Serikali imesema inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini ambapo katika mwaka huu wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha Tsh. Bilioni 100.
Kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 62 kwa Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi, aidha, Wilaya ya Manyoni ni miongoni mwa Wilaya hizo 62 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi kwa mwaka huu wa fedha.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda amesema hayo leo tarehe 21 Septemba 2022 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo Manyoni Mashariki aliyetaka kufahamu Serikali ina mpngo gani wa kujenga Chuo cha VETA Wilayani Manyoni.
Waziri Mkenda amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha 2022/23, Serikali imetenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 62 kwa Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi.