Rais wa Urusi Vladimir Putin, wakati akizungumza katika ufunguzi wa mkutano kati ya taifa lake na bara Afrika mjini St Petersburg, amesema anahitaji kuona umoja wa Afrika (AU) ukipewa nafasi ya uanachama wa kudumu katika muungano wa mataifa ya G20.
Putin amesema wanatumai kuwa uamuzi huo utafanywa mapema Septemba, wakati wa mkutano wa kilele wa G20 huko New Delhi.
Akizungumzia kuhusu hatua ya nchi yake kujiondoa kwenye mkataba ulioidhinishwa na umoja wa mataifa wa kuruhusu usafirishaji wa nafaka kutoka bandari za kusini mwa Ukraine, na hatimaye kuelekea Afrika, Putin amesema kuwa Urusi inaweza kuziba pengo hilo.
Aliongeza kuwa Urusi itatoa nafaka bila malipo kwa nchi sita za Afrika katika miezi michache ijayo.
Idadi ndogo ya viongozi wa bara Afrika wanashiriki katika mkutano huo kuliko ilivyokuwa katika mkutano wa kwanza.
‘Tunaunga mkono ushiriki wa Muungano katika kazi ya kuongoza vyama vya kimataifa na ningependa kuwakumbusha kwamba Urusi ilikuwa mojawapo ya nchi za kwanza kuitikia vyema mpango uliotolewa na Rais wa Senegal, aliyekutangulia katika nafasi hii, wa kuupa Umoja wa Afrika uanachama kamili katika G20. Tunatumai kuwa uamuzi huo utapitishwa katika mkutano wa kilele wa G20 huko New Delhi mnamo Septemba’.
‘Kama hapo awali, Urusi iko tayari kusaidia kuimarisha uhuru wa nchi za Kiafrika na kuchangia Afrika kuwa mshirika mkuu katika mfumo mpya wa mpangilio wa ulimwengu wa nchi nyingi’.
‘Tutayapa kipaumbele masuala haya katika mkutano huo unaofunguliwa leo. Pia tutajadili maamuzi ya vitendo kuhusu kujenga ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi, kuhakikisha usalama wa chakula na nishati, na kuendeleza mifumo ya afya ya kitaifa’.
‘Kupitishwa kwa mpango wa tamko la Mkutano wa pili wa Urusi-Afrika na mpango wa utekelezaji wa Umoja wa Urusi-AU kwa 2023-2024 kutasaidia kuzindua juhudi za vitendo katika maeneo yaliyotajwa hapo juu na mengine mengi’.