SERIKALI imesema imetenga jumla ya shilingi bilioni 70 kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba ili kumaliza tatizo la ukosefu wa dawa nchini.
Aidha imetenga jumla ya shilingi bilioni 85 kwa ajili ya kupunguza deni linalodaiwa na bohari ya dawa MSD lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya zenye ubora.
Akifungua mkutano mkuu wa waganga wakuu wa mikoa na wilaya zote nchini leo mjini Dodoma makamu wa rais mama SAMIAH SULUHU HASSAN amesema dawa hizo zitakazonunuliwa zitaenda moja kwa moja katika vituo vya afya vilivyopo hapa Nchini.
Amesema lengo la serikali ni kupunguza changamoto zilizopo katika sekta ya afya huku akiweka bayana dhamira ya serikali ya kujenga kiwanda cha Dawa katika mkoa wa Simiyu.
Mbali na hilo amezungumzia suala la tiba asili na tiba mbadala na kuitaka Wizara ya Afya maendeleo ya jamii,jinsia,Wazee na Watoto kuhakikisha wanazipa umuhimu kwa kuzitambua na kuzisajili.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Waganga hao dokta SUDI LEONARD ameiomba serikali kutatua tatizo la dawa na vifaa tiba lililopo nchini ambalo limekuwa likisababisha malalamiko na manung`uniko kwa wananchi hasa kwa makundi maalum kama wajawazito,watoto,wazee na wenye magonjwa sugu.
Mkutano huo ni wa siku nne wenye lengo la kujadili kwa pamoja masuala mbalimbali yahususyo afya na ustawi wa jamii,kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kutatua changamoto zilizopo ukibeba kauli mbiu isemayo mfumo na huduma bora za afya ni nguzo muhimu kuelekea Tanzania yenye viwanda na uchumi wa kati.
Unaweza ukabonyeza play kumsikiliza Makamu wa Rais Samia Suluhu