Rais wa Ghana anayeondoka Nana Akufo-Addo ameidhinisha raia kutoka nchi nyengine za Afrika kuingia nchini humo bila masharti ya viza.
Uidhinishaji huo unaifanya Ghana kuwa mojawapo ya mataifa machache ya Afrika-pamoja na Rwanda, Seychelles, Gambia, na Benin kuruhusu wananchi wenye hati za kusafiria kutoka mataifa mengine ya Afrika kuingia bila viza.
Uamuzi huu unatimiza ahadi iliyotolewa na Rais Akufo-Addo wakati wa Mazungumzo ya Mafanikio ya Afrika (APD 2024) mnamo Januari 2024.
“Wengi wenu ilibidi kupata viza ili kuhudhuria tukio hili,” alisema katika mkutano huo, akiongeza kuwa “Serikali ya Ghana imejitolea kuhakikisha usafiri bila viza kwa Waafrika wote, na mchakato umeanza kutekeleza sera mwaka huu.”
Mpango huo unalenga kukuza usafiri huru wa watu, bidhaa na huduma kote barani Afrika, na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi chini ya Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA).
Sera ya kutotumia viza inatarajiwa kuanza kutumika kabla ya muda wa Rais Akufo-Addo kukamilika Januari 6, 2025.