Mshambuliaji wa AC Milan, Rafael Leão amewachana watu “wenye mawazo finyu” baada ya kuwa mwathirika wa hivi karibuni wa ubaguzi wa rangi, huku tatizo hilo likiendelea kusumbua soka la Italia.
Leão alishiriki moja ujumbe kwenye Insta story yake kutoka kwa mtumiaji wa mtandao wa kijamii ambaye alimwandikia kwa Kiitaliano: “Siwezi kuvumilia kukuona tena. Siwezi kuvumilia tena kukuunga mkono uwanjani. Ninakuwa mbaguzi wa rangi… Ondoka haraka, wewe na wafuasi wako”.
Leão, 24, aliyajibu maoni kuhusu suala hilo kwa Kireno:akisema “Kwa bahati mbaya, daima kuna aina hii ya watu wenye mawazo finyu duniani.”
Tukio hili jipya la ubaguzi wa rangi katika soka ya Italia linakuja mwezi mmoja baada ya Leão kuondoka uwanjani na wachezaji wenzake wengine wa Milan baada ya kipa wa Rossoneri, Mike Maignan, kuathiriwa na matusi ya kibaguzi dhidi ya Udinese. Wafuasi hao walitambuliwa haraka na kupigwa marufuku maisha na Udinese.
“Tuko pamoja nawe Rafa,” Milan alisema katika ujumbe kwenye X. “Katika kundi letu la wafuasi na katika soka hakuna nafasi ya ubaguzi wa rangi.”
Matukio mengi ya ubaguzi wa rangi yametokea katika soka ya Italia na Ulaya kwa miaka mingi, na wahasiriwa nchini Italia kama vile Kevin-Prince Boateng, Mario Balotelli na Romelu Lukaku.
Mwezi uliopita, Lazio iliadhibiwa kwa kufungwa kwa sehemu ya uwanja kwa nyimbo za ubaguzi wa rangi dhidi ya Lukaku.