Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy (2007-2012) amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na Mahakama ya Paris baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya ufadhili wa kampeni yake ya Urais ya mwaka 2012.
Sarkozy anatuhumiwa kutumia karibu mara mbili ya kiwango cha fedha kinachoruhusiwa kisheria ikiwa ni kiasi cha Euro milioni 22 na nusu katika kampeni yake ya kugombea muhula wa pili wa Urais katika uchaguzi alioshindwa na Francois Hollande.
Hukumu hii imetolewa wakati ambapo Sarkozy mwenye umri wa miaka 66 alikata rufaa baada ya kukutwa na hatia nyingine March 2021 katika kesi ya ufisadi ambapo alidaiwa kumuhonga Jaji ili apate taarifa za siri kuhusu kesi ya uchunguzi dhidi yake ambapo alihukumiwa miaka mitatu jela katika kesi hiyo lakini miwili ilifutwa akabakiwa na mmoja ambao bado hajaanza kuutumikia gerezani.
Hata hivyo Sarkozy huenda akaepuka kwenda jela kwa hukumu hii mpya kwani Jaji aliyetoa hukumu hiyo amesema Sarkozy anaweza kutumikia kifungo cha nyumbani japo atavishwa kifaa maalum cha kieletroniki cha kumfuatilia.