Waziri wa Elimu Prosea Adolph Mkenda amesema serikali itahakikisha kuwa kiwango cha usomaji kwa wanafunzi waliopo katika shule ya msingi na sekondari kinaongezeka kwa kuongeza idadi ya vitabu vya ziada,huku akizitaka taasisi na wadau wengine kuunga mkono jitihada hizo ili kufikia lengo.
Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam wakati aliposhiriki kwenye matembezi ya hisani ili kuchangia upatakanaji wa vitabu kwenye shule mbali mbali ili kukuza kiwango cha usomaji kwa wanafunzi,matembezi haya yameandaliwa na chama cha wahasibu wanawake Tanzania (TAWCA).
“Kwa hiki ambacho mnakifanya leo,sisi kama serikali kinakwenda kutusaidia sana kwa sababu kama nchi bado hatujafikia lengo la kuwa na kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja,lengo letu ni kufikia huko ambako tumedhamiria kama nchi,kiukweli mmetushika mkoni katika hili” amesema Profesa Mkenda.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa chama cha wahasibu wanawake Tanzania (TAWCA) Cpa.Tumaini Lawrence,amesema mpango wa taasisi hiyo ni kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali Katika kukuza kiwango cha elimu hasa katika kuimarisha hali ya usomaji kwa wanafunzi nchini.
“Kila mwaka tumekuwa tukiendesha kampeni hii ya vitabu shuleni,tumekuwa tukipeleka vitabu hasa katika shule za serikali kwa sababu huko ndiko ambako tunaamini idadi kubwa ya watoto wetu wanasoma”amesema Cpa.Tumaini