Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi hilo, leo Septemba 13, 2024 wamechangia damu kwa wagonjwa wenye uhitaji na kufanya mazoezi ya kutembea katika Jiji la Arusha.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Debora Lukololo amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limetumia maadhimisho hayo kuwakumbuka wagonjwa kwa kuchangia damu kwa wale wenye uhitaji lakini pia kufanya matembezi ya hiari kwa kushirikiana na Wananchi kwa lengo la kufikisha ujumbe kuhusiana na masuala ya uhalifu.
ACP Lukololo ameendelea kufafanua kuwa kilele cha maadhimisho hayo kitaifa kitakua Septemba 17 mwaka huu huko mkoani Kilimanjaro ambapo kwa mkoa wa Arusha walikutana na makundi mbalimbali ikiwemo wanafunzi, bodaboda, nyumba za ibada na vyombo vya habari kwa ajili ya kutoa elimu juu ya wananchi kujiepusha na vitendo vya uhalifu.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Charles Mkombachepa pamoja na kulippngeza Jeshi la Polisi kwa kuchangia damu hiyo, amesema itaenda kusaidia kwa kiasi kikubwa wagonjwa wengi waliopo hospitali ikiwemo wale wa operesheni, wajawazito wanaojifungua, wagonjwa wa ajali na wengine wengi huku akitoa wito kwa jamii kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya kuchangia damu.
Naye Sajenti Fransis Mlay ambaye alichangia damu leo ametoa wito kwa askari wenzake na jamii kwa ujumla kuwa na utaratibu wa kuchangia damu kwani kwa kufanya hivyo wataenda kuokoa wagonjwa wengi ambao wanauhitaji wa damu katika hospitali.
Maadhimisho hayo yanaenda na kauli mbiu ‘’Huduma Bora za Kipolisi kwa Umma zinapatikana kwa kubadilika kifikra, Usimamizi wa Sheria na Matumizi ya TEHEMA’’.