Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi, pamoja na ujumbe wake, ametembelea Kiwanda cha INDESSO cha kusarifu majani ya mkarafuu na kutengeneza mafuta kwa matumizi mbalimbali kama vile dawa na manukato, kilichopo Cileungsi, Jakarta, Indonesia.
Akiwa katika kiwanda hicho, Rais Dk. Mwinyi amejionea hatua mbalimbali za kusarifu majani ya mkarafuu pamoja na shughuli nyingine zinazofanywa na kiwanda hicho.
Akitoa maelezo mbele ya Rais Dk. Mwinyi, Bw. Robby Gunawan, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, amesema kuwa Indesso imepiga hatua kubwa za mafanikio tangu kuanzishwa kwake Pemba mwaka 2019 kwa kujenga vinu 8 vya kusarifu majani ya mkarafuu pamoja na kukuza uchumi kwa kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi wa Zanzibar kupitia vinu hivyo.
Katika ziara hiyo, Rais Dk. Mwinyi ameambatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Mhe. Macocha Moshe Tembele, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Mhe. Saada Mkuya Salum, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Mhe. Sharif Ali Sharif, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Mhe. Dkt. Khalid Salum Mohamed, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mhe. Shaabani Ali Othman, na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Cosato David Chumi pamoja na Wakuu Taasisi mbalimbali za SMZ na SMT.