Raia kutoka Nigeria wamehukumiwa kifungo cha jela nchini Uingereza baada ya kupatikana na hatia ya kufoji hati zaidi ya 2,000 za ndoa kwa ajili ya kuhamasisha uhamiaji haramu. Watu hao walihukumiwa katika Mahakama ya Woolwich Crown Court jijini London.
Majina yao ni Abraham Alade Olarotimi Onifade (41), Abayomi Aderinsoye Shodipo (38), Nosimot Mojisola Gbadamosi (31), na Adekunle Kabir (54). Wote walihukumiwa kwa makosa yanayohusiana na udanganyifu na kupotosha hati za kisheria ili kurahisisha maombi ya uhamiaji haramu kwa kutumia hati za ndoa za uongo.
Onifade, ambaye ni kutoka Gravesend, Kent, na Shodipo, kutoka Manchester, walihukumiwa kifungo cha miaka sita kwa kuhusika na kuhamasisha uingiaji haramu nchini Uingereza na kutoa hati za uongo. Gbadamosi, kutoka Bolton, alihukumiwa miaka sita kwa udanganyifu, huku Kabir, kutoka London, alipokea kifungo cha miezi tisa kwa kosa la kumiliki hati ya utambulisho kwa nia mbaya.
Paul Moran, Mkuu wa Idara ya Uhamiaji katika Ofisi ya The UK Home Office, alisema, “Tutaendelea kufanya kazi kwa bidii kulinda mipaka yetu na kubomoa makundi ya uhalifu yanayotumia watu dhaifu kwa faida.”