Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb,) azitaka mamlaka zote zinazohusika kwenye mchakato wa uwekezaji ziondoe urasimu usio wa lazima kiasi cha kuwakatisha tamaa wawekezaji.
Mhe. Prof. Mkumbo ameyasema hayo kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb,) katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha mwongozo wa uwekezaji Mkoani Tanga wenye kauli mbiu Wekeza Tanga kwa Uwekezaji Endelevu.
Mhe. Prof. Mkumbo ameongeza kuwa kongamano hili linaashiria dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kukuza uchumi nchini hivyo uzinduzi huu ni hatua muhimu katika safari ya kujenga taifa linalovutia wawekezaji kutoka pande zote duniani kuja kushirikiana na Mikoa yote nchini.
Prof. Mkumbo amesema kuwa, mfumo imara wa mazingira wezeshi ya uwekezaji ndio uti wa mgongo wa Taifa lolote linalojinasibu katika kufufua na kuimarisha uwekezaji wenye ustawi.
“Katika kutengeneza fursa za ajira, kuimarisha miundombinu na kuinua ubora wa maisha kwa wananchi wake, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitenge maeneo mahsusi na kuyahodhi kwa ajili ya uwekezaji na kuyawekea miundombinu yote muhimu na kuandaa mkakati wa mawasiliano ili kuongeza kasi ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na mipango yote ya uwekezaji izingatie dhamira ya Serikali ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira” Amesema Prof. Mkumbo.
Vilevile, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba amesema kuwa lengo la uzinduzi wa muongozo wa uwekezaji ni kufungua fursa za kilimo, uchumi wa bahari, viwanda, utalii, usafiri, afya, elimu, huduma za fedha, uendelezwaji wa miji na uboreshaji wa maeneo ya michezo.
Mhe. Waziri Kindamba ameongeza kuwa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East African Crude Oil Pipeline) wenye thamani ya dola za kimarekani 3.5 bilioni ni ishara tosha ya dhamira ya Serikali yetu katika kuhakikisha nchi yetu inafanya uwekezaji mkubwa na wenye tija kwa Taifa na wananchi wa kizazi cha sasa na cha baadae.
Mhe. Kindamba amesema kuwa uwekezaji uliofanywa katika kuboresha Bandari ya Tanga uligharimu kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 429.1 ambapo kazi zilizofanyika zilikuwa ni kupanua gati na kuongeza kina na hivyo kuongeza uwezo na ufanisi wa Bandari hiyo kuhakikisha kwamba inaweza kukidhi ongezeko la shughuli inayoendelea ya ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki na shughuli nyingine za kibiashara, kiusafirishaji na kiuwekezaji. Bomba la mafuta linaloanzia Hoima nchini Uganda hadi chongoleani Tanga.
Kongamano hilo limehudhuriwa na Waheshimiwa Mabalozi kutoka Rwanda, Burundi, Uganda na wengine kushiriki kwa njia ya mtandao, Naibu waziri Wizara ya Maliasiri na Utalii Mhe. Danstan Kitandula (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge, Mheshimiwa Nurdin Babu, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na wakuu wa Wilaya, wabunge, makatibu tawala na wakurugenzi wa halmashauri.