Suluhu ya kudumu nchini Ukraine “haiwezekani” bila kushughulikia suala pana la usalama wa Ulaya, Kremlin ilisema Jumanne, wakati Marekani na Urusi zikifanya mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu tangu mashambulizi ya Moscow dhidi ya Kyiv.
Kabla ya kuanza mashambulizi yake mnamo Februari 2022, Moscow ilikuwa imeitaka NATO kujiondoa kutoka Ulaya ya kati na mashariki.
“Utatuzi wa kudumu na wa muda mrefu hauwezekani bila kuzingatia kwa kina masuala ya usalama katika bara,” msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisema, akijibu swali la AFP.
Pia alisema Moscow haitaizuia Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya alirudia kusema kwamba bado inapinga Kyiv kuwa sehemu ya NATO.
Ingawa hakuweza kutoa tathmini kuhusu hali ya sasa ya mazungumzo, Peskov alisema mazungumzo ya leo yanaweza kuleta “uwazi zaidi” juu ya uwezekano wa mkutano wa ana kwa ana kati ya Donald Trump na Vladimir Putin.
“Putin amesema mara kwa mara yuko tayari kuzungumza juu ya amani”, alisema, akisisitiza Urusi inataka kufikia malengo yake lakini ingependelea kufanya hivyo “kwa amani”.
Ilipoulizwa kama Ukraine inaweza kujiunga na Umoja wa Ulaya, Peskov ilisema: “Hii ni haki ya uhuru wa nchi yoyote, hatutaamuru.”