajiwa kupunguza muda wa kusafiri kwenda Jijini Tanga ambapo daraja hilo hadi kukamilika litagharimu Tsh. bilioni 82.19.
Katika ziara yake ameelekeza daraja lijengwe kwa ubora na viwango na ikiwezekana likamilike kabla ya muda wa mkataba December 2025 huku akiwahakikishia Viongozi kuwa awamu ya pili na ya tatu ya mradi zitakwenda vizuri na hakuna changamoto ya fedha, hivyo hakuna sababu mradi ukwame.
Aidha, ameahidi kwa awamu ya kwanza ya mradi kutoka Tanga-Pangani (50kms) watamlipa Mkandarasi ili barabara ikamilike kwa kiwango cha lami, ziara ya Mbarawa ilihudhuriwa pia na Wenyeji wake DC wa Pangani, Zainab Abdallah na Waziri wa Maji ambaye ni Mbunge wa Pangani, Jumaa Aweso.