Rais wa Misri Abdul Fattah al-Sisi anatarajiwa kuapishwa kwa muhula wa tatu mfululizo wa miaka sita kama kiongozi wa nchi hiyo.
Alichaguliwa tena Desemba kwa 89.6% ya kura zote, akiwashinda wagombea wengine watatu.
Sherehe za kuapishwa kwake zitafanyika Jumanne katika majengo mapya ya bunge karibu na mji mkuu, Cairo, gazeti linalomilikiwa na serikali Al-Ahram liliripoti.
Bw Sisi, 69, alianza kuwa rais mwaka wa 2014, mwaka mmoja baada ya kuongoza jeshi kumpindua mtangulizi wake Muislamu Mohammed Morsi.
Anasifiwa kwa kutekeleza miradi kadhaa mikubwa ya miundombinu wakati wa uongozi wake, lakini pia amekosolewa kwa uchumi mgumu unaotokana na kulemaa kwa deni na mfumuko wa bei uliokithiri.
Pauni ya Misri imepoteza zaidi ya 50% ya thamani yake dhidi ya dola ya Marekani, na kusababisha mgogoro mkubwa wa gharama za maisha.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu pia yamemshutumu Bw Sisi kwa kuwakandamiza wakosoaji.