Top Stories

Hakimu aliehukumu watu kifungo cha maisha aanza upya kesi ya Mbowe na Viongozi CHADEMA

on

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko wamefika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza wakitokea uraiani baada ya kusota mahabusu takribani miezi 3.

Mbowe na Matiko sambamba na Viongozi wengine 7 wa chama hicho wamefika mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili.

Wakili wa Serikali, Wankyo Simon alimueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo kwamba kesi imeitishwa kwa ajili ya kusikilizwa.

Hata hivyo Hakimu Simba alisema kiutaratibu inapaswa washtakiwa wakumbushwe mashtaka yao kwa sababu kesi hiyo ilikuwa kwa Hakimu mwingine Wilbard Mashauri ambaye ameteuliwa kuwa Jaji.

Wakili Wankyo aliwasomea upya washtakiwa mashtaka yao ambayo ni 13 ikiwemo uchochezi ambapo wote walikana.

Hakimu Simba ambaye hivi karibuni aliwahukumu watu kifungo cha maisha kwa kuchoma moto kituo cha Polisi Bunju A, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 29, 2019 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Mbali na Mbowe na Matiko, wengine ni Mbunge wa Iringa mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu ambao wote walikuwepo mahakamani.

Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, mwaka 2018 maeneo ya Dar es Salaam.

MABORESHO ZIWA VICTORIA YANAYOFANYWA NA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Soma na hizi

Tupia Comments