Mamalaka ya Udhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) imeanzisha ofisi za kanda tano nchini na kufikisha jumla ya kanda sita ili kusogeza huduma kwa wananchi waliopo maeneo mbalimbali kwa haraka na kwa urahisi zaidi.
Ofisi za kanda mpya zilizoanzishwa ni Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini na kuungana na Kanda mama ya Pwani ambayo ilikuwepo awali.
Akitangaza uanzishwaji wa ofisi hizo Machi 14, 2024 wakati wa kikao chake na watumishi pamoja na viongozi wa mamlaka hiyo kilichofanyika makao makuu jijini Dodoma, Mkurugenzi wa PPRA, Eliakim Maswi amesema wamefanya uteuzi wa maofisa 15 na watumishi wengine kusaidia kanda hizo kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Amesema wameziwezesha kanda hizo kwa kuteua maafisa 10 kutoka ndani ya PPRA, Maafisa watano kutoka Taasisi nyingine za Serikali, madereva watano na wataalam wa kujitolea (Interns) sita kwa ajili ya kwenda kuanzisha ofisi hizo huku akiahidi kuendelea kuziongezea wataalam kadri watakavyopatikana kwa mujibu wa ikama.
Ameongeza kuwa mamlaka ina matarajio makubwa katika kutatua changamoto mabalimbali za wadau wa mfumo wa NeST, kutoa ufafanuzi kuhusu sheria, kanuni na miongozo ya ununuzi wa umma hapa nchini.
“Ninawaomba muwe wabunifu na kutengeneza uhusiano mzuri katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka. Hii ni awamu ya kwanza na watumishi wengine wanaweza kuhamishiwa katika Ofisi za Kanda kulingana na mahitaji ya eneo au kanda husika,” amesema Maswi
Mkurugenzi huyo amewataka mameneja wa kanda hizo mpya kwenda kuiwakilisha vyema PPRA kwa kufanya kazi kwa ufanisi huku watumishi wa kanda hizo wakitakiwa kushirikiana kwa ukaribu ili kufanikisha malengo ya kanda.
Hata hivyo, Maswi amesisitiza kuwa mara baada ya kupata uzoefu katika makao makuu ya kanda, ni muhimu mameneja wa kanda wakatafuta viwanja kwa ajili ya kujenga ofisi za mikoa yao kwani anaamini kanda hizo zitaendelea kukua na kuwa na mahitaji zaidi.
Kwa sasa, ofisi za baadhi ya Kanda zinapatikana katika majengo mbalimbali ambayo ni jengo la Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Arusha zipo jengo la PSSSF, Mbeya ni jengo la NHIF pamoja na Mtwara jengo la PSSSF.