Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumamosi alimpigia simu Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev kuhusu ajali ya ndege ya Azerbaijan Airlines iliyotokea wiki hii huko Kazakhstan, na akatoa pole na rambirambi.
“Vladimir Putin aliomba radhi kwa tukio la kusikitisha lililotokea katika anga ya Urusi na kwa mara nyingine tena alitoa rambirambi zake za kina na za dhati kwa familia za wahasiriwa na kuwatakia ahueni ya haraka majeruhi,” ilisema taarifa ya Kremlin
Kabla ya ajali hiyo, ndege ya abiria ya Azerbaijan ilikuwa imefanya majaribio kadhaa ya kutua katika mji wa Grozny katika Jamhuri ya Chechen ya Urusi wakati ambapo mifumo ya ulinzi ya anga ya Urusi ilikuwa ikijibu kwa dhati shambulio la ndege zisizo na rubani za Ukraine, Putin alisisitiza.
Alimwambia Aliyev kwamba Kamati ya Uchunguzi ya Urusi ilianzisha kesi chini ya Kifungu cha 263 cha Kanuni ya Jinai, ambayo inashughulikia ukiukwaji wa sheria za usalama wa trafiki na uendeshaji wa anga.
“Hatua za awali za uchunguzi zinaendelea, huku wataalamu wa kiraia na kijeshi wakishauriwa,” iliongeza taarifa hiyo.
Siku ya Jumatano ndege ya shirika la ndege la Azerbaijan kutoka mji mkuu wa Azerbaijan Baku hadi Grozny ilianguka karibu na mji wa Aktau, Kazakhstan, na kuua watu 38 na kuwaacha manusura 29 kati ya 67 waliokuwa ndani.