Wafanyakazi wanawake wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wameadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kuwa na kongamano lililojumuisha wanawake kutoka ofisi za Dar Es Salaam na mikoani pia.
Akizungunza wakati wa maadhimisho hayo mgeni rasmi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Balozi Mwanaidi Maajar amewataka wanawake wa TANESCO kuchapa kazi kwa bidii na kutambua nafasi na wajibu wao kwenye utendaji kazi.
“Naniwaomba tubadilike na tuhakikishe tunakwenda sambamba na mabadiliko ya Teknolojia kwani ndio chachu ya kuleta maendeleo ” alisisitiza Balozi Maajar.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wanawake TUICO TANESCO Makao Makuu, Prisca Maziwa amewataka wanawake kuhakikisha wanatenga muda wa kutosha kwenye malezi ya watoto wao ili kiwajengea msingi wa maisha bora.
Katika hafla hiyo mada mbalimbali zilitolewa na wataalamu kutoka Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto cha Jeshi la Polisi ambaye alizungumzia namna ya kutumia vema dawati la Jinsia na Watoto kuripoti taarifa za unyanyasaji.
Mada nyingine iliyowasilishwa ni matumizi sahihi ya mitandao iliyotolewa na mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na mada inayohusu Saikolojia na Mahusiano iliyotolewa na mtaalamu wa Falsafa na Saikolojia Dkt. Ellie Vdwaminian
Pia katika hafla hiyo wafanyakazi wanawake kutoka Kanda ya Mashariki walinutukiwa vyeti kwa utendaji kazi wao uliotukuka.