Rais wa Marekani Joe Biden ametoa agizo la kuidhinishwa kwa vikwazo dhidi ya Sudan, akisema mapigano lazima yaishe.
Bw Biden ameziita ghasia zinazoendelea nchini Sudan maafa na usaliti kwa watu wa Sudan.
Amesema ghasia nchini Sudan “ni tisho lisilo la kawaida kwa usalama wa taifa na sera ya kigeni ya Marekani”.
Awali, Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani, Avril Haines, aliiambia kamati ya seneti kwamba mzozo huo unaweza kuendelea kwa muda mrefu, kwani pande zote zinaamini kuwa zinaweza kushinda kijeshi na haziko tayari kwa mazungumo.
Muda wa usitishaji mapigano wa sasa umeshindwa kuheshimiwa , huku mapigano makali yakiendelea katika mji mkuu Khartoum, pamoja na miji jirani ya Omdurman na Bahri.
Shirika la mpango wa chakula duniani WFP linakadiria kuwa takriban msaada wa thamani ya dola milioni 13 (£10.3m) wa chakula uliokuwa ukipelekwa Sudan umeporwa tangu mapigano yalipoibuka mwezi uliopita.
WFP linasema uporaji umekithiri nchini humo.
Shirika la Umoja wa mataifa la watoto, Unicef, lilionya kuwa hali inaelekea kuwa janga, huku watoto wakiendelea kuuliwa katika mashambulio.